SWALI: Kitabu cha Mathayo 27:44 na Marko 15:32b inazungumzia wale wanyang’anyi walioteswa pamoja na Yesu kuwa wote wawili walimtukana Yesu pia, ila tukisoma Luka 23:39 inasema ni mmoja ndiye alimtukana sasa kwanini inakuwa hivyo naomba unisaidie nielewe?.
JIBU: Tuvipitie vifungu vyenyewe;
Mathayo 27:44 “Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
Marko 15:32 Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.
Luka 23:39 “Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. 40 Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? 41 Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. 42 Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. 43 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”.
Luka 23:39 “Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.
40 Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?
41 Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.
42 Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.
43 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”.
JIBU: Ukisoma juu juu ni rahisi kusema maandiko yanajichanganya, lakini hakuna kinachojichanganya isipokuwa ni sisi wenyewe tunakosa shabaha ya kuyaelewa maandiko.
Habari hii inafanana na ile, ya wale watu wawili ambao Yesu alikutana nao kule makaburini wenye pepo, ukisoma pale utaona injili moja inaonyesha Bwana alikutana na vichaa wawili, wakati injili nyingine inaonyesha alikutana ni kichaa mmoja, Sasa habari hizo sio kwamba zinajichanganya, hivyo Ili kupata ufafanuzi wake basi fungua hapa >>> Wenye pepo
Sasa tukirudi kwenye habari hiyo tunaona Injili ya Mathayo na Marko inaonyesha kuwa wale wahalifu wawili walimdhihaki Bwana Yesu akiwa pale msalabani, bila upingamizi wowote . Lakini Injili ya Luka inaonyesha mmoja ndiye aliyemtukana lakini yule mwingine alimwomba rehema.
Kabla hatujalijibu swali, Tukumbuke kuwa Bwana Yesu alikuwa pale msalabani kwa muda mrefu sana usiopungua masaa 6, na wakati huo wote, wale wahalifu waliosulibiwa naye walikuwa wanautazama mwitikio wake, alipokuwa katika hali kama ya kwao, ni wazi kuwa mwanzoni wote walidhani Yesu ni kama mmojawapo wa wahalifu wenzao, na hiyo haikuwa shida wote kutoa kauli za kudhihaki na kukebehi na ndio maana injili ya Mathayo na Marko zinaonyesha kuwa wote walimkebehi..
Lakini ni wazi kuwa baadaye kidogo yule mmoja alitubu, akageuka, na hiyo ni pengine baada ya kuona utofauti wa Yesu na matendo aliyokuwa anayaonyesha pale msalabani, alipoona aliposhutumiwa hakurudisha majibu, alipoona anawaombea msamaha, akisema Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo, pengine hilo lilimgusa sana, alipoona upendo wake wa kipekee, japokuwa alikuwa matesoni..Hilo ndilo lililomfanya yule muhalifu mmoja ageuze mtazamo wake na kujua kabisa Kristo hakuwa na kosa lolote..
Na zaidi ya yote alipoona mpaka giza limeingia mchana kweupe, jambo ambalo si la kawaida.. Alitubu saa ile ile na mpaka kumwambia yule wenzake sisi ni kweli tumekosea, lakini huyu hakufanya kosa lolote linalomstahili yeye kuuawa. Ee Yesu unikumbuke katika ufalme wako.
Ni kitu gani tunajifunza?
Hiyo inatuonyesha uvumilivu wa Mungu jinsi ulivyo kwa wenye dhambi. Hata wewe mwenye dhambi Inawezekana umekuwa ukimdhihaki Mungu mara nyingi, ukizipuuzia njia zake na kuziona ni za watu waliorukwa na akili mara nyingi, hata umefikia hatua ya kuutukana wokovu waziwazi na Mungu mwenyewe., lakini bado Mungu anakupa nafasi ya kutubu leo. Lakini nafasi hiyo haitadumu milele. Kumbuka wahalifu wale wote walikufa baada ya muda mfupi, lakini mpaka sasa tunaongea mmoja yupo peponi mwingine yupo motoni.
Yule aliye motoni alipuuzia wokovu mpaka dakika ya mwisho hakujua kuwa hana muda mrefu wa kuishi. Swali ni Je! Wewe pia unatambua muda uliobakiwa nao hapa duniani? Kama hufahamu ni kwanini basi bado upo kwenye dhambi? Hivyo tubu leo Yesu akuokoe akuoshe dhambi zako, ufanyike mtoto wake kweli kweli. Hizi ni nyakati za mwisho. Majira haya ni ya kumalizia. Hivyo usiruhusu, dhambi iendelee kuwa sehemu ya maisha yako.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?
Wevi na wanyanga’anyi waliomtangulia Yesu walikuwa ni wapi?
TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.
USIIGEUZE NYUMBA YA MUNGU KUWA PANGO LA WANYANG’ANYI.
UFUNUO: Mlango wa 11
Rudi Nyumbani:
Print this post