by Admin | 29 September 2022 08:46 pm09
SWALI: Naomba kufahamu mstari huu unamaana gani?
Mhubiri 4:4 “Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo”.
JIBU: Sulemani ni mtu ambaye alipewa na Mungu uwezo wa kutambua hekima ya mambo yote yanayotendeka huku duniani.. Na moja ya jambo ambalo aliliona na kutolea habari zake ni kuhusiana na chanzo cha mafanikio mengi ya watu ni nini?.. Na ndio hapo anasema..
“Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake”.
Kwamba kila utajiri, au kazi za ustadi, yaani nyumba nzuri, magari mazuri, mavazi mazuri, hatua zote za mafanikio, asilimia kubwa hutokana na mtu kupingana na mwenzake, kwa tafsiri iliyo nzuri ni kwamba hutokea mtu kushindana na mwingine..ambacho chanzo chake ni wivu.
Kwamfano, mtu atasema mbona Fulani amenunua gari, mimi sijanunua, ngoja nikakope pesa nifanye kazi juu chini na mimi mwaka huu ninunue la kwangu zuri kuliko lile.. Sasa mtu kama huyu atapata gari kweli, lakini chanzo cha gari lake sio malengo yake, bali ni kwasababu wenzake wanayo magari yeye hana.
Hata mashirika makubwa, kufanikiwa kwao ni kwa mashindano, utaona kampuni moja la simu limetoa ofa hii, kesho lingine linaiga ofa ile ile na zaidi, ili lisipoteze wateja.. Hivyo yamefanikiwa kwa njia hizo hizo, za mashindano.
Tajiri mmoja atashindana na tajiri mwenzake ili awe namba moja, hivyo atafanya kazi kwa bidii usiku kucha, ili asishindwe na mwenzake, watashindana kibidhaa n.k.. Mchungaji mmoja atashindana na mchungaji mwingine kwa wingi wa washirika, au kwa ukubwa wa kanisa,
Sasa hayo yote Sulemani ameyaona na kusema ni ubatili, ni sawa na kujilisha(kuufuata) Upepo. Maana yake ni kuwa mafanikio yanayokuja kutoka katika wivu, au mashindano, hayana afya yoyote kiroho.
Hii inatufundisha nini?
Wafilipi 2:14-15 inasema..
“14 Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano,
15 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu”
Kama watakatifu, hatupaswi kutafuta kitu chochote kwa kushindana, utasema mwenzangu ana neema kubwa kama ile, ngoja na mimi nikafunge na kuomba nimpite,. Hapana, bali tunapaswa tuishi kwa kumtazama Mungu,kila mmoja katika nafasi yake aliyopewa na Mungu, na kuitendea bidii hiyo, kwasababu kwa kupitia hiyo ndio Mungu atatufanikisha, na sio kwa neema za wengine..
Bwana atubariki.
Shalom.
Tafadhali share na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Amali” na “Ijara” katika biblia?
Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri.
Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe;(Mithali 16:2)
Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)
Mego ni nini kama tunavyosoma katika biblia? (Mithali 17:1)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/09/29/inatokana-na-mtu-kupingana-na-mwenzake/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.