Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

by Admin | 20 September 2022 08:46 pm09

Kwa tafsiri za kidunia mtu asiye na akili ni mtu ambaye hawezi kufiriki, kuelewa, kuwasiliana, kupanga au kutatua matatizo. Hivyo, mwanadamu mwenye mtindio wa ubongo, anajulikana kama hana akili, mtu anayefeli darasani, anajulikana kama hana akili, mtu anayeshindwa na wenzake katika maisha anajulikana pia kama asiye na akili.

Lakini je! Biblia nayo inasemaje kuhusiana na mtu asiye na akili. Sifa zake ni zipi.

Zifuatazo ndizo sifa za mtu asiye na akili mbele za Mungu, ikiwa wewe unayo mojawapo au zote, basi fahamu huna akili, haijalishi utakuwa ni wa kwanza, kimaisha, au kielimu, au kicheo. Mungu anakuona unao mtindio wa ubongo, hujakamilika. Na matokeo yake utashindwa kutumia akili zako zote kumpenda yeye kama alivyotupa maagizo katika ‘Mathayo 22:37’

1) Kutomtafuta Mungu:

Zaburi 14:2 “Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. 3 Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja”.

Ukishaona Mungu hana umuhimu kwako, ni uthibitisho tosha,akili zako zimepunguka kwa kiasi kikubwa mno. Ni sawa, na mbwa asiyemjua bwana wake anayemfuga siku zote. Au mtoto asiyemtambua mama yake amnyonyeshaye kila siku. Fanya bidii kumtafuta Muumba wako, kwasababu hilo ndio jaribio la kwanza alilotuumbia Mungu, ili kuthibitisha kwamba kweli sisi ni wanadamu tuliokamilika, tunaweza kumtafuta aliyetubuni.?

2) Kuwadharau wengine:

Mithali 11:12 “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza”.

Ukishajiona wewe ni bora kuliko mtu mwingine, au unamwona mwenzako hana lolote jipya la kukufaa wewe, tambua kuwa tayari akili yako imeathirika, fanya haraka sana, kujirekebisha katika eneo hilo, ili usipoteze upeo wako wa kufikiri vema, na wa kupambanua mambo. Kamwe usimdharau mtu yeyote duniani. Hata kama ni mpumbavu wa mwisho.. Kwasababu Mungu naye hamdharau mtu aliyemuumba  japokuwa ni mnyonge (Ayubu 36:5)

3) Kuwaonea watu:

Mithali 28:16 “Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake”.

Kumuonea mtu kwasababu ya unyonge wake, au udhaifu wake, ni jambo la hatari sana. Ukimdhulumu mwenzako, au kumnyima haki yake, au kutumia hila kumwibia kisa tu hana maarifa ya jambo hilo, kumpiga mkeo, au watoto bila sababu, basi fahamu kuwa wewe ni sawa ni mjinga mbele za Mungu.. Tukae mbali na uonevu wa aina yoyote.

4) Kufanya uasherati:

Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Uzinzi, ni kipingamizi sio tu cha kiroho, bali pia cha kiakili. Watu wazinzi, wanajiharibia sana uwezo wao wa kupambanua mambo ya kiroho kwa sehemu kubwa sana. Kwasababu Roho Mtakatifu huwa anategemea miili yetu kutenda kazi, hivyo mwili wako unapochafuliwa, hawezi kupata nafasi ya kuwa mwalimu wako. Ndio hapo Unabaki tu kuwa wewe kama wewe, kama mnyama tu. Epuka uzinzi kwa gharama zote, ni hatari..

5) Kutokuwaza  juu ya hukumu:

Mithali 15:24 “Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini”.

Hapo biblia inatueleza wazi, mtu mwenye akili, huwaza ni jinsi gani atakavyoepukana na kuzimu iliyo chini, huwaza kwenda mbinguni, huwaza kuepukana na ziwa la moto. Lakini kinyume chake ni kweli, mtu asiyewaza hatma ya maisha yake baada ya kufa itakuwaje, badala yake yupo tu, anachowaza ni ajengeje magorofa hapa duniani, ukimweleza habari za kuzimu hata hashtuki, huyo kwa Bwana hana akili.

6) Kutopenda maagizo:

Mithali 10:8 “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka”

Ukiwa ni mtu wa kupinga maagizo mema, unayopewa, bali unajiona upo sawa machoni pako mwenyewe, ukielezwa, uvaaji vimini ni dhambi, unasema hatupo agano la kale, unapoelezwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ni lazima, unasema sisi hatuamini hilo. Ujue kuwa unajiangamiza mwenyewe. Kila agizo lililo kwenye Neno la Mungu linapaswa lipokelewe na kukubaliwa kama lilivyo pasipo kuuliza uliza.

7) Kusahau sahau, sheria za Mungu:

Mithali 10:14 “Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu”.

Ukiwa mtu wa kutozingatia, au kutotendea kazi kile unachoambiwa au kukisikia, kuhusiana na mafundisho ya adili, yaani unasahau sahau, amri au fadhili za Mungu, unakuwa mwepesi kuanguka ovyo katika dhambi, ni uthibitisho kuwa huna akili kwa mujibu wa kibiblia. Tunapaswa tuwe watu wa kuzitafakari sheria za Mungu wakati wote, kama vile mwanafunzi akaririvyo kila siku masomo yake, ili yamsaidie kufaulu mitihani yake ya mwisho.

Mithali 3:3 “Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu”.

8) Uvivu:

Mithali 24:30 “Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake”.

Ukiwa mvivu, wa kufanya kazi ya Mungu.  Bwana anasema huna akili, yaani Ikiwa hujishughulishi na chochote, unajitafutia matitizo yako mwenyewe. Tumeumbwa, tujishughulishe, kama Mungu alivyojishughulisha..Kama huwezi mtumikia Bwana kwa kujitoa kwa asilimia zote kwenye kazi yake, ni lazima ufanye kazi ya mikono, ili ufanikiwe. Lakini tukishindwa kujishughulisha, ni kwa hasara yetu wenyewe.

Hivyo tukiwa tuna mojawapo ya tabia hizo ni busara tukazidhibiti ndani yetu. Ili tuweze kuishi kwa akili Bwana anazotaka tuwe nazo.  

Zingatia: Mungu anazungumza na mtu mwenye akili timamu, rohoni. Ni lazima tufikie hapo ili Bwana aseme na sisi.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mpumbavu ni nani katika biblia? (Zaburi 14:1, Mithali 10:14)

Kutia mkono chini ya paja kama ishara ya kiapo, kulimaanisha nini?

Watu wenye ulemavu wa akili, wataenda mbinguni?

Nini maana ya ‘Hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma’?

HAKUVAA NGUO SIKU NYINGI.

NI NINI BWANA ANATAZAMIA KILA TUNAPOSHIRIKI MEZA YAKE.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/09/20/mtu-asiye-na-akili-ni-nani-kibiblia/