NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

Shalom, karibu tuyatafakari maandiko.

Bwana Yesu ameruhusu miujiza itokee kwenye maisha yetu kwa malengo makuu mawili (2), Lengo la Kwanza ni ili SISI TUPATE FAIDA (TUNUFAIKE) na lengo la pili; ni ili TUTUBU.

Wengi wetu tunalijua hili lengo la Kwanza, na ndilo tunalolitafuta kwa bidii, pasipo kujua kuwa Lengo la pili ndio kuu kuliko la Kwanza, na ndilo Mungu analoliangalia kuliko yote.

Ndugu unaweza kumwomba Bwana Yesu akuponye kansa, na kwa huruma zake akakuponya, unaweza kumwomba Bwana Yesu akupandishe cheo kazini na kwa huruma zake akakufungulia mlango huo, ukapata fursa kazini, unaweza kumwomba Bwana Yesu akufungulie mlango wa riziki au kazi, au akupe uzao na kweli akakufanyia muujiza huo mkubwa ukapata uliyoyahitaji, unaweza kumwomba akufanikishe katika ndoa au masomo, na ikatokea kama ulivyomwomba..

Sasa fahamu kuwa Bwana Yesu kakufanyia muujiza huo au miujiza hiyo, lengo lake ni ili wewe uwe na furaha, na uishi maisha mazuri sawasawa na maneno yake haya..

Yohana 6: 23 “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.

24  Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu”

Hilo ni lengo la kwanza la Bwana kuruhusu miujiza maishani mwako, lakini sio lengo kuu. Kwasababu unaweza kuponywa Kansa, au Ukimwi lakini bado ukaenda kwenye ziwa la Moto, unaweza kupata kazi nzuri, na kufunguliwa tumbo na kuzaa watoto wengi, lakini bado siku ile akakukana. Kwahiyo lengo kuu la miujiza ya Bwana si kutimiza furaha zetu, au mapenzi yetu. Bali lengo lake kuu ni ili sisi TUTUBU TUNAPOIONA MIUJIZA HIYO!!.

Je unakumbuka Mtume Petro kilichomtokea baada ya Bwana kumfanyia muujiza ule mkubwa wa kupata samaki wengi?..Petro hakufurahia tu kupata riziki, hakufurahia kupata fedha za kwenda kununua kiwanja cha kujenga, kwasababu ya ule wingi wa samaki, hakufurahia mikopo atakayokwenda kukopesha hapo baadaye kwasababu ya wingi wa wale samaki.. bali utaona alikimbilia toba..

Luka 5:4  “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5  Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6  Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7  wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.

8  Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA.

9  Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata”

Umeona?.. Simoni hakusema hapo “ondoka kwangu Bwana kwa kuwa mimi ni mtu maskini” au kwakuwa mimi ni mtu mwenye matatizo mengi ya kiuchumi au kibiashara.. bali alisema “kwakuwa mimi ni mtu mwenye dhambi” (maana yake alitubu).. Na ndipo Bwana akamwambia tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba katika miji ile ile ambayo Petro alikutana na Bwana mara ya kwanza, yaani miji mitatu ya (Bethsaida, Kapernaumu na Korazini), Miji hii yote ilikuwa kando ya bahari ya Galilaya..Bwana Yesu alikuwa akitembea huku na huko katika miji hiyo, na kufanya miujiza kama hiyo hiyo, aliyoifanya kwa Petro.

Lakini tofauti ya Petro na watu wengine wa miji hiyo, ni kwamba Petro alitubu kwa miujiza ya Bwana, lakini wengine wengi wa miji hiyo, waliifurahia tu miujiza ya Bwana lakini hawakutubu.

Walifurahia tu watoto wao kuona wanatokwa na mapepo, lakini hawakufikiri kuacha dhambi zao, ingawa Bwana alikuwa anawahubiria toba, walifurahia kubarikiwa kazi zao na biashara zao lakini hawakufikiria kutubu, hawakufurahia kuacha ulevi wao, wala kuacha uzinzi wao, wala kuacha rushwa zao wala kuacha mambo mengine mabaya, ingawa waliifurahia miujiza ya Bwana.

Na hatimaye Bwana Yesu akawaambia maneno yafuatayo…

Mathayo 11:20  “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo NDANI YAKE ILIFANYIKA MIUJIZA YAKE ILIYO MINGI, KWA SABABU HAIKUTUBU.

21  Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23  Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”

Hapo anasema alianza kuikemea kwasababu haikutubu “si kwasababu haikushukuru baada ya kufanyiwa miujiza”, au si kwasababu waliitumia vibaya ile miujiza, kwamba baada ya kubarikiwa katika shughuli zao walitumia vibaya fedha!.. La!!.. lakini iliikemea kwasababu moja tu kwamba HAIKUTUBU!!

Na tena anasema itakuwa ni rahisi kwa Sodoma kustahimili adhabu yake siku ile ya hukumu kuliko miji hiyo, maana yake ni kwamba kumbe pamoja na kwamba watu wa Sodoma na Gomora waliadhibiwa kwa moto katika mwili, lakini kumbe kuna bado kuna adhabu nyingine inawangojea huko!! Hii inaogopesha sana..

Lakini Bwana Yesu anazidi kusema, itakuwa ni rahisi watu wa Sodoma kustahimili adhabu kuliko watu wa miji hiyo ya Korazini, na Bethsaida na Kapernaumu. Maana yake adhabu ya watu wa Kapernaumu na Korazini na Bethsaida itakuwa ni kubwa sana, katika ziwa la moto.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, Tumwogope Mungu!.. Miujiza anayotufanyia kila siku ambayo tunaiona kwa macho yetu sio kwa lengo la kutuburudisha bali ni kwa lengo la sisi Kuamini kwamba yupo na kwamba yeye hapendi UCHAFU, hivyo tutubu!, tuyatakase  maisha yetu, ili tusipate hasara siku ya mwisho ya hukumu.

Ukiaona Bwana kakujibu maombi yako, ni kwasababu anataka uache usengenyaji wako, ukiona Bwana kakujibu maombi yako kimuujiza ni ujumbe kwako kwamba anataka uache kuvaa unavyovaa nguo za kubana na zisizo na heshima, anataka uache ulevi wako, na si kwamba anakusapoti na ulevi wako au uzinzi wako, au uuaji wako, amekuonyesha miujiza hiyo ili wewe ujue kwamba yeye yupo na anakutazama.

Lakini ukidharau sauti ya Mungu hiyo, ambayo inakutaka utubu, na kuifurahia miujiza tu na ishara, basi fahamu kuwa unajiwekea akiba ya hasira ya Mungu..

Warumi 2:4 “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa WEMA WA MUNGU WAKUVUTA UPATE KUTUBU?

5  Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu”

Mpokee Yesu leo na tubu kwa kudhamiria kuacha dhambi na kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na Bwana atakukubali na kukupatia kipawa cha Roho wake mtakatifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NAYE ALIKUWA HANA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 5)

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Furaha ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
robert kamau
robert kamau
1 year ago

AMEN na hitaji NENO kila Waikato +254 0715186510 kenya