Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

Daudi anapomwambia Mungu, kuwa GONGO LAKE na FIMBO YAKE vinamfariji, alikuwa anamaanisha nini?..

Jibu: Tusome,

Zaburi 23:1 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.

2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

3 Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.

4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, GONGO LAKO NA FIMBO YAKO VYANIFARIJI”.

Zamani wachungaji wa kondoo na Mbuzi, walikuwa wanatembea na Zana hizo mbili (Gongo na Fimbo), zilizokuwa zinazowasaidia katika shughuli zao uchungaji. Na kila zana likuwa na kazi yake.

GONGO: Hii ilikuwa ni kipande cha kifupi cha fimbo maalum, iliyonyooka, ambayo ilikuwa Nene kidogo na fupi, Na kazi ya Gongo, ilikuwa si nyingine Zaidi ya kupiga maadui wa mifugo kama Mbwa mwitu, dubu, Mbweha, fisi n.k Kwahiyo wachugaji walitembea nayo wakiwa katika uchungaji, ili kundi liwe salama..Fisi walipotokea kutaka kukamata kondoo, wachungaji waliwapiga kwa gongo hilo.

FIMBO: Hii ni Zana ya pili, ambayo haikuwa kwa lengo la kudhuru maadui, bali kwa lengo la kuwaongoza kondoo. Fimbo ya Mchungaji ilikuwa ni ndefu na yenye mkunjo mwishoni, na lengo la mkunjo huo ni kumvuta kondoo anapokuwa kwenye hatari au anapoelekea kwenye hatari, mkunjo ule unasaidia kuishika shingo ya kondoo au mguu wa kondoo na kumvuta kutoka kwenye hatari.. vile vile, kazi nyingine ya fimbo hiyo ni kuwaongoza kondoo wakae kwenye mstari, wasitoke.

Sasa swali ni kwanini Daudi aseme Fimbo ya Bwana na Gongo lake vinamfariji?

Ni kwasababu yeye (Daudi) anajifananisha na kondoo na Mungu anamfananisha na Mchungaji aliyeshika Fimbo na Gongo, kwamba kondoo anapoona kuwa mchungaji wake kashika Gongo, basi anakuwa hana wasiwasi kwasababu anajua gongo lile kazi yake ni kuwapiga maadui zake.. Hivyo Daudi hakuogopa maadui kwasababu Bwana ndiye mchungaji wake, hivyo gongo lile lilikuwa Faraja kwake.

Vile vile, Fimbo ya Bwana, ambayo ina mkunjo mwishoni, ilimfariji kwasababu yeye kama kondoo alijua hawezi kupotea, kwasababu ile Fimbo itamwongoza katika njia iliyonyooka, Zaidi sana hata atakapopita kando ya bonde la Mauti, Fimbo ile itamwongoza katika njia iliyonyooka, na hatapotea kamwe.

Na sisi katika roho ni kondoo na Yesu ni Mchungaji, Mkuu.. Ambaye naye pia ameshika Gongo na Fimbo, kutulinda na kutuchunga.

Waebrania 13:20 “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu MCHUNGAJI MKUU WA KONDOO, kwa damu ya agano la milele, yeye BWANA WETU YESU”

Umeona?..Bwana Yesu ni Mchungaji Mkuu wa Kondoo.. wengine ni wachungaji, lakini si wachungaji wakuu.., hali kadhalika wengine ni wachungaji, lakini si wachungaji wema… Lakini Bwana Yesu ni mchungaji Mkuu, na Mchungaji mwema.., anawachunga kondoo katika njia iliyo nyooka kwa fimbo yake, wala hakuna hata mmoja atapotea akiwa kwake, vile vile anaweza kutoa uhai wake kwaajili ya kuwaokoa kondoo..

Yohana 10:11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

12 Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.

13 Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake”.

Je! Umempokea Yesu leo?.. Je Bwana Yesu ni mchungaji wako?.. kama hujampokea Yesu, bado wewe ni kondoo uliyepotea,  ambaye Bwana Yesu, mchungaji mwema ANAKUTAFUTA!!!, kwasababu hapo ulipo haupo salama, mbwa-mwitu wanasikia harufu yako toka mbali na wanakusogelea kwa kasi, fisi na dubu, wanasikia harufu yako na wanakukaribia ili wakudhuru, wakufanye kitoweo… Leo hii umemwona Mchungaji mwema Yesu Kristo, mkimbilie huyo uwe salama, ili hatimaye useme kama Daudi.. “Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na chochote, gongo lake na fimbo yake vyanifariji”.

Huko kwenye ulevi ulipo, umepotea, huko kwenye uzinzi, na uasherati ulipo umepotea, huko kwenye dansi ulipo na kwenye miziki, fasheni, na anasa za kidunia umepotea!.. haupo salama!.. Maisha yako yapo hatarini, wewe ni windo bora la mapepo yote, ni windo bora la wachawi, ni windo bora la mauti. Na vyote hivyo vinakutafuta.. Haupo salama kabisa!..kimbilia kwa Yesu…

Kama bado hujaokoka na unahitaji kuokoka ili uwe salama ndani ya Mchungaji mwema Yesu, basi wasiliana nasi inbox tuweze kuomba nawe, sala fupi ya kumkaribisha Bwana Yesu, maishani mwako.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma.

Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu?

Ni kwa namna gani Yesu ni Simba wa Yuda?

Kwa namna gani mauti hufanya kazi ndani yetu na uzima kwa wengine? (2Wakorintho 4:12).

JAWABU LA MAISHA YA MTU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Prisca komba
Prisca komba
1 year ago

Amina nipekupat mtumishi

Anonymous
Anonymous
1 year ago

Amen

samari
samari
1 year ago

Amina sana mtumishi Mungu awe pamoja nanyi