Maana ya watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.

Maana ya watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.

SWALI: Nini maana ya hili Neno “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6).


JIBU: Maarifa yanayozungumziwa hapo sio maarifa ya darasani.. ingawa hata hayo ya shuleni pia ni maarifa na yana nafasi yake katika maisha, lakini yaliyozungumziwa hapo sio hayo..

Maarifa yanayozungumziwa hapo ni maarifa ya kumjua Mungu.

Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”

Hali kadhalika biblia inaposema “Mkamate sana Elimu, usimwache aende zake, maana yeye ndio uzima wako (Mithali 4:13)”.. Tafsiri ya kwanza ya mstari huo sio Elimu ya kidunia, bali ni elimu ya Ufalme wa Mbinguni.

Mathayo 13:51  “Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.

52  Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale”

Kasome pia (Yohana 7:15-17, Marko 1:27,1Timotheo 6:3-5, Matendo 17:18-34), Na pia kuna somo tuliloliandikwa lenye kichwa “Fahamu majira tuliyopo na nini unapaswa uwe nacho”, upatapo nafasi lipitie utapata kuelewa Zaidi.

Kwahiyo mbele za Mungu mtu asiye na Elimu ni yule asiyezijua siri za ufalme wa Mbinguni ikiwemo uweza wa Mungu, na mtu asiye na maarifa ni yule asiyeyajua maarifa ya kimbinguni (maana yake hajui chochote kuhusu Mungu), haijalishi atakuwa na Elimu ya kidunia kubwa kiasi gani; awe profesa, awe dokta awe waziri au awe mtu yeyote yule mwenye elimu kubwa..kama hana Elimu na Maarifa ya ufalme wa mbinguni, basi mbingu inamwona ni hana Elimu wala maarifa yoyote…Na hivyo Ataangamizwa.

Sasa tukirudi kwenye huo mstari wa Hosea kuna kitu cha kujifunza Zaidi..Hebu tuusome tena kwa makini..

Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako”

Ukisoma kwa makini hapo inasema “watu wangu wanaangamizwa!” na sio “wanaangamia”..Maana yake ni kwamba mtu akikosa maarifa ya kimbinguni kuna kitu cha nje kitamwangamiza. Hataangamia tu peke yake..La! bali kuna kitu kitakuja kumwangamiza.

 Kwa lugha nyepesi ni kwamba maarifa ni kama “ULINZI”. Unapokuwa na maarifa mengi ya kumjua Mungu basi ni ngumu kushambuliwa na Adui yetu shetani na majeshi yake.

Mithali 1:26 “Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo; 

27 Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.

 28 Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.

  29 KWA KUWA WALICHUKIA MAARIFA, WALA HAWAKUCHAGUA KUMCHA BWANA. 

30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote. 

31 Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

 32 Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. 

33 Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya”.

Kwahiyo ni jukumu letu kila mmoja kuyatafuta Maarifa ya Mungu kwa bidii ili tusiangamizwe!..Ukikosa maarifa ya ki-Mungu, utawaogopa wachawi, ukikosa maarifa ya ki-Mungu hutajua tunaishi siku gani hizi, na hivyo utapotea katika hiki kizazi, na mwisho kwenda kuangamizwa katika moto wa milele.

Bwana atubariki.

Mada Nyinginezo:

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

MSHIKE SANA ELIMU.

CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA,

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

USITOKE NJE YA HIFADHI YA MUNGU.

KUMCHA MUNGU NI NINI? NA MTU ANAMCHAJE MUNGU?

DAKIKA MOJA TU, INAKUFANYA UMWAMINI SHETANI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Shose
Shose
1 year ago

Maarifa yanayozungumziwa hapa ni kweli si maarifa ya darasani bali ni maarifa ya moja kwa moja yarokayo kwa Mungu kuja kwa kuhani na kuachiliwa kwa watu wa Mungu ili wasiangamie. Makuhani wamekaa nje ya uwepo hivyo kukosa neno la maarifa toka kwa Mungu na kisha kwa wakristo. Nyakati hizi kondoo wanazagaa na kupigwa kikatili. Makuhani wanaeanyoshea vidole na kuwasema walivyokosa maarifa.