MSHIKE SANA ELIMU.

MSHIKE SANA ELIMU.

ELIMU ni UFUNGUO wa maisha, hiyo ni kweli, lakini ELIMU ILIYO SAHIHI sio tu ufunguo wa maisha, bali pia ni ufunguo wa kila kitu. Na kwa jinsi elimu ya mtu huyo itakavyozidi kuwa kubwa zaidi ndivyo uwezekano wa mtu huyo kufanya mambo yote unavyozidi kuwa mkubwa zaidi.

Kumbuka zipo Elimu kuu tatu zilizopo ulimwengu sasa. 

1)Elimu ya ufalme wa mbinguni.

2)Elimu ya kidunia

3)Elimu ya ufalme wa giza

Leo hii tunaweza kufurahia mafanikio tuliyoyafikia ya kiteknolojia kwa mfano kuchat na watu mitandaoni, kupaa angani kwa ndege, kuzungumza na ndugu zetu walio mbali kwa simu, kutunza vyakula katika majokofu, katazama tv n.k..sio kwasababu dunia imebalika maumbile yake tofauti na ya zamani hapana!, Ni kwasababu wapo watu waliokaa chini kwa muda mrefu mahabara, na katika makarakana usiku na mchana, wengine hata kutokuoa au kuhatarisha maisha yao, wakisoma na kujifunza kanuni za huu ulimwengu jinsi ya kuendana nazo na kwa namna gani watazitumia kubuni njia mbadala ya kuunda vitu. Na kwa bidii yao ya kujifunza na kusoma sana kwa muda mrefu ikawapelekea kugundua vitu ambavyo hata kwa namna ya kawaida unaweza ukasema haviwezakani kutokea. Lakini tunaviona katika jamii zetu kila siku vipo..

Kadhalika shetani naye hakuna jambo ameweza kufanikiwa kulipata kwa mwanadamu kirahisi rahisi kama sio kwa Elimu. Alisoma kanuni za Mungu za uumbaji kwa muda mrefu sana, hivyo kwa kuwatazama viumbe wake na vitu vya asili na nguvu na mamlaka Mungu aliyoweka ndani yao, akagundua kuwa akiwafanya waende kinyume na zile kanuni basi yeye atakuwa na uwezo wa kuzitumia kwa manufaa yake. Na ndio maana jambo la kwanza pale Edeni Shetani hakuja kwa utisho wowote wa silaha kwa Adamu na Hawa hapana bali alikuja na UDANGANYIFU. Ambao alijua kwa huo ataweza kuwadhoofisha UWEZO wao hivyo kirahisi atawapokonya mamlaka yao waliyopewa na Mungu katika hii dunia..

Na ndivyo alivyofanya na kufanikiwa kuuweka ulimwengu chini yake mpaka tunaona alipokuja Bwana wetu Yesu Kristo kuyachukua yale mamlaka tena Adamu aliyoyapoteza. Na haishii hapo tu! kwasababu shetani lengo lake ni kutaka kuwa kama Mungu, na kwasasa ameshafahamu kuwa hawezi tena kufikia malengo yake kwasababu ya YESU basi anachokifanya ni kuwa piga upofu wanadamu wote wasifikie katika viwango vya MAARIFA/ELIMU ambayo Bwana anataka watu wake wavifikie.

Na ndio maana biblia inasema katika Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;”..Shetani ataendelea kutuangamiza kama tutakosa maarifa ya kimbinguni.

Sasa Elimu hizo mbili yaani (Elimu ya dunia na Elimu ya ufalme wa giza), japo kila moja inajitahidi kwa upande wake, kutatua kila jambo, lakini hata moja haijaweza kuleta suluhisho la mambo ya msingi yamuhusuyo mwanadamu. Kwamfano hakuna elimu yoyote inayoweza kuleta dawa ya kifo na kutoa uzima wa milele, au kufufua mfu, au kuumba, au kusimamisha jua, au kuupiga mwezi, au kuamisha visiwa na milima, hakuna hata moja inayoweza kutabiri mambo yanayokuja,..hakuna hata moja ya hizo inazoweza kufanya jambo kama hilo. Wanasayansi wote pamoja na shetani mwenyewe hawana maarifa hayo.

Ni ELIMU moja tu YA KWELI ambayo Mungu aliiweka tangu mwanzo ndiyo inayoweza kufanya mambo yote, nayo ni ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI BASI!!.

Hivyo pale Biblia inaposema katika Mithali 4:13 “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.”

Haimaanishi ELIMU yoyote tu ile, iliyopo kila mahali, hapana sio elimu ya ulimwengu huu, kama vile isivyokuwa elimu ya wachawi, bali Elimu inayozungumziwa pale ni Elimu inayohusiana na hicho kitabu chenyewe (yaani BIBLIA).

Na kama vile Elimu yoyote ile ilivyo na gharama kuipata kadhalika na kuisoma, vivyo hivyo na hii ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI izidiyo elimu zote inayo gharama nyingi za kuipata. Kila mkristo anapoamini na kumpa Bwana maisha yake ni sawa na mtoto kwa mara ya kwanza aliyeenda kuanzishwa elimu ya awali, anaitwa mwanafunzi, tunafahamu kuwa siku hiyo hiyo hawezi kujua kila kitu kinachohusu shule, siku hiyo hiyo hawezi kupaisha ndege, au kufanya operesheni, hapana bali atakavyozidi kuonyesha bidii ya kujifunza kila siku, kidogo kidogo atajikuta anaongeza kitu katika kichwa chake, atavuka darasa moja, anakwenda lingine hivyo hivyo mpaka baadaye akifika chuo kikuu, ambapo kiwango cha yale maarifa kitakuwa kimeshakolea ndani yake sasa hapo ndio anakuwa na uwezo wa kurusha ndege.

Na ndivyo tunavyojifunza kwa Bwana wetu YESU KRISTO, tunamwona kama vile alivyo, hakuzaliwa na kipawa tu basi cha kuwa na hekima nyingi kiasi kile na kujawa uwezo mkuu kama ule. Biblia haitufundishi hivyo bali tunamwona Bwana tangu akiwa mdogo alikuwa ni mtu mwenye bidii sana KUSOMA ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI, alikuwa akijifunza kupita kiasi hata akiwa na umri wa miaka 12 tu, biblia inarekodi siku tatu usiku na mchana alikuwa akijifunza habari za YEHOVA kwa marabi(Waalimu wa Torati), akiuliza maswali, pale ambapo hakuwa anapaelewa, alisahau hata kula kwa ajili ya KUSOMA TU! Aliwasahau wazazi wake, aliona ule muda walioenda Yerusalemu na wazazi wake ni mchache sana wa yeye kujifunza,

Tunasoma;

Luka 2:45 “na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.

46 Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, AKIWASIKILIZA NA KUWAULIZA MASWALI.

47 Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake”.

Biblia inasema pia aliendelea kuwa mtu wa namna hiyo hiyo, akitoka katika hatua moja ya hekima hadi nyingi.. Tunasoma

Luka 2:52 Naye Yesu akazidi kuendelea katika HEKIMA NA KIMO, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Unaona hapo aliendelea katika Hekima, siku baada ya siku na KIMO kinachozungumziwa hapo sio urefu wa mwili, bali ni KIMO cha KUMJUA MUNGU. Aliweza kuona mahali waandishi walikwama, yeye hakuridhika akavuka pale na kuzidi kujifunza zaidi mpaka siku moja akawa ZAIDI ya wale MARABI waliokuwa juu yake wakimfundisha.

 Tunasoma;

Mathayo 13:51 “Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.

52 Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake VITU VIPYA NA VYA KALE”.

Bwana yeye kama mwandishi mkuu pia aliweza kutoa katika hekima yake vitu vipya na vitu vya kale (Agano jipya na Agano la Kale), kwasababu Elimu ya Ufalme wa mbinguni ilikuwa imemkaa sana ndani yake.

Hiyo ni sababu leo hii tunamwona Bwana kuwa mtu ambaye hakushindwa na jambo lolote, hakukuwa na tatizo lolote lililoweza kusimama mbele yake, alipewa maarifa yote na Mungu, alipewa maarifu ya namna ya kuutoa uhai wake na kuurudisha, ni nani leo hii anaouwezo huo?, aliweza kuamrisha mbingu, bahari, na upepo vyote vikamtii,hakukuwa na mgonjwa yoyote aliyeletwa mbele zake asiweze kumponya, Mungu alimpa kila kitu angali akiwa bado hapa duniani.. Na ndipo hapo shetani akajua kuwa hakuna tena tumaini kwake kwasababu vyote alivyovitarijia siku moja avipate vyote vimeshafunuliwa kwa BWANA wetu YESU KRISTO. Haleluya!. Kazi aliyobakiwa nayo sasa ni kutuangamiza kwa kukosa kwetu maarifa ya kumjua YESU KRISTO BWANA WETU.

Bwana YESU alitupa ushauri sisi wote, kwamba “TUJIFUNZE KWAKE” (Mathayo 11:29). Na pia alisema yeye ndiye njia ya kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye (Yoh 14:6). Hivyo ni lazima tujifunze katika NJIA ZAKE ili na sisi tupate akili tupone.

Kama wachawi na wanasayansi hawalali kila siku wapo wanachunguza na kutafiti juu ya mambo yao na ufalme wao, inatupasaje sisi wakristo ambayo ELIMU YETU inaweza kufanya makubwa zaidi ya hayo?

Ukristo mwanzo wake ni kuamini na kubatizwa, lakini pia ni zaidi ya hapo. Bwana anataka kutupa maarifa ya ziada katika maisha yetu ya kumjua yeye, ili na sisi pia tukue katika kimo na hekima, kama Bwana, lakini tunakuwa wavivu wa KUSOMA na KUJIFUNZA NENO LA MUNGU kila siku.

Japokuwa Paulo alikuwa ni mtume wa Kristo aliyejaa mafunuo mengi, na ambaye mpaka sasa tunatumia nyaraka zake kama urejesho wetu wa kimaandiko, lakini hakuacha KUSOMA na KUJIFUNZA kila siku Elimu ya Ufalme wa mbinguni. Tunasoma akimwambia Timotheo..

2Timotheo 4: 13 Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, NA VILE VITABU, HASA VILE VYA NGOZI.

Unaona hapo?, alihitaji Kusoma, kwasababu Elimu ya ufalme wa mbinguni ni kuu sana haina mwisho wake. Hakujiona kuwa amefika au anafahamu kila kitu bali alitaka zaidi na zaidi kujifunza kumjua Mungu katika upana wake na marefu yake. Na hakuishia hapo bali alimwagiza pia Timotheo afanye vivyo hivyo, kama tunavyosoma katika

1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.

13 Hata nitakapokuja, UFANYE BIDII KATIKA KUSOMA na kuonya na kufundisha.”

Hivyo na sisi pia kama watoto wachanga, tuitafute sana Elimu ya ufalme wa mbinguni, kwa kutafiti na kuchunguza mambo yote yamuhusuyo MUNGU wa ISRAELI na YESU KRISTO BWANA WETU katika maandiko angali tunaishi sasa, ili tukifikie kile cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo. Amen.

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani NA KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, NA KUCHUKULIWA NA KILA UPEPO WA ELIMU, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO YA MASHETANI

JE! UMEFUNDISHWA?

UPEPO WA ROHO.

NINI MAANA YA “NITAWAVUTA WOTE KWANGU” (YOHANA12:32)?

JE KUNA ANDIKO LINALOMRUHUSU MWANAMKE KUWA SISTER?

YOHANA MBATIZAJI ALIBATIZWA NA NANI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Hamisi Nkuluzi
Hamisi Nkuluzi
3 years ago

Mungu kubariki nimesoma na kukubaliana 200% , suala hili linatumika vibaya ndio maana wengi wanadhani kuwa na Theolojia , Sayansi nk pasipo kulijua Neno kwa kuongozwa na Roho wa Mungu wamefikia KIMO , ukweli hauwezi kupata matunda. Matokeo yaliyopo kwa makanisa mengi ni migogoro mingi kutokana na kuhitimu Elimu ya Dunia hii.Kwa nini walezi wa Bwana Yesu hawakumpeleka shule wala Yeye kutafuta badala yake alidumu kuchambua Torati na Kuuliza maswali ?