UPEPO WA ROHO.

UPEPO WA ROHO.

YOHANA 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.”

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lisifiwe daima, Ni siku nyingine tena Bwana aliyotupa kwa neema zake na leo tutaangalia vifungu hivyo ni kwanini Yesu aliifananisha hali ya mtu aliyezaliwa kwa Roho na kama UPEPO UVUMAO.

Yapo mambo matatu hapo Bwana aliyoyasema  kuhusu Upepo,

1)   La kwanza ni Upepo Huvuma upendako

2)   La pili ni: Sauti yake waisikia (lakini hauuoni)

3)   Na la tatu ni Hujui utokako wala unakokwenda.

Na mwisho akamalizia kusema “NDIVYO ILIVYO HALI YAKE MTU ALIYEZALIWA NA ROHO”. Hii ina maana gani? Ni wazi kuwa inamaanisha  pale Roho wa Mungu anapoingia ndani ya mtu kwa mara ya kwanza basi hali yake inabadilika na kufanana na tabia inayoweza kulinganishwa na tabia ya upepo.

Tabia hizi ni mara tu baada ya mtu kuzaliwa kwa Roho, kwahiyo tunaweza kusema Upepo huo ni Roho mtakatifu ndani ya mtu. Kwasababu ndiye aliyemfanya kuwa hivyo. Kama tunavyofahamu tabia ya upepo, kwanza ni kitu kisichoweza kuonekana  kwa macho lakini utaisikia sauti yake pale unapovuma, au utauhisi katika mwili wako pale unapopita karibu na wewe, lakini usijue chanzo  chake ni wapi na hatma ya safari yake itaishia wapi!!.

Kadhalika  Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mwamini tabia hizi za upepo wa Roho huingia ndani yake. Pale mtu alipoamua na kudhamiria kweli kumpa Kristo maisha yake. Basi kuanzia huo wakati na kuendelea ndani yake kunakuwa na nguvu isiyojulikana chanzo chake ni nini kwa nje! Watu wa nje wanaweza kushangaa mbona huyu mtu tabia yake imebadilika kwa ghafla hivi,wasijue ni nani aliyembadilisha, wakijaribu kachunguza labda ni dini hawaoni, labda ni dhehebu hawaoni, labda ni mwanadamu hawaoni, na ndio hapo utaona maisha ya yule mtu yanabadilika, pengine mambo aliyokuwa anapenda kuyafanya hapo mwanzo yanageuzwa ghafla, maisha aliyokuwa anaishi nyuma yanageuka ghafla, mara nyingine atajikuta anachukia hata kufanya baadhi ya vitu alivyokuwa anavifanya nyuma, anajikuta kiini cha maisha yake ni kumwangalia Bwana YESU tu mahali popote alipo…Baadhi ya mambo yasiyokuwa na maana yataanza kumkera, anaanza kutokujiona kuwa huru akiwa katika vikao vya usengenyaji, tofauti na alivyokuwa hapo mwanzo..

Hii yote inatokea ni kwasababu yule Roho aliye ndani yake humsukuma kufanya vitu ambavyo hata pengine yeye mwenyewe hajui ni kwanini anavifanya, saa nyingine anaweza akadhani ni kwa akili zake anafanya hivyo.Au ni kwasababu ametokea tu kupenda mwenyewe Lakini ukweli ni kwamba sio yeye anafanya hivyo bali ni Roho wa Mungu ndani yake atembeaye kama upepo usioonekana anamwelekeza asikojua yeye.

Atajikuta anaanza kuchukia kupenda pombe, ambapo hapo mwanzo alikuwa anazitamani, anajikuta kuvaa vimini na suruali anajiona kama yupo uchi au anajiaibisha mbele za watu hivyo anajikuta anaanza kupenda kuvaa sketi ndefu ambazo hapo mwanzo alikuwa akivaa anajiona kama mshamba. Anajikuta anatamani kusoma biblia, au kusikiliza Neno la Mungu sana, ambapo hapo kwanza alikuwa hana mpango navyo. Anajikuta kampani za marafiki wa kidunia ni mzigo mkubwa kwake tofauti na jinsi alivyokuwa nyuma. Anajikuta hata akipitia dhiki kubwa kiasi gani kwa ajili ya imani hapepesuki mpaka watu wa nje! Wanashangaa huyu mtu ni wa dizaini gani. N.k.

Na hata baada ya muda mrefu kupita ukimuuliza ilikuwaje kuwaje ukaweza kuacha dhambi na mambo ya kidunia pamoja na majaribu mazito kiasi kile atakwambia kwa kweli sifahamu nguvu hiyo ilitoka wapi,nilijikuta tu ninamsimamo na maamuzi yangu..nilijikuta tu kuna nguvu fulani ndani yangu ikinisukuma kunipeleka sehemu Fulani,sasa huo ulikuwa ni ule upepo wa Roho ambao ulikuwa unampeleka asikotazamia yeye kwenda,.ataishia kukwambia ni neema za Mungu tu.

Na ndio maana katika siku ile ya Pentekoste Roho aliposhuka kwa watu kwa mara ya kwanza Ishara ya kwanza aliyoshuka nayo ni ishara ya  UVUMI WA UPEPO uendao kwa kasi, sio kwasababu  Mungu alikuwa anataka kuwaonyesha watu uweza wake wa kuamuru tufani, hapana, bali Upepo ule ulifunua jambo kubwa sana katika roho  kwa waumini wa kweli waliokuwa Yerusalemu..na ndio maana ukichunguza kwa makini baada ya pale maisha na mienendo ya mitume ilibadilika  ghafla tangu ule wakati, walipokea ujasiri usio wa kawaida kuhubiri injili, walijawa na Imani kwa Mungu, hawakuwaogopa maadui zao tena, na kwenda kujificha kama ilivyokuwa pale mwanzo.. Mara nyingi roho alikuwa akiwatwaa na kuwapeleka wasikojua, na huko wanapofika wanalihubiri Neno la Mungu kwa ushujaa mwingi..Tunamwona mtu kama Filipo alitwaliwa na Roho na kupelekwa kule Roho alipopenda kumpeleka.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI.

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Unaona kulikuwa na Upepo wasiojua ulipotoka ,Ule ulifunua UPEPO WA ROHO, ambao ndio ulioathiri maisha yao kuanzia ule wakati na kuendelea.

Unaona umuhimu kwa kuzaliwa kwa Roho? Leo hii ni kwasababu gani huwezi kushinda tamaa, na dhambi, ni kwasababu moja tu, nayo ni hii HAUJAZALIWA MARA YA PILI hivyo ule upepo wa Roho hauwezi ukawa na nguvu juu ya maisha yako. Haujamkaribisha Roho ndani ya maisha yako. Kama ungekuwa umezaliwa kwa Roho ile nguvu ingekusukuma mahali usipojua kama vile UPEPO uvumapo na usingeona kuwa dhambi ni jambo gumu kuliacha kwasababu ni Roho mwenyewe angekuwa anatenda kazi ndani yako.. Nguvu ile Ingekusukuma kule usikoweza kufika, ingekusukuma kutenda mapenzi ya Mungu na kumtazama Kristo kila wakati.

Kumbuka Nikodemo  alikuwa ni Farisayo wa mtu dini sana, anayejua maandiko sana lakini hakuwa amezaliwa mara ya pili, unaona? kumbe unaweza ukawa wa kidini na usiwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Ndugu Usiridhike na dhehebu lako, au kanisa lako ukajiona kuwa tayari umekamilika na huku unaona kabisa maisha yako ya kikristo yanadorora siku baada ya siku..Na ndio maana maandiko yanasema, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO HAWEZI KUUINGIA UFALME WA MBINGUNI hapo hata kama uwe unayafahamu maandiko kiasi gani, huwezi kuuingia ufalme wa mbinguni, Bwana Yesu anasema hivyo.

Lakini Mtu anazaliwaje kwa Roho na kwa Maji?

Ni kwa kukudhamiria kabisa kutubu na kuacha dhambi na maisha ya kale.Wengi hawafanyi hivyo, toba haitoki moyoni bali midomoni na ndio maana inakuwa ngumu Roho wa Mungu kukaa ndani yao. Na maana ya toba sio kuomba msamaha tu, bali ni KUGEUKA AU KUACHA. Hivyo unapogeuka na kukusudia kuacha dhambi hata usiposema kwa mdomo hiyo tayari ni TOBA, Hivyo ukizingatia hayo na Mungu akishaona nia yako yeye mwenyewe atakuosha “roho yako”,  kwa maji (ambayo ni DAMU yake na Neno lake) na kukugawia Roho wake ndani yako atakayekuweza kukusaidia kuishinda dhambi siku zote za maisha uliyopo hapa duniani..

Kama maandiko yanavyosema:

 Ezekieli 36: 24 “Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25 Nami NITAWANYUNYIZIA MAJI SAFI, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.

26 Nami nitawapa ninyi moyo mpya, NAMI NITATIA ROHO MPYA NDANI YENU, NAMI NITATOA MOYO WA JIWE ULIOMO NDANI YA MWILI WENU, NAMI NITAWAPA MOYO WA NYAMA.

27 NAMI NITATIA ROHO YANGU NDANI YENU, NA KUWAENDESHA KATIKA SHERIA ZANGU, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

28 Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”

Hivyo mambo hayo hayatimiliki pasipo kuambatana na ishara ya wazi ya nje kuonyesha kuwa hicho kilichotendeka nje ndicho kilichofanyika rohoni mwako. Kwahiyo ni lazima mtu akazamishwe kwenye MAJI mengi akabatizwe kwa maji tele,kama Bwana alivyoagiza na ni katika JINA LA YESU, kuonyesha kuwa ameoshwa dhambi zake kwa maji ya Roho, kisha ndipo awe na uhakika kuwa amepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu ndani yako.

Hivyo ikiwa haujachukua uamuzi huo fanya hivyo haraka, ili neema hii ipate kuwa juu yako. Na ule UPEPO wa ROHO MTAKATIFU utakuvumisha na kukupeleka usikojua wewe, Na mwisho wake utashangaa umetulia mahali Mungu ambapo alikusudia..na utakuwa na uhakika siku ile kunyakuliwa juu kwenda mbinguni kumlaki Bwana, katika upepo huo wa kisulisuli kama Nabii Eliya.

Chukua muda wako kuwahubiria habari njema za wokovu, ndugu zako, marafiki zako na jamaa zako popote pale ulipo, ili na wao wapone, shetani asipate mazao.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

IMANI YENYE MATENDO;

MWAMBA WETU.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments