CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA,

CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA,

Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi”.


Shalom, Jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maneno ya Mungu yanayobubujisha uzima wa milele ndani yetu.

Kama tunavyosoma katika biblia kuna wakati ambao huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo ilifika katika kilele chake, yaani habari zake zilivuma karibia kila mahali, sehemu zote habari zake zilikuwa zinazungumziwa,..Mpaka watu kutoka mataifa mbali mbali wakawa wanakuja kutaka kumwona YESU. Na kuja kwao hakukuwa kwa ajili ya kufuata miujiza tu hapana, bali kwa lengo la kupata wokovu aliokuwa nao.

Mpaka ikafikia wayunani nao wakawa wanatafuta kumwona Yesu..

Yohana 12:20 “Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.

21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu”.

Unaona?? Lakini Bwana alipoona mazingira yale, na mwitikio ule mkubwa wa watu wengi na wengine kutoka mataifa mbalimbali, aliwaambia wanafunzi wake maneno haya..

Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi”.

Aliwapa mfano huo ulio hai wa chembe ya ngano, ili kuwafundisha watu ni kwanini Mungu ampokee, kwanini Mungu amtukuze kiasi kile, ambapo sisi watu wa kizazi hiki ndio tunaojua ni kwa namna gani Mungu amemtukuza Bwana wetu YESU kwa namna isiyokuwa ya kawaida, leo hii mtu aliye maarufu kuliko wote duniani kwa wakati wote ni YESU KRISTO, na mtu anayezungumziwa sana, kwa kila dakika na kila sekunde moja ni YESU, na jina linalotajawa mara nyingi Zaidi kulingana na takwimu za dunia ni YESU KRISTO, haijalishi ni watu wangapi maarufu watapita hapo katikati lakini yeye atabakia kuwa mtu asiye karibiwa hata kwa nukta moja kwa sifa, na umaarufu duniani kwa wakati wote…

Lakini siri ya yeye kuwa hivyo, ndio ilikuwa katika ule mfano wa chembe (mbegu) ya ngano..akawaambia kama ngano isipotupwa ardhini, ikachimbiwa chini sehemu chafu, ikaoza, na mwisho wa siku ikafa kabisa, basi haiwezi kuzaa na kutoa mazao, na kuletea faida yoyote ulimwenguni.. itaendelea kubakia tu palepale ghalani, katika hali ile ile kwa miezi na miezi na miaka kwa miaka.. Hiyo ni kanuni ya asili kabisa, inajulikana hata kwa mbegu nyingine zote.

Bwana Yesu alikubali kufa kwanza, na kuonekana sio kitu, kwa ulimwengu, soma

(Isaya 53:3 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.”),

Unaona? ulimwenguni wote ulimchukia kwa maisha yake ya kuchukia dhambi, alionekana kama mtu baki duniani,na hiyo ilimfanya aonekana pia kama amerukwa na akili soma..(Marko 3:21)

Yohana mbatizaji alisema alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea (Yohana 1:11).. Alikiri kabisa kwa ndugu zake, kuwa ulimwengu hauwezi kuwachukia wao, bali unamchukia yeye kwasasabu anazishuhudia kazi zake kuwa ni mbovu (Yohana 7:7)..

Embu mwangalie jinsi alivyojikana nafsi,..Jinsi alivyokubali kuoza kwa habari ya ulimwenguni..Lakini hapa sasa Mungu anamtukuza, anamletea mataifa, waje wamsujudie, wanadhani ilitokea tu juu juu.. Ndipo anapowaambia wanafunzi wake..

Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.

25 Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.

26 Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu”.

Hata na sisi leo hii ni kwanini wokovu wetu unaonekana umekwama mahali Fulani..yaani tangu tuliposema tumeokoka hadi leo, hatuoni badiliko lolote katika roho zetu..ni kwasababu hatukujikana nafsi..Hatukukubali kuoza ardhini kwa habari ya ulimwengu..

Tulipookoka tulikuwa bado tunataka tuonekana ni wa kisasa, kwamba na sisi tunajua kwenda na wakati, na fashion za kiulimwengu, tuvae na sisi vimini vyetu kama zamani, tuvae suruali zetu kama zamani tusiwe tofauti na wale wanenguaji..tuendelee kuhudhuria katika kumbi za starehe..tuendelee kulewa vilabuni, tuendelee kukaa na watu wanaozungumza maneno ya mizaha muda wote,..tuendelee na biashara zetu haramu..tuzidi kuwa wakidunia..tusipende kujifunza maneno ya Mungu marefu, tupende mafundisho mepesi mepesi, tunayotutabiria mafanikio..n.k.

Kwa namna hiyo Bwana Yesu anatuambia..tutabaki katika hali hiyo hiyo katika roho..miaka nenda miaka rudi..hutaona badiliko lolote katika roho yako, hutaona Bwana akikupigisha hatua nyingine rohoni..utakuwa unakwenda kanisani unarudi, unahudhuria madarasa ya biblia kila siku..Lakini maisha yako hayana ushuhudu wowote..

Yaani kwa kifupi ukiulizwa tangu siku uliposema umeokoka hadi leo, ni jambo gani Mungu kakuongezea ndani ya maisha yako, utasema sijaona.. Hatuzungumzii masuala ya fedha, kwasababu si kila mwenye fedha amebarikiwa, japo Baraka zinaweza kuambata na fedha..lakini fedha si lazima ziambatane na Baraka..Tunachozungumzia ni mafanikio yako ya rohoni..Je! Roho yako imenufaishwa na huo wokovu kiasi gani tangu uliposema umeokoka?..

Damu ya YESU imeleta badiliko gani jipya katika maisha yako? Je! Zile chemchemi za maji ya uzima zinabubujika ndani yako? Je! Roho Mtakatifu anakushuhudia ndani yako kuwa wewe ni mwana wa Mungu?, Je! Siku kwa siku unamwona akitembea katika maisha yako,

Je! Wokovu wako ulishawahi kuwa faida kwa wengine nao pia wakaupokea?..Je! ndani yako dhambi imekuwa mbali na wewe kiasi gani?..Je utakatifu ni mrahisi kwako? N.k

Kama ni La! Basi ujue mbegu yako haijaoza..na ndio maana huna matunda yoyote..

Kama unafikiria kutubu dhambi zako..basi ujue kuwa toba inaambatana na kitendo cha kujikana nafsi, mahali ambapo unasema msalaba mbele dunia nyuma..Unakuwa tayari kuchekwa kwa ajili ya wokovu wako..Unakuwa tayari kuonekana ni mshamba kwa ajili ya wokovu wako, unakuwa tayari kuonekana umerukwa na akili kwa ajili ya kukubali kwako kuishi maisha matakatifu..

Hapo ndipo unapooza…mbinguni unaonekana umeipoteza nafsi yako,..mpaka unakufa kabisa kwa habari ya ulimwengu..Sasa baada ya hapo, Mungu ndipo anapokuhuisha na kuanza kukuchipua tena kutoka ardhini, na kidogo kidogo anakukuza, anakutoa hatua moja hadi nyingine, unaanza kumwona Mungu katika viwango vya tofauti na pale mwanzo, unauhisi ule uhalisia wa wokovu ndani yako yako..

Na ghafla utashangaa anakufikisha mahali ambapo, wewe mwenyewe hukudhania kama ungeweza kufika kwa wakati huo..na hata yale uliyoyapoteza Mungu anakurudishia kwa wakati wake ukifika..Mwisho wa siku unakuwa na matunda kote kote…

Hivyo ndugu, kama hujaubeba msalaba, basi tujikane nafsi leo mfuate Yesu..maana huko ndipo yeye anapotungojea wote. Ili na sisi tubarikiwe kama yeye, tusibaki katika hali ile ile rohoni siku zote.

Shalom. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JIKANE NAFSI MTEULE WA MUNGU.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

HAKIKISHA UNALIELEWA NENO.

NI NANI ALIYEWALOGA?

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

TUWATAFAKARI NZIGE WA JANGWANI.

MAONO YA NABII AMOSI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amina