JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

Jinsi sodoma na gomora ilivyokuwa inavutia sana.

Mwanzo 13:10 “Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.

11 Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao”.

Ndugu kama ulikuwa hujui, basi leo ujue, kuwa dhambi ni kitu kinachovutia sana! Kama dhambi ingekuwa haivutii hakuna mtu leo hii angenaswa na mtego wowote wa dhambi..Wengi wetu tunajua habari ya Lutu na mjomba wake Ibrahimu jinsi walivyopishana kauli kutokana na wingi wa mali walizokuwa nazo, mpaka ikafikia hatua sasa wajitenge kila mmoja achague upande wake wa kukaa.

Lutu akapewa kipaumbele cha kwanza cha kuchagua, akafanya utafiti wake wa mji bora wa kukaa, ndipo akaitazama miji yote iliyokuwa kando kando na pale walipokuwepo yeye na Ibrahimu, mwishowe akafanikiwa kuona miji mizuri sana, ambayo hakukuwa na mfano wake katika kaanani yote na miji yenyewe ni Sodoma na Gomora. Biblia inasema miji hiyo ilikuwa mfano wa BUSTANI YA MUNGU (Edeni). Ilikuwa nzuri karibia ifanane na Edeni..Hivyo sio kila mahali panapoonekana pazuri Mungu yupo…Uzuri wa sodoma na Gomora ulifananishwa na Edeni, lakini ilikuwa ni bustani ya shetani…Shetani naye anayo Edeni yake ambayo kwa uzuri inakaribi Ilikuwa ni miji yenye kijani kibichi, yenye chemchemi za maji, na mwonekano wa kuvutia.

Vivyo hivyo ilikuwa ni miji yenye ustaarabu uliomakini, yenye uchumi mkubwa, yenye fursa nyingi za biashara, isiyo na njaa wala kiu, miji ambayo mtu ukiishi unajua nini maana ya maisha,.mbali sana na hiyo Kaanani ambayo alikuwa anaishi yeye na Ibrahimu, ambayo ni jangwa tupu, hakuna hata chakula cha kutosha maji yenyewe ni ya shida, kama nusu-kijiji tu..

Na hiyo ndiyo sababu mojawapo iliyowafanya watu wa miji ile wasimwongope Mungu, wamuone kuwa si kitu cha maana sana kwao, wakaanza kujiamulia kuishi tu kama wapendavyo kama wanyama, wanazini wao kwa wao jinsia moja, wanazini na wanyama. N.k.

Sasa Lutu yeye hakuangalia nyuma ya pazia kuna nini..Yeye maadamu anaona fursa, na maisha mazuri akaamua kuingia moja kwa moja, kumbe kama sio neema ya Mungu ndio ulikuwa mwisho wake..

Biblia inatuambia wazi kabisa kama ilivyokuwa katika siku za Lutu ndivyo itakavyokuja kuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu.. Wote tunajua jinsi dunia ya leo ilivyo tofauti sana ile ya zamani, ustaarabu uliopo leo hii ni mkubwa sana, utajiri uliopo duniani leo hauwezi kulinganishwa na ule uliokuwepo wakati ule, teknolojia, elimu, uchumi, miundombinu ni ya ajabu sana, kiasi kwamba ukimleta mtu wa karne ya 18 ukamuonyesha miji ya kisasa iliyopo duniani pamoja na teknolojia tulizonazo anaweza kusema huu sio ulimwengu wa wanadamu, bali ni kitu kingine…

Lakini mambo hayo mawili yanakwenda sambamba, “mafanikio pamoja na uovu vinashadiiana”.. Leo hii huoni jinsi ndoa za jinsia moja zinavyohalalishwa kila mahali mambo ambayo huko zamani hayakuwepo?, ndoa za wanyama na wanadamu, uzinzi sasahivi kila mahali mtu akiwa na simu ya mkononi tu, tayari anaufahamu uzinzi wote wa ulimwenguni..jambo ambalo hata sodoma halikuwepo, Mungu leo hii anatukanwa hadharani, ukipeleka habari za Mungu tu unaonekana kama mpinga-uhuru wa haki za kibinadamu, unaonekana kama mtu wa kale mwenye itikadi za kizamani.

Na wana wa Mungu wanapoona, mbona Mungu hachukui hatua yoyote dhidi yao, nao pia wanakwenda kujichanganya na maovu yao, ..Hawajui kuwa wanajiangamiza wao wenyewe bila kujua.

Kule Sodoma..Siku ya maangamizo ilipofika haikumaliza hata siku moja, mji ile ilikuwa imeshakuwa jivu yote..Vivyo hivyo na siku ya maangamizi ya huu ulimwengu ambayo ipo mbioni kutokea ambayo biblia ilishasema itakuja kwa ghafla sana, tena na cha kuogopesha zaidi itakuja katika kipindi cha amani,..soma.

1Wathesalonike 5:2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Sasa kama na wewe upo katikati ya sodoma, usidhani itakuwa ni rahisi, kupona wakati huo ..

Mungu alishatuasa watoto wake tutoke huko, tujitenge nao mambo ya ulimwengu.. (Ufunuo 18:4)..Tusiyakaribia hata kidogo…Tutoke Sodoma wala tusiikaribie hata kidogo…Tukae nayo mbali sana maelfu ya Maili…Kumbuka sio tu Sodoma na Gomora pekee yake ndio ziliteketezwa wakati wa Nuhu..Biblia inasema hata ile miji iliyokuwa kando kando ya Sodoma na Gomora iliteketezwa pia (kasome Yuda 1:7)..Haikuwa na maasi kama Sodoma na Gomora..lakini kitendo tu cha kuwa karibu na miji hiyo tayari ilikuwa imeshanajisika nayo pia..Kadhalika leo..tunaaswa tukae mbali na uchafu wa dunia hii, wala tusifungwe nira na wasio amini kwa jinsi isivyo sawasawa. (2Wakorintho 6:14) ili nasi tusije tukachanganywa huko huko katika hasira ya Mungu.

1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”.

Unaona? Ikiwa umeokoka halafu bado unapenda kwenda disko basi ujue upo Sodoma, umeokoka na bado unasikiliza miziki ya kidunia, unavaa nguo za kikahaba, vimini na masuruali, ujue unaishi sodoma bado..Na siku ile ya Unyakuo hutakwenda popote.. utabaki hapa chini ukingojea hukumu ya Mungu kulingana na Biblia.

Ni maombi yangu, hutachukuliwa na tamaa kama za Lutu, kwa kupenda mambo haya ya kitambo ya ulimwenguni, bali sote tutajitahidi tumtazame Kristo na mambo ya ufalme wa mbinguni, hadi siku ile ya ukombozi wetu utakapofika.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MTU ASIYE PAMOJA NAMI YU KINYUME CHANGU.

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

MAJINI WAZURI WAPO?

NI NINI KINAKUPATA UNAPOIPUUZIA INJILI?

INJILI YA MILELE NI IPI KATIKA BIBLIA?

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

SADAKA YA MALIMBUKO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Nini maana ya lile fungu linalosema mwenye nacho ataongezewa na yule asiyenacho ata kile Kodogo alichonacho atanyang’anywa?