Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

SWALI: Je! Mungu anashindwa na mwanadamu? Kama sio Kwanini siku ile aliposhindana na Yakobo alikiri kushindwa?

Mwanzo 32:25 “Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.

26 Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki.

27 Akamwuliza, Jina lako n’nani? Akasema, Yakobo.

28 Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda”.

JIBU: Jibu ni ndio Mungu anakubali kushindwa, Pengine utauliza unakubalije kushindwa wakati yeye ni Mungu asiyeshindwa na chochote.

Tabia za Mungu sio kama  zetu, Mungu huwa anathamini sana, NIA, BIDII na MATAMANIO ya mtu, kiasi kwamba hata kama matamanio hayo yatakuwa  kinyume na mpango wake, au mapenzi yake, ikiwa tu mtu huyo ataendelea kuking’ang’ania basi mwisho wa siku atamwachia, akipate anachokitafuta haijalishi kitakuwa ni kibaya au chema. Huko ndiko kushindwa kwa Mungu.

Na ndicho kilichotokea kwa Yakobo, aliposhindana na Mungu usiku kucha, akiomba apewe jambo ambalo halikuwa mpango wa Mungu kumpa wakati ule, lakini alipong’ang’ania bila kukata tamaa, kwa kupigana mieleka, ikambidi Mungu ampe tu kulingana na haja yake.

Jambo hili hili utaliona pia wakati ule Bwana Yesu akiwa duniani, utakumbuka kuwa mwanzoni kabisa alitumwa kwa Wayahudi na sio kwetu sisi mataifa, lakini siku moja alikutana na mwanamke mmoja king’ang’anizi wa kimataifa aliyeishi nchi moja iliyoitwa Tiro. Mwanamke huyo alikuwa na binti yake aliyesumbuliwa na mapepo. Na alipokutana na Yesu alitaka aponywe, lakini Yesu hakuongea naye chochote, kwasababu sio hakutumwa kwao, lakini mama huyo hakukata tamaa, baada ya kumlilia sana,  ndipo Yesu akafungua kinywa chake akamwambia, maneno haya;

Mathayo 15:24 “Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli

25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.

26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.

Unaona, hapo, neema ya wokovu ilikuwa haijatufikia bado watu wa mataifa, kwasababu Kristo alikuwa hajasulibiwa bado, lakini mwanamke huyu, aliiwahi kabla hata ya wakati wenyewe kujika, jambo ambalo lilikuwa kinyume kabisa na mpango wa Mungu. Na ndio maana Kristo alitumia maneno magumu kama yale ili mradi tu adhoofishe mataminio yake, akawa hajibiwi, akawa anaitwa mbwa. Lakini mwisho wa siku Yesu kuona bado ni king’ang’anizi basi akakubali kushindwa. Akampa haja ya moyo wake, kama alivyofanya kwa Yakobo.

Hata wewe leo hii, unaweza shindana na Mungu nawe ukamshinda, hilo linawezekana kabisa, pengine hukustahili kupokea  uponyaji wa ugonjwa wako sasa, kutokana na mambo uliyomkosea Mungu, pengine,hustahili kupewa hilo hitaji lako kwa sasa hivi, labda pengine  limekusudiwa ulipokee baadaye sana, baada ya miaka 15, pengine hustahili kuwa na hiyo karama sasa hivi, lakini uking’ang’ana na Mungu, anaweza kukusogezea karibu hilo hitaji lako haijalishi alitaka litimie baada ya miaka 20.

Na ndio maana Bwana Yesu alituambia mfano huu, naomba nawe pia uutafakari vizuri;

Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”.

Usichoke kung’ang’ana na Mungu wako..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

BWANA HUWAJUA HAO WAMKIMBILIAO.

kwanini Yakobo amefananishwa na mdudu?(Isa 42:14)

Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?

Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki;

Maswali na Majibu

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments