Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?

Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?

SWALI: Ni nini alichokifanya Yakobo kwa ile mifugo ya Labani mpaka ikaongezeka kwake kwa wingi kuliko ya mjomba yake?


Tukisoma biblia tunaona baada ya Yakobo kumtumkia mjomba yake Labani kwa miaka 14, ilifika wakati akataka sasa kwenda kujitegemea na kuilea  familia yake mwenyewe. Ndipo Labani akamwuliza amlipe nini?

Sasa kwasababu Yakobo alikuwa anachunga mifugo yake, na kwa njia hiyo Mungu alibariki Labani kuwa na mifugo, basi Yakobo akamwomba  sehemu ya mifugo yake akaichunge ili ile itakayozaliwa baadaye iwe ni mshahara wake. Ndipo Labani akakubali akaingia naye mapatano kuwa Yakobo ataichukua tu ile mifugo yenye madoa na marakaraka, na myeusi, lakini ile mingine atamwachie yeye. Na kwamba kile kitakachozaliwa kikiwa ni cha marakaraka basi kitaendelea kuwa ni cha Yakobo lakini kikiwa ni kingine basi mali hiyo ni ya Labani.

Hivyo, Labani alivyoona hivyo, akakubali kwa moyo mkunjufu, kwasababu alijua kabisa hilo haliwezekani, na hata likiwezekana basi litakuwa ni kwa uchache sana. Ndipo wakakubaliana kwa moyo mmoja,Yakobo akawachukua wale wenye madoadoa na marakaraka wakatenganana kwa umbali wa mwendo wa siku tatu.

Ndipo Yakobo akabuni njia yake. Tusome..

Mwanzo 30:35 “Basi akatoa siku ile mbuzi waume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe.

36 Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia.

37 Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito.

38 Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.

39 Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka.

40 Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani.

41 Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito,

42 lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo.

43 Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda”.

Kama tunavyosoma hapo, Yakobo, alikwenda kusimamisha fito za miti, mahali ambapo mifugo inanywea maji, kwa kawaida mifugo inakutanika mingi sehemu moja mahali pa kunywea maji na hivyo ni rahisi kukutana kwa ajili ya kuzaliana., Lakini biblia haituelezi chochote, ni nini lengo la Yakobo kufanya vile, alikuwa analengo gani pale watakapozitazama zile fito, pengine labda alidhani zitasisimua homoni vina saba vyao na kusababisha wazae wanyama wenye maraka raka, au zile fito ziliwasaidia katika kuzaliana kulingana na jamii yao kwa haraka, hatujui imani ya Yakobo ilikuwa ni nini, pengine alikuwa anajaribu kutumia njia za kisayansi aliyoingundua mwenyewe au kusimuliwa, vilevile hatujui  biblia haijatueleza..

Lakini tunachojua ni kuwa alichokifanya kwa mitazamo yake sicho ambacho kiliwapelekea wale kondoo zake na mbuzi zake kuzaliwa wenye marakaraka au madoa doa.. Utakuja kuliona hilo katika mistari inayofuata, alipokuwa akimwambia Raheli juu ya ndoto aliyoiota.

Mwanzo 31:7 “Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru.

 8 Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.

 9 Hivi Mungu akamnyang’anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.

10 IKAWA, WAKATI WALE WANYAMA WALIPOCHUKUA MIMBA, NALIINUA MACHO YANGU NIKAONA KATIKA NDOTO, NA TAZAMA, MABEBERU WALIOWAPANDA HAO WANYAMA WALIKUWA NA MILIA, NA MADOADOA, NA MARAKARAKA.

11 Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.

Unaona? Hivyo si fito zilizowafanya wale kondoo na mbuzi wazae wanyama wenye marakaraka bali ni nguvu za Mungu rohoni,.

Hata sasa, hiyo ni kutuonyesha kuwa Mungu akitaka kukubariki, haijalishi bidii zako nyingi kiasi gani, au uvumbuzi wako unaoudhani utakusaidia, Ukiwa mcha Mungu, ni Mungu ndiye atakaye kupa uwezo huo wa kuvipata. Japokuwa inaweza kuonekana kwa nje kama ni wewe ndio uliyefanya kwa ushapu wako. Bali kiuhalisia si wewe, ni Mungu ndiye aliyekutia nguvu.  Kama Yakobo asingekuwa mcha Mungu, unadhani ni nini angeambulia pale kama sio majani ya fito tu.

Kumbukumbu 8:12 “Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;

13 na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;

14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa……………….

17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo

18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo”.

Bwana atusaidie tulishike agano lake.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

SAUTI NI SAUTI YA YAKOBO, LAKINI MIKONO NI YA ESAU.

Ni udhaifu gani ulikuwa katika macho ya Lea mke wa Yakobo?

Yakobo alikuwa na watoto wangapi?

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Hurmphrey
Hurmphrey
1 year ago

Nashukuru Mungu sana kwa neema haliyo wapa ya kuchambua maandiko kupitia Nguvu za Mungu