NI MAJIRA YAPI YA NEEMA WEWE UPO?

NI MAJIRA YAPI YA NEEMA WEWE UPO?

Kuna wakati wa kukokotwa-kokotwa, lakini kuna majira ya  kuachwa ufanye maamuzi mwenyewe, na usipofanya unakufa. Mtu aliye mchanga kiroho, ni rahisi Mungu kuchukuliana naye katika mambo yasiyofaa kutokana na uchanga wake kwa siku zile za awali, lakini haiwezi kuwa hivyo siku zote, kwa jinsi siku zinavyokwenda, kusukumwa sukumwa hakutakuwepo, ni kuwa makini sana!.

Ukitafakari habari ya Mke wa Lutu, unaweza kupata picha halisi jambo hili lilivyo, yeye alidhani ataendelea kuvutwa-vutwa tu nyakati zote, lakini walipofikishwa mahali Fulani, nje kidogo ya mji wameshaijua njia, waliambiwa wajiponye wenyewe nafsi zao, lakini yeye akageuka nyuma, na wakati ule ule akawa jiwe la chumvi.

Mwanzo 19:15 Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. 

16 AKAKAWIA-KAWIA; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, KWA JINSI BWANA ALIVYOMHURUMIA, wakamtoa wakamweka nje ya mji. 

17 Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea.

Hatari tuliyonayo sisi tuliopo katika siku hizi za mwisho, katika kanisa hili la Laodikia (Ufunuo 3:14-21), ni kwamba tunafahamu mambo mengi, na tumeshaona mifano mingi kwenye maandiko na kwenye historia, lakini geuko la dhati ndani ya wengi halipo, tukifikiri  tutalinganishwa na wale watu wa zamani. Neema kwako wewe haifanyi kazi katika kukokotwa tena, bali katika kukimbia. Ilifika wakati Yesu hakuwaambia tena wanafunzi wake “nifuate”, aliwaambia na “ninyi mnataka kuondoka?”

Halikadhali, kama umeshaokoka, jichunge sana, dhambi usiifanye rafiki kwako, ukidhani kila kosa tu utakalolifanya upo msamaha, acha hayo mawazo, unajitafutia kuwa mke wa lutu. Neno la Mungu linasema;

Waebrania 6:4  Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5  na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6  wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7  Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu; 8  bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.

Ni kusimama imara, sio tena kumbelezewa injili, sio tena kukumbushwa-kumbushwa wajibu wako wewe kama mkristo, na kuambiwa kaombe, nenda ibadani, mtafute Mungu, acha anasa, soma biblia. Ni wakati wa kujitambua kuwa sasa umeshatolewa nje ya mji, changamka, zama ndani ya Kristo. Acha kuwa vuguvugu utatapikwa, zama hizi ni zama za uovu. Wokovu wa mawazo mawili sio sasa, neema hiyo haipo kwetu mimi na wewe siku hizi za mwisho. Injili ya maneno laini, isikupumbaze, fanya Imara uteule wako na wito wako.

Ufunuo 22:10  Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11  Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa

12  Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

Kimbia, usiangalie nyuma.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je! “majira na sheria” mpinga-kristo atakayokuja kubalisha ni kupindua siku ya sabato na kuwa jumapili?

Nini tofauti ya Majira na Wakati?

UMEJIANDAAJE KWA NYAKATI ZA KUWA PEKE YAKO?

WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments