Je ni sahihi kuweka walinzi kulinda mali zetu?

Je ni sahihi kuweka walinzi kulinda mali zetu?

SWALI: Je ni sahihi kwa sisi tuliookoka na tunaomtegemea Mungu kuweka walinzi kulinda mali zetu  au mali za kanisa?. Kwasababu Biblia inasema Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure (Zab.127:1).

JIBU: Si dhambi kuweka walinzi au kuweka ulinzi katika mali zako, tena ni jambo la busara zaidi na la hekima. Unapokuwa na biashara yako au kazi yako ambayo ni halali inayompendeza Mungu, na ndani ya yake una mali nyingi, basi ni hekima kuweka ulinzi na pia kuifunga na kuhakikisha haitachukuliwa au kuibiwa kirahisi. Sio dhambi kabisa kufanya hivyo.

Kitu pekee ambacho si sawa na hakimpendezi Mungu, ni sisi kutegemea hao walinzi kama ndio msaada wetu na tegemeo letu la mwisho. Hapo ndipo linapokuja hilo neno..

Zaburi  127:1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure”.

Kinyume chake ni kweli, Bwana akiijenga nyumba wajengao hawafanyi kazi bure, kadhalika Bwana akiulinda mji wakeshao hawakeshi bure. Vile vile Bwana akiwa upande wetu kwa chochote tukifanyacho, hicho tunachokifanya hakitakuwa bure.

Ipo mifano kadha wa kadha katika biblia ya kujifunza, lakini itoshe tu leo kujifunza juu ya Nehemia, mtumishi wa Mungu. Wakati alipopata maono ya kwenda kuukarabati mji mtakatifu Yerusalemu, alikutana na vizuizi vingi, vya watu kuyapinga hayo maono..Hivyo ikampelekea kuingia katika hatari kubwa hata kufikia kupoteza maisha yake, lakini yeye alikuwa anamcha Mungu, na kumtegemea..na alimtegemea kwa kila kitu, lakini ulipofika wakati wa kuijenga nyumba ile hakuwa na budi ya kumwomba Mungu na pia kuweka walinzi huku anaifanya kazi ile… Lengo ni ili wasirudishwe nyuma na maadui zao..

Nehemia 4:7 “Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno;

 8 wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.

9 BALI SISI TULIMWOMBA DUA MUNGU WETU, TENA TUKAWEKA WALINZI, MCHANA NA USIKU, KWA SABABU YAO, ILI KUWAPINGA”.

Umeona, waliomba dua na pia wakaweka walinzi, lakini pamoja na kuweka walinzi, tumaini lao lote halikuwa kwa hao walinzi, bali walimtumainia Mungu, hivyo hawakukesha bure katika kuujenga huo mji na kuulinda, ndio maana mpaka leo kipande hicho cha ukuta kulichojengwa na Nehemia kipo Israeli, pale Yerusalemu maelfu ya miaka imepita bado sehemu ya ukuta ipo mpaka leo. (Tazama picha juu).

Hao waliweka walinzi na kukesha kuulinda na kuujenga mji, na mpaka leo sehemu ya ukuta ipo, kazi yao haikuwa bure..Lakini kama wangeweka walinzi na kuujenga huku wakizitumainia nguvu zao, hapo lingetimia hilo neno.. “Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye afanya kazi bure”..Ni wazi kuwa wangeshambuliwa na maadui zao na huo mji wanaoujenga wasingemaliza.

Kwahiyo tunajifunza, tuwapo na kitu chochote ambacho Mungu katubariki kwa hicho, basi hatuna budi kukutunza na kukulinda kwa kadiri tuwezavyo, Sio hekima wala akili kuacha milango wazi ya nyumba yako usiku, au kuacha wazi mlango wa sehemu ya biashara yako mpaka asubuhi ukiamini kuwa hakuna atakayeingia na kuzichukua mali zako. Nakuambia ukweli ukija asubuhi hutakuta chochote, kwasababu unamjaribu Mungu.

Itokee bahati mbaya umesahau kufunga mlango wa maingilio ya sehemu za mali zako, hapo Bwana ataingilia kati kuzilinda mali hizo utazikuta salama kimiujiza miujiza tu, haijalishi zipo mazingira gani… lakini kamwe usimjaribu Mungu kwa kuacha kukilinda kile ulicho nacho, huku ukisema Mungu atazilinda tu..hapo utakuwa unamjaribu Mungu na unatenda dhambi..

Na sio vitu vya mwilini tu ambavyo tunajukumu la kuvilinda, bali hata vitu vya rohoni, ambavyo ndio vya muhimu zaidi. Na cha kwanza kabisa cha kukilinda ni WOKOVU mtu alioupata..

Biblia inasema..

Ufunuo 3:11  “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Na pia inasema..

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

 24 Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.

 25 Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa”

Umeona?..baada ya kumpokea Yesu sio wakati wa kujilegeza na kusema nipo salama!..bali ndio wakati wa kukilinda kile ulichokipokea..kwasababu WIZI wa rohoni upo!!…shetani anatafuta kwa hali na mali kuiba vile vya rohoni tulivyopewa na Mungu.

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba ulinzi wa vitu vya rohoni na mwilini unapaswa uwe tabia ya kila mkristo, kama vile ilivyo tabia ya Mungu kutulinda sisi, yeye ijapokuwa ametupa tayari wokovu lakini bado anawatuma malaika wake kutuzunguka kutulinda pande zote usiku na mchana, hivyo na sisi hatuna budi kulinda vile tulivyopewa.

Bwana atubariki.

Kama hujampokea Yesu, nakushauri ufanye hivyo leo, hizi ni siku za Mwisho, na parapanda inakaribia kulia na Kristo kuchukua watu wake, kwenda nao mawinguni, Je! Utakuwa wapi siku hiyo?

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

Swali: Je Ni sahihi kwa Mkristo kupeleka kesi mahakamani?

 Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Ubarikiwe Mtumshi wa Mungu niko tayari kufanya kazi ya Mungu katika kwel yote Marko 9 38