Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

 Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

SWALI: Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako, mafuta ya upako au chumvi katika kufanya maombezi?


JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa kinachomponya mtu ni damu ya Yesu Pekee. Na ndani ya damu ya Yesu ndio kuna Jina la Yesu…Hivyo jina la Yesu linapotajwa ni tangazo maalumu la damu ya Yesu katika utendaji kazi wake, hivyo kila ugonjwa au tatizo kwa jina la Yesu linaondoka na kupotea kabisa!.

Kwahiyo haipaswi kwa vyovyote vile kufikiri au kuamini kwamba kitu kingine zaidi ya damu ya Yesu kinaweza kumponya mtu au kinaweza kuondoa matatizo ya mtu au kumbariki. Kuamini hivyo hakuna tofauti na kuabudu sanamu.

Sasa pamoja na hayo, Mungu ameruhusu uponyaji wa damu ya Yesu wakati mwingine ufuatane na maagizo Fulani…Kwamfano daktari anaweza kutoa dawa kwa mgonjwa wa ngozi na kutolea maagizo kwamba akameze vidonge hivi na maji ya kutosha..au akampa vidonge vingine na kumwambia akavitie kwenye maji kisha aogee, afanye hivyo mara tatu kwa siku tatu na huo ugonjwa huo wa ngozi utamwisha..Au anaweza asimpe kidonge chochote na badala yake akamchoma sindano tu na bado ukapona vile vile…Ni kwajinsi tu yeye atakavyopenda kuchagua njia iliyobora.

Na Roho Mtakatifu ni hivyo hivyo…katika suala la kumponya mtu, mara nyingine anaweza kuambatanisha na maagizo Fulani…aidha mtu atumie mafuta, au udongo kwa jinsi Roho Mtakatifu atakavyopenda…kama alivyofanya Bwana katika Yohana 9:6 (alimwongoza atumie tope la mate yake), au anaweza akampa mtu maelekezo atumie unga kama Elisha alivyofanya katika 2Wafalme 4:41, au chumvi kama alivyofanya Elisha katika 2Wafalme 2:21 au kutumia leso kama alivyofanya Paulo katika Matendo 19:11-12..au chochote kile…Lakini ni kulingana na uongozo wa Roho Mtakatifu…Na sio kama mtindo!..kama inavyofanyika leo na wengi wanaofahamika kama watumishi wa Mungu.

Leo hii kila tatizo linatatuliwa na chumvi wanazoziita chumvi za upako, au mafuta …hata mtu akiugua tu, suluhisho ni mafuta ya upako! Au maji ya upako!..kila kitu ni mafuta ya Upako na ni kitendo endelevu na kinachojirudia kila siku…Sasa hilo sio agizo la Roho Mtakatifu…kwasababu Roho Mtakatifu hana mtindo Fulani/staili Fulani ya kumponya mtu.

Kwasababu hata Bwana Yesu sio kila mahali watu walipomjia mwenye matatizo Fulani alikuwa anatema mate chini na kutengeneza tope na kuwapaka na kufunguliwa shida zao!…utaona alifanya hivyo mara moja tu! Na tena kuna jambo alikuwa anafundisha, Na hakuna sehemu nyingine yoyote alirudia kufanya hivyo, kuonyesha kuwa nyakati zote alikuwa anasubiria maagizo ya Roho Mtakatifu, na hakufanya agizo Fulani la Roho Mtakatifu kuwa kama mtindo.

Na sio yeye tu! Hata Elisha hakuwa na staili/mtindo wake maalumu, wala hata Mtume Paulo ambaye nguo zake na Leso yake kuna wakati ilitumika hata kuondoa mapepo(Matendo 19:12)…utaona kuwa haikuwa hivyo kila mara, na wala Paulo hakugeuza kuwa kama mtindo..kwamba kila aliyekutana naye alimtupia leso ili afunguliwe!..hutaona akizituma nguo zake korintho au Galatia watu wakafunguliwe wala hakuwahi kuhubiri hayo mambo… sehemu kubwa sana alikuwa anatumia jina la Yesu…na alikuwa anamuhubiri Kristo na si mavazi yake wala leso zake. Na mitume wengine wote wa Bwana Yesu ni hivyo hivyo…tunamsoma Mtume Petro kuna wakati hadi kivuli chake kilikuwa kikimpitia mtu mwenye ugonjwa, Yule mgonjwa anafunguliwa! (kasome Matendo 5:15). Lakini hutaona mahali popote Petro akiitumia hiyo kama ndio staili yake/mtindo wa kuwafanya watu wafunguliwe…bali utaona mara karibia zote alikuwa anatumia Jina la Yesu tu!..

Matendo 3:3 “Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.

4 Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.

5 Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.

6 Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, SIMAMA UENDE.

7 Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.

8 Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu”.

Hapo Petro hakutumia “kivuli” chake!…Bali jina kuu la YESU KRISTO!.

Sasa utauliza mbona kuna watu wanayatumia maji ya upako, au mafuta ya upako kama mtindo wao na wanafunguliwa?

Wengi wanaofunguliwa ni wale ambao ni wachanga kiimani, ambao ndio kwanza wamemjua Kristo, au wameingia kwenye imani ya kikristo, Hivyo Bwana anaruhusu wapokee miujiza yao kwa njia yoyote ile..ili wazidi kumsogelea Mungu katika hivyo vipindi vya awali, lakini baada ya kipindi Fulani kupita wakaujua ukweli, au kusikia injili kwa muda mrefu na kushupaza shingo, zinabadilika kwao kuwa ibada za sanamu, na havitawapii chochote zaidi ya kuzidi kuwaweka mbali na Mungu, na hata wakati mwingine kuingiliwa na mapepo, na kupoteza hata vile walivyo navyo kwasababu ni ibada za sanamu…wanatanga huko na huko kutafuta na kununua maji ya upako, chumvi ya upako…Na kwasababu wengi wao hawapendi kuzidi kumjua Mungu wanadanganyika!

Na manabii wengi wa uongo wamezuka sasa, katika siku hizi za mwisho kama ilivyotabiriwa…Mungu ameachilia nguvu ya upotevu kwa wale wote wanaoukataa ukweli…Na nguvu hiyo ya upotevu kaiweka ndani ya manabii wa uongo…Na lengo la nguvu hiyo ni ili watu wote wanaoukataa ukweli wazidi kudanganyika!…ili tofauti ya magugu na ngano ionekane kwaajili ya mavuno.(Mavuno hayawezi kuja bila magugu na ngano kujitenga kisawasawa!..)

2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Hivyo ni wakati wa kuwa makini sana na kuwa macho, na kujihadhari na roho zidanganyazo!…Kama hujapewa maagizo yoyote na Roho Mtakatifu basi usikurupuke kutumia maji,chumvi, udongo, au chochote kile ni hatari sana kwa roho yako!…Tumia Jina la Yesu tu pekee linatosha…

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 693036618/ 0789001312

Mada Nyinginezo:

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

BIRIKA LA SILOAMU.

Nini tofauti kati ya Amri, sheria na Hukumu?

Mtu astahiliye hofu ni yupi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
NURU MFAKO
NURU MFAKO
2 years ago

Amen,SOMO zuri sana, Mungu aendelee kukutia nguvu katika kuifanya kazi yake.

Julius R.
Julius R.
3 years ago

nashukuru kwa masomo yako Mungu akubariki

Noel Sylvester ruhigwa
Noel Sylvester ruhigwa
3 years ago

Nimebarikiwa