MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.

MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.

Mathayo 17:21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

Kuna mambo ambayo kamwe hayawezi kutokea bila kufunga…Neno “kufunga” maana yake ni “kutokuruhusu kitu kiingie wala kitoke sehemu fulani”…..kwamfano kuku ili aweze kuwa na Watoto hana budi kupitia kipindi cha mfungo wa siku 21, kutaga mayai sio kuwa na Watoto, bado kuna kazi nyingine ya ziada…itambidi, ajizuie kula, ajizuie kuzurura-zurura mitaani…ajizuie kucheza na wenzake..ili asilipoteze lile joto, vinginevyo akiwa mzembe mayai yatakuwa viza..na ndege wote wa angani ni hivyo hivyo, upo wakati itawabidi waliache anga kidogo, wajifungie ndani kutamia mayai yao.

Na sio tu mfungo wa kutokujizuia kula unahitajika ili kuumba jambo jipya…bali pia mfungo wa Maisha…kwamfano ili mwanafunzi aweze kufanya vizuri katika mitihani yake…hana budi kufunga milango fulani fulani…atakwenda shule ya bweni (huko tayari ni kifungoni)..atakaa huko miezi hata 6 bila kutoka hata nje ya uzio wa shule, mbali na wazazi wake na ndugu zake, na mafariki zake wa mtaani…ni kama tu kuku aliyeko bandani, sio hilo tu peke yake, itamlazimu aache matumizi ya simu, tv, aache kuangalia tamthilia hizi au zile, movie, aache kabisa kuzurura…itambidi kila siku za muda wake wa masomo aishi Maisha ya kuitumikia elimu..ataamka mapema asubuhi, atachelewa kulala…Sasa anafanya hayo ili asilipoteze lile joto…

Kwasababu anajua akishika mambo mawili au Zaidi kwa wakati mmoja…hatafaulu…kichwa hicho hicho kimoja akikijaza tamthilia, movie na miziki na wakati huo huo masomo…HATAFAULU!…Kwahiyo ni bora aache kimoja afuate kingine…Na Zaidi ya yote anakuwa radhi kuvumilia vyakula vibovu vya shuleni mpaka anahitimu ili tu apate anachokitafuta…

Vivyo hivyo…na katika Imani…hatuna budi kufunga baadhi ya mambo ili TUPATE YALIYO BORA!…Utasema mimi miaka yote nimeshindwa kuushinda uasherati…ni kwasababu haujaamua kuutoa maishani mwako…bado hujafunga baadhi ya milango!…Mbona wengine waliookoka wanaweza kwanini wewe ushindwe?..maana yake tatizo lipo kwako sio kwa Mungu wako!….Hujafunga hiyo milango ya uasherati…bado kuna vimelea vinavyokuchochea wewe kuendelea kuwa hivyo ulivyo…na hivyo si vingine Zaidi ya kampani ulizonazo, au picha unazoziangalia, au mazungumzo unayoyazungumza kila wakati yenye maudhui ya kizinzi, au mitandao unayoitembelea, au mtu unayeishi naye…Kama ukifunga kweli kweli na ukamaanisha kuutafuta uso wa Mungu…hayo mambo hayatakuendesha kamwe!!…

Kwanini hulielewi Neno la Mungu unapolisoma na huku umeshaokoka?… ni tabia tu uliyonayo!…na sababu zake ni zile zile za kwanini mwanafunzi haelewi anaposoma…Ni kwasababu hajaamua kuacha kila kitu na kuongeza umakini kwa kile anachokisoma….Utaona anafungua tu kitabu na kusoma Mada iliyopo katikati ya kitabu, halafu analalamika haelewi…sasa ataelewa vipi?..na wakati mada za kwanza zilipokuwa zinafundishwa darasani yeye alikuwa anacheza huko nje wakati wenzake wanasoma?…

Hali kadhalika utaelewa vipi kitabu cha Yeremia wakati madarasa ya biblia yanayofundishwa makanisani huudhurii??..Hujawahi hata kukisoma kitabu cha Mwanzo peke yako na kukimaliza…utakielewa vipi kitabu cha kutoka?…wakati wa asubuhi au jioni wa utulivu ambao ungetakiwa kukaa chini kwa bidii yako mwenyewe kusoma Biblia…wakati huo ndio unafungua whatsapp na facebook?, kusoma Habari za kidunia??…halafu unalalamika hulielewi neno?…Nakuambia ukweli biblia ni kitabu kirahisi sana kukielewa kuliko vitabu vyote endapo tu, tutaamua kumtii Mungu na kuzingatia kulisoma Neno lake kwa bidii…

kwasababu Roho Mtakatifu yupo kutusaidia kulielewa, kwahiyo kazi inakuwa rahisi sana…

Lakini kama Maisha yako hutajishughulisha kutenga muda kusoma Neno lako mwenyewe, angalau kuanzia kitabu cha Mwanzo, ukatulia, ukasoma hatua kwa hatua..bila kutegemea kufundishwa na mtu…utajikuta ufahamu wako unakuwa kwa haraka sana…na KUZALISHA KITU KIPYA KATIKA MAISHA. Lakini ukipalilia tabia ya kutolisoma kwa bidii Neno, hautazalisha chochote…

Hivyo funga leo vitu ambavyo ulikuwa umeviachia mlango wazi katika Maisha yako, ambavyo vinazuia wewe kutoivisha kitu chochote kipya!…matamthilia ya Kikorea, ya ki-Nigeria, ya-Kifilipino, ya Ki-hindi na mamovie yote pamoja na MIPIRA!…ni mambo yanayoondoa joto la Maisha yako ya kiroho, Jitenge achana nayo Jiondokee..…Wewe utaona unajifurahisha tu, lakini katika roho mayai uliokuwa unayatamia yanazidi kupoa na kuwa viza!…kwasababu tulivyoumbwa hatuwezi kushikilia mambo mawili kwa wakati mmoja.

Je Umewahi kuwasikia watu wanaosema “Ngoja nikatazame tamthilia fulani nipoteze mawazo au ngoja nikatazame movie au mpira nipoteze mawazo au kupunguza stress?”…. umewahi kujiuliza kwanini wanahusisha na neno “kuondoa stress au kupunguza mawazo”?….Ni kwasababu ni kweli wanapokwenda kutazama hayo mambo yanasababisha kile kitu ambacho kilikuwa kimeingia ndani ya mioyo yao kipotee, hivyo kama wakiendelea kujiburudisha hivyo kwa kipindi fulani hatimaye kile kitu ambacho kilikuwa kinawaumiza kichwa kinamezwa na zile burudani….Hali kadhalika kama mtu alikuwa ametoka kusoma Neno vizuri na kulielewa…ile ni mbegu inakuwa imepandwa ndani yake….Lakini sasa anapotoka na kwenda kutazama vichekesho, au mipira, au movie, au tamthilia wakati wote au kuhudhuria hudhuria party party zisizo za muhimu, kidogo kidogo kile kilichopandwa ndani yake kinaanza kujizika….hata kama hapendi! Kitapotea tu!..na baada ya kipindi kupita atajikuta kakisahau kabisa….

Hivyo tunajukumu zito la kulinda kile kilichowekwa ndani yetu na Mungu ili tupate kile tunachokitafuta kumbuka biblia tena hili Neno.

“namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”.

Nyakati hizi ni za mwisho. Tukaze mwendo tuufikie mwisho mwema wenye mafanikio.

Kwani biblia inasema.. “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. (Ufunuo 3:11) ”…

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

DUNIANI MNAYO DHIKI.

ALIYOKUTANA NAYO YESU, YERIKO.

WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

MIJI YA MAKIMBILIO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amina..ubarikiwe