WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

Shalom,

Jina la mwokozi wetu, Mfalme wa Wafalme na Bwana wa mabwana, Yesu Kristo libarikiwe daima. Ni siku nyingine tena hivyo Nakukaribisha tuyatafakari pamoja maandiko.

Neno linasema..

Warumi 10:1 “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.

 2  Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa”.

Kama tunavyoweza kuona hapo kuwa “Juhudi” tu peke yake hazitoshi, kama hatuna maarifa ya kutosha ya kumwabudu Mungu, tutakuwa tunafanya kazi bure.. Na hapa ndipo kundi kubwa la sisi wanadamu tunaposhindwa kumfikia Mungu, tunaishia kuona kama vile Mungu hayupo na sisi japokuwa tunajibidiisha kwake..

Leo tutayatazama makundi mawili  ya watu wa namna hii katika biblia ambao kweli yana bidii kwa ajili ya Mungu lakini sio katika maarifa:

Kundi la kwanza ni lile la watu walio ndani ya Imani ya Kikristo.

Na Kundi la Pili ni lile lililo nje Ya Imani ya Kikristo, lakini linadai kuwa linamtafuta Mungu wa kweli na linampenda.

Tutayatazama yote mawili kibiblia, na ikiwa mimi au wewe, au sote  tunaangukia kwenye mojawapo ya makundi hayo basi tujithamini mapema na kugeuka haraka sana kabla ya kupotea kwetu.

Tukianzana na hili kundi la kwanza ambalo ni la wale walio ndani ya Kristo…

Sasa Katika biblia Kuna mtu anaitwa Martha. Huyu Siku moja alimkaribisha Bwana Yesu kwake. Lakini yeye hakujua Kristo anataka nini, badala yake akawa anajitaabisha na mambo mengine yasiyo na maana sana machoni pa Bwana, mara anakwenda kuosha vyombo, mara anakwenda jikoni kuandaa chakula, mara anachota  maji kwenye majagi kwa ajili ya wageni,  mara anafanya hiki mara kile,..Na kibaya zaidi kilichokuwa kinamkasirisha ni pale anapomwona mdogo wake, Miriamu hajisumbui kwa lolote ameketi tu pale miguuni pake akimsikiliza Bwana..

Martha kuona vile akidhani ni utomvu wa nidhani, akamsemelea kwa Bwana ili aondoke pale..Lakini Bwana akasema..

Luka 10:41 “…. Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;

42  lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa”.

Sasa huyu ni mfano wa watu ambao wanaobidii kweli kwa ajili ya Mungu lakini si katika maarifa..Wanadhani Mungu anapendezwa na taabu zao na masumbufu yao na huku maagizo ya msingi ya rohoni wanayaacha yawapite..

Leo hii lipo kundi la wakristo, ambao, hawana muda wa kuyatafakari maneno ya uzima ya Kristo, hawana muda wa kusali, hawana muda wa kumwomba Roho Mtakatifu awafundishe mapenzi ya YESU, hawana hata muda wa kuutafuta ubatizo sahihi, lakini kwenye kwaya wapo na wana bidii sana, kwenye ujenzi wa kanisa wapo, na wanajitoa kwa bidii, kwenye michango yote wapo haiwapiti, wako tayari kufanya hiki au kile kwa ajili tu ya Mungu hawaachi, wanajitoa kweli hata usafi wa kanisa ni wenye bidii sana, lakini tukirudi kwenye bible-study tu, huwaoni,..

Ni kweli wanachokifanya si kibaya, wanajuhudi kwa ajili ya Mungu lakini si katika maarifa kama vile Martha..Hivyo mbele za Mungu wanaonekana hawajafanya chochote haijalishi bidii yao ni kubwa kiasi gani. Kwasababu mambo ya msingi wameyaacha. Kwasababu ni heri usiwe unaimba kwaya, ni heri ukawa hufanyi mambo mengine lakini Neno la Mungu unalishika kwa bidii na unalisoma sana na kulichunguza, na umebatizwa, na umepokea Roho Mtakatifu, unaweza ukakosa kitu cha kuchangia lakini ukawa ni mtu wa kusali sana, ukawa ni mtu ambaye haiwezi kupita siku hujajifunza biblia na kuisoma peke yako pasipo kusubiria mtu fulani akuelezee, huku ukimtegemea Roho Mtakatifu akufundishe n.k.

Kundi la Pili: Ni la watu ambao si wakristo, lakini wapo ulimwenguni kote wanadai kuwa wanamuheshimu Mungu.. Na wengi wao ni kweli wanao nia nzuri, na wanaweza wakawa na juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu kuliko hata wewe, lakini mwisho wake, watu wa namna hii, huwa ndio wanakwenda mbali kabisa na mpango wa Mungu, na wakati mwingine wanaiharibu kabisa kazi yake.. Na hiyo yote ni kutokana na kukosa maarifa ya kumwabudia Mungu.

Mfano wa watu hawa ni Mtume Paulo mwenyewe. Yeye kabla ya kumpokea Kristo alikuwa ni mtu mwenye bidii kwa Mungu kweli, lakini kwasababu alikosa maarifa matokeo yake akawa anawaua mpaka wakristo akidhani anamtolea Mungu sadaka (Wafilipi 3:6-7)..Na wayahudi wengine wote ndio walikuwa vivyo hivyo kama yeye.

Wengine walio katika kundi hili ni waislamu..Sio wote unaowaona wanawachinja watu kule Syria na Iraq na Somalia ukadhani hawampendi Mungu..hapana, wengine wanafanya vile kwasababu wanadhani ndio wanamuheshimu Mungu, kama mtume Paulo, kumbe juhudi zao si katika maarifa na hivyo inawafanya wazidi kupotea Zaidi na kwenda kinyume na Mungu, na hata kuwa adui wa Mungu kabisa..Kama vile Neno linavyosema..

Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa..”

Lakini maarifa sahihi yanapatikana wapi?

Ndugu, ni kwanini tunasisitiza sana YESU, YESU, YESU,? Nikwasababu maarifa yote na hekima yote zinapatikana kwake tu (Wakolosai 2:3). Huyo tu, ukimpata, au ukimjua katika usahihi wote, basi ujue kuwa utamwabudu Mungu katika maarifa na sio katika ujinga.

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”

Na Yesu yupo wapi? Jibu ni kuwa Yupo katika NENO lake(biblia)..Hivyo kama wewe ni muislamu au upo katika dini nyingine yoyote, mgeukie Yesu sasa, mwamini yeye, ayaongoze Maisha yako. umwabudu Mungu katika maarifa anayoyataka, ili akufurahie..kwasababu anasema..

Yohana 14:6  “…Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”… Hakuna njia nyingine ya kumfikia Baba isipokuwa kwa kupitia Yesu.

Vilevile na wewe kama ni mkristo lakini bado unasua sua, unaishi kidini dini tu,..kwaya kwako ni muhimu kuliko kulisoma Neno, kutoa sadaka nyingi kwako ni muhimu kuliko kuutafuta ubatizo sahihi na Roho Mtakatifu, Huu ni wakati wako wa kujihurumia, na kugeuka na kuanza kumwabudu yeye katika Roho na Kweli, kwa kujifunza mapenzi yake katika Neno lake (biblia).

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu ni wakina nani?

Je! Mwanamke anapaswa afunikwe kichwa anapokuwa ibadani?

NI NINI TUNAJIFUNZA JUU YA MT. DENIS WA UFARANSA?

Chapa zake Yesu ni zipi hizo?

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

MTANGO WA YONA.

SAKRAMENTI NI NINI, NA JE! IPO KATIKA MAANDIKO?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Sanga Emmanuel
Sanga Emmanuel
1 year ago

Najifunza sana,naomba kuendelea kujifunza