UTAPATAJE RAHA NAFSINI?

UTAPATAJE RAHA NAFSINI?

Mathayo 11: 28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”

Kama ukiutafakari huo mfano Bwana Yesu alioutoa….utagundua kwamba aliwafananisha watu aliowaona mbele yao na punda wa kubeba mizigo ambao Bwana wao hao punda kawafunga NIRA shingoni na kuwabebesha mizigo waivute huko nyuma. Na kitu kingine Bwana Yesu alichokiona kwa hao punda ni kwamba wamefunga NIRA shingoni ambayo ni ngumu sana, pengine inachubua ngozi ya shingo sana…na sio hicho tu, aliona pia mzigo wanaobebeshwa na Bwana wao ni mkubwa sana, kuliko uwezo wao…Na lililobaya kuliko yote, ambalo naamini ndilo lililomfanya azungumze ni “tabia ya bwana wa hao punda”…kwani alikuwa ni mkali sana na sio mnyenyekevu…pengine alikuwa anawatandika viboko, na alikuwa anawaendesha kwa ukali, na awapi pumziko ni kazi tu mwanzo mwisho..

Hivyo Bwana Yesu kuona vile akawahurumia….akasema maneno yafuatayo..

“Njooni kwangu ninyi nyote(maana yake mwacheni huyo Bwana wetu mje kwangu mimi) msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha…..zingatia hilo neno “nitawapumzisha”..maana yake huko walipokuwepo walikuwa hawapumzishwi, lakini hapa wanaahidiwa Pumziko…Lakini hajaishia hapo tu anaendelea kusema…jitieni nira yangu mjifunze kwangu (maana yake vueni hiyo nira ngumu ya Bwana wenu mvae ya kwangu)..na pia mjifunze kwangu (maana yake mchukue mafunzo yangu ya namna ya kufanya kazi hizo za mizigo)…kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo (sio kama huyo Bwana wenu ambaye anawatumikisha kwa ukali na hana unyenyekevu)..Na Bwana Yesu anamalizia kwa kusema NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU.

Hebu tafakari hilo tukio…Ni sawa na wewe unafanya kazi mahali Fulani ambapo boss wako anakupa mshahara mdogo sana, halafu anakufanyisha kazi nyingi kuliko hata uwezo wako, halafu pamoja na hayo yote, anakuwa mkali kwako na kukunyanyasa…Na kisha anatokea mtu mwingine anakuhurumia anakwambia njoo fanya kazi kwangu, nitakupa mshahara mzuri, nitakupa kazi za wastani, kwakuwa mshahara wangu mimi ni mzuri na kazi zangu si nyingi…na zaidi ya yote mimi ni mpole na mnyenyekevu…nawe utapata raha maishani mwako?…Je utakataa kwenda???..Bila shaka utaondoka kwa miguu yote miwili pasipo kutazama nyuma..

Na ndivyo hivyo hivyo tunapokuwa dhambini…Biblia inasema atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi…maana yake kila ambaye hajampokea Yesu anakuwa chini ya utumwa wa shetani penda asipende…na shetani ni bwana anayetesa, asiye mnyenyekevu, mkali, na nira yake ni ngumu na mzigo wake ni mzito kwa ufupi ni muuaji, yupo kwa maslahi yake akutumie wewe kupata watu wengi wa kuwapeleka jehanamu na mwisho wa siku akumalizie na wewe…

Lakini Bwana Yesu anatokea leo mbele yako na kukwambia mwanangu…utumwa uliotumikishwa na shetani..unatosha, vua hiyo nira, tua huo mzigo…njoo kwangu UTAPATA RAHA NAFSINI..Je hutaki raha??

Hivyo kama hujampokea Kristo leo..huu ndio wakati wa kutua mzigo wako Kalvari…hupendi raha?..kama hupendi sawa unaweza kuendelea kubaki kwenye dhambi…lakini kama unataka raha nafsini mwako..sio wakati wakuichezea hiyo fursa..vua leo hivyo vimini, tupa hizo hereni, hizo lipstick zitupe, hizo suruali ulizokuwa unazivaa acha kuzivaa kuanzia leo…sigara na pombe ulizokuwa unakunywa, uasherati uliokuwa unaufanya wote uweke chini ni mzigo mzito…mfuate Yesu leo..na hakuna haja ya kuhadithiwa wala kusimuliwa baada ya kuviacha hivyo vyote..utaona mwenyewe raha itakayoingia ndani yako…utaona kama ulikuwa umechukuliwa msukule sasa umerudia akili yako timamu…utakuwa huru kuliko maelezo, wala hutatamani kumrudia shetani tena..utajilaumu kwanini hukumgeukia Kristo tangu zamani. Hata sisi tulikuwa hivyo, lakini raha hii tumeionja tukaona ni kweli.

Shetani atakuonea wivu baada ya kumkimbia, atakutishia hivi na vile, lakini usiogope utakuwa chini ya Bwana ambaye si mkali kama shetani wala si mkorofi maisha yako yote…

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?

AMEFUFUKA KWELI KWELI.

JE WAKRISTO TUNARUHUSIWA KUSHEHEREKEA VALENTINE’S DAY?

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Pius
Pius
2 years ago

Thanks