KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

Tukishaokoka tu hatujiishii tu kwenye kujitenga na dhambi, kama vile kuzini, kuvaa nguo za uchi uchi, kuiba, kula rushwa, kutoa mimba, n.k..Sio tu hapo bali pia tunapaswa tuishi maisha ya kujizuia na mambo mengine mengi… Yapo mambo mengi ambayo tunaweza kuyafanya lakini hatujui kuwa yanaweza kuzisonga imani zetu na wakati mwingine tushindwe kuzaa matunda..

Kwamfano rafiki yako wa kidunia anaweza kukwambia naomba nisindikize kwenye birthday ya rafiki yangu, jambo hilo linaweza lisiwe ni dhambi, lakini kabla ya kufikiria kufanya hivyo jiulize?, Je! Ni faida gani na hasara gani utapata kwenye shughuli kama hizo?..Faida inaweza ikawa ni kula na kucheka, lakini tusijidanganye, hasara rohoni zitakuwa ni nyingi kuliko faida? Ukitoka pale ndio utajua.

Au Kuna tamthilia fulani kwenye Tv, halafu unasema haina shida, ni burudani, lakini ukweli ni kwamba, akili yako yote itahamia kule, kitu kitakachokupa furaha ni pale unapoikumbuka ile tamthilia ilipoishia..Na hivyo unakuwa mtumwa wa hiyo.

Au Unaunga urafiki na kila mtu wa mtaani kwako, hata wale waovu, wewe kila mtu tu ni rafiki Kwanini usichague kuishi nao kama majirani, wa kusalimia na kujuliana hali, mpaka ijiingize ndani muwe marafiki, mkutane kila siku mjadili mambo mengine ambayo hata sio ya maana?.

Una magroup kama 50 ya kuchat whatsapp, kuanzia ya shule ya chekechea, mpaka chuo, magroup mpaka ya marafiki wa mtaani, mpaka ya michezo na ya vichekesho vya kila namna..Hayo yote yanakusaidia nini, rohoni? Lakini group la kujifunza biblia unalo moja tu..Akili yako inaposongwa na mambo mengi inaisonga ile mbegu ya Mungu iliyopandwa au inayopandwa ndani yako isikue (sawa na ule mfano Bwana Yesu alioutoa wa mbegu zilizopandwa kwenye miiba, ambazo zilisongwa na shughuli na hazikuzaa)

Kabla ya kwenda kuzurura huku na huko vijiweni ulishawahi kujiuliza kuna umuhimu gani wa kwenda huko?

Tukiishi maisha ya namna hiyo ya kutojizuia biblia inatuambia.. hatutaipokea tuzo kamwe tuliyowekewa mbele yetu.

1Wakorintho 9:24 “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.

25 Na kila ashindanaye katika michezo HUJIZUIA KATIKA YOTE; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika”.

Unaona Mtume Paulo anaendelea kusema…

“26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;

27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”.

Si kila kitu cha kuvutia tunapaswa tukijaribu, ni lazima tujifunze kujizuia, kama vile wanamichezo, na kuchagua vipi vya kuchukua na vipi vya kuacha.. ili kusudi kwamba tupate muda mwingi wa kutumia kumtafakari Mungu, na kusali, na kufanya ibada..Vinginevyo wakati wote tutaona ratiba imesonga, muda ni kidogo wa kujihusisha na mambo ya msingi ya wokovu wetu.

Ndio hapo Utashangaa unapojaribu kwenda mlimani au sehemu yako faragha kusali mara marafiki wanakupigia simu, wanakuuliza upo wapi, tunataka tuje? Mara muda wa tamthilia umefika unawaza umalize ibada haraka haraka uende ukaangalie(mawazo yako yote yapo kule), mara unafungua whatsap ili ukaangalie ni nini kinaendelea huko, na kwenye lile group lako moja la Neno ulilojiunga, hapo hapo message kama 200 zinaingia kutoka magroup mengine tofauti tofauti, yanakuvutia usome hizo message jiulize utapata wapi muda wa kulitafakari vizuri Neno la Mungu?.

Hivyo muda wako utakuwa ni wasongwa songwa tu hivyo daima.

Chagua marafiki tu wachache wa karibu, hao wengine kama wanaulazima wabakie kuwa marafiki wa mbali ambao hawawezi kujishikamanisha na wewe muda mwingi..Pia Acha kufuatilia movie na thamthilia za Kikorea na nyinginezo kwenye TV, ziache zipite,dunia hii inapita ndugu (na hayo ma-movie na matamthilia karibia yote yana maudhui ya kipepo, kuyafuatilia ni kujiongezea idadi ya mapepo tu maishani mwako.)… Left magroup yote yasiyo na maana, bakiwa na yale ya kujifunza Neno la Mungu,.na ya familia…Group la watu wa shule ya msingi ulilosoma miaka 10 au 20 huko nyuma linakusaidia nini kwasasa?..labda lingekuwa na maana kwako kama ungekuwa huna jukumu lingine la kuutafuta uso wa Mungu, lakini kwasababu umepewa jukumu lingine na mamlaka iliyo juu…hilo group la shule ya msingi ondoka, kwasababu linakuchukulia muda wako na ilihali huo muda ungeutumia kusoma biblia…Mbona kabla ya hii mitandao ulikuwa unaweza kuishi na ulikuwa na furaha tu..kwanini sasahivi ushindwe?

Futa mazoea na baadhi ya watu unaoishi nao mtaani, abakie kuwa jirani mwema kwako basi, lakini kuingiliana maisha futa uhusiano huo, sio lazima ujiunge vijiweni mwao..wala usiogope kwamba siku ukipata matatizo hawatakusaidia…(Bwana ndiye ngome yetu na kimbilio letu hatuna hofu na wanadamu, Waebrania 13:6), tunapomtii Mungu na yeye anakuwa upande wetu na si upande wa Adui.

Na baada ya kufanya hayo…utakuwa umeuokoa muda mwingi sana sasa utumie huo muda wako ulioupata, kuomba, kusoma biblia, kujifunza Neno la Mungu kwa bidii, kufanya ibada, nakuambia ukijijenga utamaduni huo licha tu ya kuwa utapata amani Fulani moyoni lakini pia utamwona Mungu maishani mwako kwa namna isiyokuwa ya kawaida. Atajifunua kwako.. Matokeo yake Utakuwa kiroho kwa haraka sana na kwa kasi, mpaka kumzalia Mungu matunda ndani ya kipindi kifupi sana..Lakini tukiyaendekeza maisha ya kutojizuia, miezi, itaenda, miaka itaenda, tutakuwa wale wale wachanga, ambao ni rahisi kuchukuliwa tena na ibilisi.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?

UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.

MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.

KWANINI USIICHAGUE TUZO ISIYOHARIBIKA?

NI NANI ALIYEWALOGA?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Rogath Henry
Rogath Henry
4 years ago

Samahani huyo ndugu mwenye hizo namba mbona hapatikani?

Rogath Henry
Rogath Henry
4 years ago

Samahani nina swali: je kufanya mazoezi ya viungo napaswa kujiepusha nayo?