VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

Karibu katika mwendelezo wa kujifunza vitabu vya biblia.

Kwa ufupi tumeshapitia vitabu vinne vya kwanza yaani kitabu cha Mwanzo, kutoka,Mambo ya Walawi na Hesabu na leo Kwa Neema za Bwana tutasogea mbele na vitabu vingine vinne vinavyofuata.

5) KUMBUKUMBU LA TORATI:

Kitabu hichi cha kumbukumbu la torati kiliandikwa na Musa, katika hatua za mwisho kabisa karibia na wana wa Israeli kuingia nchi ya Ahadi, Musa alipewa maagizo na Mungu aandike kitabu hichi kwaajili ya ukumbusho wa Torati..Kama jina lake lilivyo “kumbukumbu la Torati”..kwahiyo ni wazi kuwa kilikuwa ni kitabu cha kumbukumbu ya vitu ambavyo walikuwa tayari walishapewa au kuagizwa.

Mungu aliruhusu kitabu hichi kiandikwe kwaajili ya kizazi kipya cha wana wa Israeli, waliozaliwa katikati ya safari. Kwasababu wengi wa waliotoka nchi ya Misri walikufa njiani, kutokana na manung’uniko yao kwa Mungu ndio wale waliyoyaona matendo yote makuu Mungu aliyowatendea kwa macho yao lakini hawakutaka kumwamini na hiyo ikapelekea Mungu kuchukizwa nao, Mpaka kuwaahidia kuwa hakuna hata mmoja aliyetoka nchi ya Misri atayaeiona nchi ya Ahadi isipokuwa Kalebu na Yoshua tu! Ndivyo ilivyokuja kutimia kama ilivyo, wote walikufa wakabaki watoto wao..na hawa watoto waliozaliwa jangwani walikuwa hawamjui Mungu wa Israeli vizuri, hawakuyaona matendo Mungu aliyoyafanya wakiwa kule Misri,

kwahiyo ililazimika Kitabu kiandikwe ili kuwakumbusha TORATI ya Mungu aliyowapa wakiwa jangwani…ili wasije wakakengeuka na kumkosea Mungu kama baba zao na mama zao walivyofanya.

Kumbukumbu la torati 6: 4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.

5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

6 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;

7 NAWE UWAFUNDISHE WATOTO WAKO KWA BIDII, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo”.

Kwahiyo kwa maagizo ya kitabu hichi cha kumbukumbu la torati, watoto wote waliozaliwa katikati ya safari kiliwasaidia kuwakumbusha matendo ya Mungu yote aliyoyafanya tangu alipowatoa wana wa Israeli katika nyumba ya utumwa, Kwahiyo kilibeba kumbukumbu ya sheria na amri zote za Mungu kuanzia Amri kumi mpaka sheria za Makuhani (Walawi). Kwahiyo kwa ufupi tunaweza kusema ni kama kitabu cha marudio ya sheria, hukumu, na baraka..Mungu alizowawekea wana wa Israeli wakiwa njiani kuelekea Nchi ya Kaanani.(Ndio maana kikaitwa kumbukumbu la Torati)

6) KITABU CHA YOSHUA:

Kitabu cha Yoshua kiliandikwa na Yoshua mwenyewe, baada ya Musa kufa…Yoshua ndiye aliyekabidhiwa gurudumu na Mungu mwenyewe, kuwaongoza wana wa Israeli kuingia nchi ya Kaanani, baada ya kuzunguka miaka 40 jangwani..Kwahiyo Yoshua na Kalebu ndio waliosalia miongoni wa waliotoka Misri, hawa wawili ndio waliobebeshwa jukumu kukiingiza kizazi kipya cha wana wa Israeli katika nchi ya ahadi.

Kusudi kubwa la kuandika hichi kitabu cha Yoshua ni kuonyesha jinsi Wana wa Israeli walivyoshindana katika kutwaa urithi wao walioahidiwa…Hatua kwa hatua, jinsi walivyopigana vita na kuyatoa yale mataifa saba yaliyoshikilia urithi wao..Ni kitabu cha Vita, chini ya amiri jeshi wao Yoshua, Bwana aliyemtia mafuta kwa kuwashindania Israeli.

Yoshua 1: 1 “Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema,

2 Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.

3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.

4 Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu.

5 Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha”.

Kwahiyo rekodi yote ya vita, iliandikwa ndani ya hichi kitabu cha yoshua, ni sawa kipindi kile Rais Nyerere amwagize aliyekuwa mkuu wa Majeshi, aandike kitabu cha jinsi walivyovamia majeshi ya Uganda na kuyaangusha, kwenye vita dhidi ya Idd Amin, hatua kwa hatua jinsi walivyoteka jimbo moja baada ya lingine, na hatimaye jinsi walivyofanikiwa kuiteka Uganda yote na kuuangusha utawala wa Idd Amini. Ndivyo kitabu cha Yoshua kilivyo kinaelezea hatua kwa hatua namna Israeli walivyoteka na kuyatwaa maeneo ambayo Mungu aliwaahidia yatakuwa urithi wao katika nchi ya Ahadi.

Na hichi kitabu cha yoshua  pia kiliandikwa kwa dhumuni ya kuonyesha mipaka ya wana wa Israeli katika nchi mpya ya Kaanani waliyoiingia..kwamba kila Kabila liligawiwa sehemu yake..

Kumbuka vitabu hivi pia, havikuandikwa kama hadithi tu, kutufurahisha sisi tunaosoma wa vizazi hivi..hapana bali kila kitabu kina kimebeba maana kubwa sana na ujumbe mzito katika roho. Vitabu hivi vina maudhui makubwa sana katika kutufundisha sisi watu wa siku za mwisho. Hivyo nakushauri unaposoma vitabu hivi, omba Roho wa Mungu akusaidie kupata uelewa ya ujumbe kwa wakati wako husika. Na hakika utafurahia na kujifunza mengi sana.

7) KITABU CHA WAAMUZI:

 Kitabu kinachofuata ni kitabu cha Waamuzi kitabu hichi kiliandikwa na nabii Samweli. Kama jina la kitabu lilivyo “waamuzi” maana yake ni kitabu kinachozungumzia watu fulani ambao wamewekwa kutoa “suluhisho la mwisho la mambo yahusuyo nchi” au kwa lugha rahisi tunaweza kuwaita mahakimu.

Sasa Nabii Samweli ndiye aliyeagizwa na Bwana akiandike hichi kitabu cha Waamuzi, miaka mingi sana baada ya waamuzi wote kupita…aliagizwa aandike mambo waliyoyafanya hawa waamuzi moja baada ya lingine, kwani matendo yao yamebeba ufunuo wa KiMungu mkubwa sana ambao ungekuja kueleweka na vizazi vya mbeleni..ambao ndio sisi tunaosoma sasa.

Waamuzi walikuwa ni watu waliokuwa wanatoa maamuzi ya mwisho katika Israeli, baada tu ya wana wa Israeli kuingia katika nchi ya Kaanani..Mungu hakuwahi kuweka muamuzi katika nchi, lakini kwasababu ya kukengeuka kwa wana wa Israeli na kuiacha sheria na maagizo yake, Ndipo Mungu aliwatupa kwenye mikono ya maadui zao wateswe lakini walipomlilia Mungu, ndipo Mungu akawatumia mwokozi ili awaokoe kutoka kwenye shida zao, na huyo mwokozi Bwana aliyewatumia baada ya kuwaokoa katika shida zao ndio anakuwa kama MWAMUZI wa Taifa hilo kwa wakati huo.

Kitabu cha Waamuzi 2: 8 “Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi.

9 Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.

10 Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.

11 WANA WA ISRAELI WALIFANYA YALIYOKUWA NI MAOVU MBELE ZA MACHO YA BWANA, NAO WAKAWATUMIKIA MABAALI.

12 Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.

13 Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.

14 HASIRA YA BWANA IKAWAKA JUU YA ISRAELI, NAYE AKAWATIA KATIKA MIKONO YA WATU WALIOWATEKA NYARA, AKAWAUZA NA KUWATIA KATIKA MIKONO YA ADUI ZAO PANDE ZOTE; HATA WASIWEZE TENA KUSIMAMA MBELE YA ADUI ZAO.

15 Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.

16 KISHA BWANA AKAWAINUA WAAMUZI, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.

17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo.

18 Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.

19 Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi”.

Katika Israeli walipita waamuzi 16 Samsoni akiwa mmoja wao, na Gideoni na Debora, na Yefta n.k. Hawa wote waliiamua Israeli kwa vipindi tofauti tofauti walikuwa wana madaraka karibia yafanane na ya kifalme lakini hawakuwa wafalme..Na Samweli mwandishi wa kitabu hichi ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Mwisho katika Israeli, ni sharti mwamuzi wa Mwisho ndiye awe mwandishi kwasababu yeye ndiye atakayekuwa na rekodi ya matukio yote ya waamuzi waliomtangulia…Mwamuzi wa kwanza haiwezekani apewe jukumu la kuandika historia ya mbeleni, ni lazima yule wa mwisho ndio awe muhasisi….

Kwahiyo hichi kitabu cha WAAMUZI, unapokisoma kimebeba siri nyingi Mungu alizozificha ndani ya hawa waamuzi, ukimsoma Gideoni utaona ufunuo wa ajabu sana, Vivyo hivyo Samsoni, vivyo hivyo Debora, vivyo hivyo Yeftha na wengine wote.

8) KITABU CHA RUTHU:

Hichi kitabu cha Ruthu ni kitabu cha Nane katika Biblia..Kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Samweli yule yule aliyekuwa mwamuzi wa Mwisho wa Israeli, na aliyeandika kitabu cha Waamuzi, Bwana alimwongoza Nabii Samweli akiandike kitabu hichi kwani kimebeba maudhui makubwa sana katika mwili na katika Roho kwa kanisa lake..katika siku za mbeleni.

Kama jina la kitabu lilivyo RUTHU, Ikimaanisha kuwa ni kitabu kinachomwelezea mtu anayeitwa Ruthu. 

Kinaelezea maisha ya Ruthu, na kinaelezea jinsi Mungu alivyomlipaji wa thawabu kwa wote wenye haki, jinsi alivyomlipa Ruthu kwa uvumilivu wake na upendo wake..Mpaka kufanyika kuwa mama wa Bibi wa Mfalme Mkuu atakayekuja kutokea miaka michache mbeleni (yaani Mfalme Daudi)…

Mwana wa Mjukuu wa Ruthu ndiye Mfalme Daudi. Yaani katika uzao wa tumbo lake ukawa uzao wa kifalme. Jinsi gani Mungu anawapa thawabu hata watoto wa watoto wetu endapo sisi tukimcha yeye na kumpendeza na kuwa wavumilivu na wenye upendo kama wa Ruthu…Kumbuka Ruthu hakuwa hata mwisraeli alikuwa ni mtu wa mataifa lakini kwa upendo wake na uvumilivu wake…katika uzao wa tumbo lake akatoka Mfalme Mkuu Daudi, aliye Baba yake Suleimani…na katika Mnyororo huo ndio MFALME WA WAFALME, YESU KRISTO KATOKEA!! Ni Baraka kiasi gani…

Kwahiyo  hichi kitabu cha Ruthu kimebeba maudhui makubwa sana ya kutufundisha sisi watu wa siku za mwisho, tukianza kuzungumzia jambo moja baada ya lingine na kulitolea ufafanuzi tutamaliza kurasa na kurasa hapa…lakini wewe mwenyewe chukua nafasi ya kukisoma hichi kitabu cha Ruthu na Bwana atakupa ufunuo wa kipekee..na Pia utahitaji maelezo marefu juu ya kitabu hichi cha Ruthu unaweza kubofya hapa kwa uchambuzi zaidi >>> MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

Bwana akubariki sana..

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

 

Tutaendelea na sura zinazofuata Bofya hapa >>> VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 3


Mada Nyinginezo:

BWANA ALIMPA FARAO MOYO MGUMU, ASIMTII, JE! HAPO BWANA ATAMHUKUMU KAMA MKOSAJI SIKU ILE?

KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?

RAHABU.

HUYU AZAZELI NI NANI TUNAYEMSOMA KATIKA(WALAWI 16:8)

SANDUKU LA AGANO LILIKUWA LINAWAKILISHA NINI KATIKA AGANO JIPYA?

YATAFUTE YALIYO JUU SIKU ZOTE.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Sekuri olivier
Sekuri olivier
2 years ago

Tunashukuru sana kwa mafundisho mazuri ya biblia,lakini watu wengi wanatamani kujua ujumbe wandani uliopo ktk vitabo vya unabii, mfano kitabu cha Daniel na ufunuo, tunaomba tafsiri ya pembe ambalo lina mdomo kama mtu na hill hutamka maneno ya Ku mukufuru mwenyezi mungu. Ktiabu cha daniel