RAHABU.

RAHABU.

Shalom mtu wa Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo hilo ndilo linalotufanya tuishi mpaka sasa hivi mimi na wewe.

Leo, tutajifunza Juu ya huyu mwanamke anayeitwa Rahabu wengi wetu tunaifahamu historia yake, ni mwanamke aliyekuwa kahaba katika nchi ile ya Yeriko, kipindi kile wana wa Israel wanatoka Misri kuelekea nchi ya ahadi, Ikumbukwe kuwa mji wa Yeriko ulikuwa mji uliosifika sana wakati ule katika ukanda wote wa Jordani, kwa utajiri, wa kifedha, kilimo, na hata wa kijeshi, embu fikiria enzi zile tayari mji wote ulikuwa umeshazungushiwa ukuta, jambo ambalo hata sasa hivi nchi nyingi hata kama ni ndogo kiasi gani hazijafikia hiyo hatua.

Leo hii tunaona ni sehemu ndogo tu ya Taifa la China imeweka ukuta na imewekwa katika maajabu ya dunia, Jeriko leo hii ingekuwapo, tungeiweka wapi?..Ukuta ule ulikuwa mkubwa kiasi cha kuruhusu magari ya farasi kupita juu yake na watu kujenga nyumba zao kando kando mwa kuta zile. Na zaidi ya yote watu waliokuwepo kule walikuwa ni majitu kweli kweli watu hodari wa vita..Kwahiyo kulikuwa hakuna namna yoyote mji huu usiogopwe na mataifa mengine.

Sasa huyu mwanamke naye alikuwa akiishi ndani ya mji huu, akifanya kazi zake za ukahaba,lakini ndani yake kulikuwa ni kitu kingine tofauti ambacho kilimfanya asiangamie pamoja na mji ule na zaidi ya yote alihesabiwa miongoni mwa wana wa Israeli, na kama hiyo haitoshi aliingizwa katika uzao ya kifalme, wa simba wa Yuda, wa Bwana wetu Yesu Kristo.Mfalme Mkuu Haleluya!!.

Ni siri kubwa sana imelala hapo, na hiyo inatuhusu kwa sehemu kubwa sisi kama kanisa la Kristo, watu wa mataifa katika nyakati hizi za mwisho tunazoishi.

Sasa tukimchunguza Rahabu, utaona ni mtu ambaye aliyaweka moyoni sana yale mambo ambayo Mungu alikuwa anawafanyia wana wa Israeli kule Misri Miaka 40 iliyopita na shuhuda zote alizokuwa anawafanyia kule jangwani..Na hiyo ilimfanya aamini kabisa kuwa ufalme wao ni lazima uje kuangushwa tu siku moja na ndio maana utaona makazi yake aliyaweka ukingoni kabisa mwa mji, na sio katikati ya mji.

Yoshua 2:9 “akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu.

10 Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng’ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa.

11 Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.”

Hivyo utaona sasa wakati ule ulipofika wa wale wapepelezi kuingia katika nchi yeye ndiye aliyewakaribisha nyumbani kwake, na kuwaficha darini pale wenyeji wa nchi walipokuja kuwaulizia kwake, aliwaambia wameshaondoka kwake hivyo wawafuatie nje ya mji, ndipo baadaye baada ya wenyeji kuondoka akawashusha kwenye ukuta kwa kupitia dirisha la nyumba yake,

Lakini wale wapepelezi kabla hawajaondoka walimpa masharti matatu, ya kuzingati ndani ya siku chache zilizobakia kabla ya uharibifu kuanza, walimwambia:

1) Habari ile isijulikane na mtu mwingine yoyote isipokuwa yeye na familia yake tu.

2) Wafunge kamba ile nyekundu dirishani mwao ili siku ile watakapokuja kuuteketeza mji wawatambue.

3) Mtu yeyote asitoke nje ya malango:

Na kama tunavyosoma habari wana wa Israeli walipovuka tu Yordani, kuuzunguka ule mji, na baadaye kuanza vita, wale wapepelezi wawili wakamfuata Rahabu nyumbani kwake, na kumwondoa ndani yeye pamoja na ndugu zake wote, wakaweleta kambini walipokuwa wayahudi wengine wote kisha mji wote ukatetekezwa kwa moto hakukusalia kiumbe chochote kilicho hai.

Habari hii inatupa picha ya mambo yanayoendelea rohoni katika hizi siku za mwisho, Rahabu anawakilisha kanisa la Kristo (Bibi-arusi wa kweli) ambaye ameokolewa katika dhambi za uasherati wa kiroho unaondelea sasa hivi duniani.

Na cha kushangaza leo hii hakuna mtu yoyote asiyefahamu kuwa Kristo yupo mlangoni kurudi, na atakaporudi ulimwengu huu wote utateketezwa sawasawa na alivyoahidi hata ukimuuliza mtu asiye mkristo atakwambia nafahamu hilo. shuhuda zake tumezisikia tangu miaka 2000 iliyopita lakini bado watu wanaendelea kufanya maovu wakijifariji kwa kuta za dhambi walizojiwekea..Dalili zote zinaonyesha tunaishi katika kizazi ambacho kitashuhudia kurudi kwa pili kwa Kristo lakini watu bado wanafumba macho yao wasione hayo kama tu vile watu wa Yeriko walivyokuwa..

Lakini Rahabu japo alikuwa katika mji ule mwovu aliijenga nyumba yake ukingoni kabisa mwa mji, kuonyesha kuwa akili zake na mawazo yake yote yalikuwa nje! Kutazama mbali kinachokuja..Ndivyo walivyo wakristo wachache sana wa Bwana Yesu leo, japo wanaishi ulimwenguni lakini wapo ukingoni kabisa mwa ulimwengu, hawajichanganyi na uovu unaoendelea duniani mpaka kumsahau Mungu na ufalme wake ambao upo karibuni kutokea..Sikuzote mtu ukiwa katikati ya mji huwezi kuona au kujua yanayoendelea nje ya mji, ndivyo ilivyo kwa kundi kubwa la watu sasa, hawaoni kuwa Kristo yupo nje ya kuta zetu ni PARAPANDA TU! Inasubiriwa ilie wema waondoshwe waangamizi yaanze.

Tunaona pia Rahabu alipewa maagizo matatu, moja wapo, ni ile kamba nyekundu: Kuonyesha kuwa kitakachomwokoa mtu, ni agano lililokatika damu ya Yesu, na si kingine chochote, njia ni moja tu ya kumfikia Mungu, ikiwa humwamini Kristo leo huku unatumai uokoke kwa njia nyingine..utaangamia tu.Ni heri leo ukaitii injili uokolewe.

Pili aliambiwa mtu yoyote asitoke nje ya malango ya nyumba yako, atakayetoka hata kama ni ndugu yako damu yake itakuwa juu yake mwenyewe: Hii inafunua wale ambao wapo vuguvugu, katika siku hizi za mwisho ukiamua kumfuata Yesu mfuate kweli kweli, hakuna nafasi ya kuingia na kutoka, aidha aumue kuwa nje moja kwa moja, au ndani moja kwa moja…. vinginevyo utafananishwa na ule mfano Bwana Yesu aliousema wa mke wa Lutu. Na inasikitisha kuwa lipo kundi la wakristo (ambalo biblia inaliita pia wanawali wapumbavu (Mathayo 25)) watakao kosa unyakuo kwa tabia hizo za kutojali mambo ya muhimu ya wokovu. Na hao watabaki hapa kuingia katika ile dhiki kuu..Ndugu ni wakati wa kuchagua ni wapi unasimama leo?.

Tatu, waliambiwa habari zile asizifahamu mtu yoyote isipokuwa wana familia tu: Nataka nikuambie Jeriko ilipewa muda mrefu wa kutubu na kujisalimisha, miaka yote 40 Mungu aliyokuwa anawazungusha wana wa Israeli jangwani ulikuwa ni muda wa Taifa la Yeriko kutubu, na mataifa mengine yaliyokuwa Kaanani, walionyeshwa kwa vitendo jinsi Misri ilivyopigwa ndivyo watakavyokuja kupigwa na wao, lakini kama Taifa hawakutaka kusikia isipokuwa mtu mmoja tu aliyeitwa Rahabu, sasa siku wapepelezi walipokuja walimfunulia mipango yao na kumwambia asimwambie mtu yoyote isipokuwa wana familia tu!, Hii ni aina ya injili mpya ambayo alihubiriwa Rahabu yeye peke yake, na hiyo si injili ya kuambiwa atubu bali ni injili ya maagizo ya kujiokoa nafsi yako.

Halikadhalika, wakati huu ambao watu wengi wanaipuuzia injili itafika wakati Mungu ataanza kusema ni lile kundi tu ambalo limeshajiweka tayari..Hapa ndipo Mungu atakapoizidisha imani ya watu wake wawezi kunyakuliwa (watakuwa wanapewa maagizo fulani fulani)…Na ghafla tu ulimwengu utashangaa hao watu hawapo..kumbe siku nyingi tayari wapo mbinguni katika karamu ya mwanakondoo lakini wale waliosalia, ni dhiki na shida na ghadhabu ya Mungu inawahusu.

Na mwisho tunamwona Rahabu hakuwa mwanamke wa kiyahudi lakini aliingizwa kwa nguvu katika uzao wa kifalme wa Yesu Kristo Bwana wetu, mambo ambayo hata wayahudi wengi wa wazao ya Ibrahimu walikosa neema hiyo soma (Mathayo 1:5).

Vivyo hivyo na wewe leo hii ukiamua kutubu dhambi zako katika hizi siku chache zilizobakia kabla ya unyakuo, basi moja kwa moja utaingizwa katika mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, wa Yesu Kristo BWANA wetu. (1Petro 2:9). Usijiangalia kwasasa wewe ni mchafu kiasi gani, Rahabu alikuwa ni mchafu kuliko watu wengi wa Yeriko.

Ni rahisi tu kuingia katika huu ufalme! Tubu kwa kumaanisha kumwishia Bwana Yesu na kudhamiria kuacha dhambi, pili kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi katika jina la YESU KRISTO, na Mungu mwenyewe atakupa Roho wake atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote mpaka siku ya UNYAKUO.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine.Na Mungu atakubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

UNYAKUO.

SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!

KIKOMBE CHA GHADHABU YA MUNGU KINAJAA…TUBU UMGEUKIE MUNGU

 EPUKA MUHURI WA SHETANI


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments