UFUNUO: Mlango wa 10.

UFUNUO: Mlango wa 10.

Shalom…Karibu katika mwendelezo wa Kitabu cha Ufunuo..ambapo leo kwa Neema za Bwana tutaendelea na ile sura la 10..Kama hujapitia sura zilizotangulia, ni vizuri ungezipitia kwanza ili tuweze kwenda pamoja katika hizi sura zinazofuata.

Katika sura iliyopita tumeona malaika sita wakipita baragumu zao, na tuliona matukio yaliyoambatana na baragumu hizo, lakini katika sura hiyo hatukuona malaika wa saba akipiga baragumu lake, ikifunua kuwa kuna vitu Fulani vinapaswa viendelee kabla malaika wa mwisho kupiga baragumu…Na ndio tunaona katika sura hii ya 10, Yohana anakatishwa maono ya baragumu la mwisho la saba na kuonyweshwa ono lingine la Ajabu, ambalo ufunuo wake utatimia kabla ya baragumu la mwisho la saba kupigwa..Tusome.

Ufunuo 10: 1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto”.

Sasa huyu malaika si mwingine Zaidi ya Bwana Yesu Kristo, kumbuka Bwana Yesu sio malaika viumbe wa rohoni wanaotumika mbinguni, hapana! Bali ni “MALAIKA WA AGANO” au kwa lugha nyingine “MJUMBE WA AGANO” (Malaki 3:1 Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule MJUMBE WA AGANO mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.

…Kwa lugha ya kiingereza “ANGEL OF THE COVENANT or MESSENGER OF THE COVENANT”…Neno malaika ni neno la kigiriki lenye tafsiri ya MJUMBE…kwahiyo kuna aina mbili za wajumbe,1) Wajumbe wa kimbinguni ambao ndio malaika wa rohoni, 2) na pia wapo wajumbe wa kidunia, ambao hao ni wanadamu…Yohana Mbatizaji alikuwa ni Mjumbe wa Mungu wa kidunia, Gabrieli ni mjumbe wa Mungu wa kimbinguni…wote hawa ni Malaika, kwa kigiriki ‘Angelos’ kwa kiebrania ‘Malokh’ kwa Kiswahili ‘Malaika’. Kadhalika wale malaika saba wa makanisa saba ya Asia tuliowaona katika Ufunuo Mlango wa 2 na wa 3 wale ni wanadamu.

Hivyo katika Ono hili Yohana anaonyeshwa Malaika mwenye nguvu akitoka mbinguni, kirahisi Zaidi tunaweza kusema Yohana alimwona Mjumbe mwenye nguvu akitoka mbinguni…Sasa Mjumbe huyu si mwingine Zaidi ya BWANA YESU KRISTO, Akiwa katika mfumo wa ‘KIMALAIKA WA MBINGUNI’..Ni Yesu Kristo mwenyewe akijidhihirisha kama Malaika katika ono… lakini  utasema Bwana anaweza akajidhihirisha kama Malaika?…Jibu ni ndio! Anaweza…

Mwanzoni kabisa wa kitabu hichi tunamwona akijifunua kwa sifa kama za viumbe vya rohoni, malaika walizo nazo, utaona katika Ono Yohana alimwona ana macho kama miali ya moto…na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana. (Ufu.1:13-15), hakuna mwanadamu wa namna hiyo…Lakini alikuwa ni Bwana akijifunua kwa sifa za malaika..Na hapa hivyo hivyo ni Bwana Yesu yule yule akishuka kutoka Mbinguni kwa mfano wa Malaika…Uso wake uking’aa kama jua, na miguu yake kama nguzo ya moto…Uso wake kung’aa kama jua unadhihirisha utukufu wake… ukuu wake, kama vile jua linavyong’aa na kuangaza sana na kuwa Nuru ya Ulimwengu mzima..Kadhalika Kristo naye ni Nuru ya ulimwengu, maandiko yanasema hivyo katika Yohana 8:12..Na ni Kristo pekee ambaye uso wake unang’aa kama jua, hakuna mjumbe wowote wa duniani wala mbinguni ambaye uso wake unang’aa kama jua..Ndio maana utaona tena alijidhihirisha kwa namna hiyo mbele ya wanafunzi wake katika..

Mathayo 17: 1 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; 2 akageuka sura yake mbele yao; USO WAKE UKANG’AA KAMA JUA, mavazi yake yakawa meupe kama nuru”.

Na pia katika Ono alilooneshwa Yohana alimwona, akiwa amevikwa wingu kama vazi, wingu linaashiria utukufu wa Mungu, ndio maana tunasoma mahali Fulani kwamba Kristo atakuja na Mawingu, kama alivyoondoka na mawingu, na sisi tutamlaki mawinguni (Utukufuni). Na pia tunaona juu ya kichwa chake kulikuwa na upinde wa Mvua, Upinde wa Mvua unaashiria Agano la Mungu analofanya na wanadamu, Kwamba Kristo ni Bwana wa maagano, kama vile alivyoweka Agano lake na nchi kuwa hataiangamiza dunia tena kwa gharika ya maji, na mpaka leo hilo Neno lake hajalitangua, vivyo hivyo, maneno yake mengine yote yaliyosalia hawezi kuyatangua, yeye ni Mungu wa kushika maagano, ndio maana unaona juu ya kichwa kuna moja ya ishara ya Maagano yake aliyoyafanya juu ya nchi kuashiria kuwa mwenye mamlaka ya kuangia maagano amesimama naye ni mmoja tu Yesu kristo.

Tukiendelea na mstari wa pili biblia inasema..

Ufunuo 10:2 “Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi”

Katika mkono wake wa alikuwa na kitabu kilichofunguliwa..Kitabu hichi ni kitabu cha Ukombozi, ambacho ndio kile tulichokiona katika mlango wa 5 wa kitabu hichi cha Ufunuo..kitabu hichi ndio kimebeba siri zote za URITHI WA MWANADAMU, yaani mwongozo wote wa namna ya kuishi katika hii dunia milele kama Mungu alivyomkusudia mwanadamu aishi, na kilikuwa ndani na nje na kimefungwa na mihuri saba…Na kama tulivyosoma katika Ufunuo Mlango wa 5 hakuonekana mtu yoyote mbinguni au duniani aliyestahili kukifungua wala kukitazama kitabu hicho isipokuwa Mwana-Kondoo pekee tu peke yake, Na hivyo mwanakondoo ndiye akakipokea na akazivunja mihuri zake..Na hapa anaonekana akikishika kikiwa kimefunguliwa.

Ndugu, Siri zote za ukombozi zimuhusuzo mwanadamu, kuanzia kuumbwa kwake mpaka sasa, na urithi wote wa namna ya kuitawala hii dunia na siri zote, mpaka milele anazo sasa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye ndiye aliyeketi sasa katika Kiti cha Enzi, alipokuwa hapa duniani alikuwa hajapokea bado mamlaka,hivyo hata siku ya kurudi kwake ilikuwa haijafunuliwa ndio maana akasema…siku hiyo hakuna aijuaye isipokuwa Baba tu!..Lakini sasa ameshakipokea hicho kitabu cha Ukombozi, hivyo siri zote zikiwemo tarehe na muda, na saa ya kuuhukumu ulimwengu anazijua, hakuna kilichojificha tena kwake. Mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, na vizazi vyote na kila kitu kimewekwa Dhahiri mbele zake.

Na hapa anaonekana amekishika hicho kitabu kikiwa kimefunguliwa, hakina tena mihuri kwasababu mihuri yote imeshavunjwa, na akashuka na kuweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi.

Kwanini ameweka hivyo miguu yake mmoja habarini mwingine nchi kavu…Tutakuja kuona hapo mbeleni kidogo sababu ya yeye kufanya hivyo.

Tukiendelea na mstari unaofuata Yohana anaendelea kuona na kusikia mambo mapya..

Ufunuo 10: 3 “Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.

4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.”

Sasa tunaona pindi huyu Malaika aliposhuka tuu, alilia kwa sauti kuu…kama vile simba angurumaye…Naam Kristo ni Simba wa Yuda akinguruma, mbingu na nchi ni lazima zitetemeke…Yohana alimwona katika maono mengine mwanzoni kabisa wa kitabu hichi, akasema sauti yake ikiwa kama sauti ya maji mengi, lakini hapa anatoa sauti kama ya Simba. Na cha ajabu Zaidi, alipotoa hiyo sauti, ikaambatana na ngurumo..Ni kawaida mahali pakitokea sauti kubwa ni lazima hiyo sauti itikise vitu Fulani mahali Fulani ambavyo hivyo vitu kwa mtikisiko huo vitatoa sauti fulani…Hata ukiangalia spika kubwa zinazotumika kwenye mikutano..utaona zinapotoa yale mawimbi yake makubwa ya sauti, kuna kitu mfano wa kitambaa kigumu kimewekwa kwa mbele..na utaona na chenyewe sauti inapotoka kinakuwa kinatikisika na kama sio imara kinaweza hata kuchanika..kwaajili ya nguvu ya Sauti..Na pia utaweza kusikia mwangwi wake mahali Fulani kwa mbali…hata mara nne au tano…lakini ni sauti hiyo hiyo moja, imezaa nyingine nyingi…..Na ndivyo hapa, Sauti moja ya Kama mngurumo wa Simba imetengeneza ngurumo nyingine saba mahali Fulani.

Na Yohana aliposikia hizo sauti za Ngurumo saba…alikuwa tayari kuandika…kwasababu aliambiwa aandike kila alichokiona na kukisikia…Lakini alipokuwa katika kuandika sasa sauti ya hizi ngurumo saba, akasikia sauti ikimwambia “USIANDIKE! Hayo maneno uliyoyasikia yaliyonenwa na hizo ngurumo saba.”

Sasa hizi ngurumo saba ni sauti saba, ambazo zote zimeakisi kutoka kwenye ili sauti moja kuu ya KRISTO YESU..Ni kama mwangwi…Kwahiyo ni wazi kuwa zitakuwa zinazungumzia kitu kimoja…zitakuwa hazipingani…isipokuwa zitakuwa zinatofautiana kidogo sana katika kutoa ujumbe kwasababu hata mwangwi ulioakisiwa kwenye jiwe ni tofauti na uliokisiwa kwenye mwamba…ingawa maneno ni yale yale, isipokuwa yameakisiwa katika sehemu mbili tofauti..Na ngurumo saba zitakuwa ni sauti saba, zenye ujumbe unaokaribiana sana, usiopingana na mwingine…ambazo zitakuja kufunuliwa kipindi kifupi sana kabla ya unyakuo kufika. Katika hizo Bibi arusi atapata Imani ya kwenda kwenye unyakuo…Zitakuwa ni Siri Fulani baadhi ambazo zipo katika kile kitabu Bwana Yesu alichokishika katika mkono wake kilichofunguliwa…Na Siri hizo Bwana atazifunua kwenye Kanisa lake kupitia huduma 7/watu 7 ambao atawanyanyua kwa kipindi kimoja. Kumbuka mambo hayo hayajaandikwa kwenye biblia, yatakuwa ni mambo mapya kabisa, Kutakuwa na vitu vya kipekee kwa Bibi-arusi, na hiyo ndiyo itamletea Imani ya kwenda kwenye unyakuo…Kwa maelezo marefu kuhusu “ngurumo saba” bofya hapa⏩ NGURUMO SABA

Tukiendelea mbele Zaidi tunasoma..

Ufunuo 10:5 “Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,

6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; 

7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii”.

Sasa tukirudi pale, kwanini Mguu mmoja Bwana aliuweka juu ya nchi na mwingine juu ya Bahari…Ni kwasababu ya KIAPO kinachokwenda kufuata..

Katika hali za kawaida za desturi za kiulimwengu, watu wakienda mahakamani, wakitaka kutoa ushahidi au kuzungumza ukweli, sharti wasimame wima, hauwezi kuapa huku umekaa… na baada ya hapo, unanyoosha mkono wako mmoja wa kuume juu! Na kisha anaapa kusema ukweli…Kama ni kiongozi anaapishwa anakamata kile kitabu anachoapia na kukinyanyua juu na kuapa kupitia hicho.

Na hapa Bwana anakwenda kuapa! Na kuna vitu vitatu ambavyo wanadamu waliambiwa wasiape kabisa cha kwanza.1) MBINGU: kwasababu ndipo kiti cha Enzi cha Mungu kilipo 2) NCHI: kwasababu ndipo pa kuwekea miguu pa Mungu 3) KICHWA: kwasababu hatuwezi kuufanya unywele wetu kuwa mweupe au mweusi.

Mathayo 5:33 “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi”

Lakini huyu Malaika Mkuu unaona anakiuka vyote hivyo…Kwanini? ni KWASABABU Kilichopo Mbinguni ndio kiti chake cha Enzi, hakuna aliye zaidi yake…Na pia anaapa kwa nchi kwasababu ndipo ilipo Miguu yake…Ndio maana unaona mguu mmoja upo juu ya Bahari na mwingine juu ya nchi. Na vilevile kuonyesha kuwa anamiliki vyote vilivyo chini ya nchi kuzimu(ambapo ni baharini) na juu ya nchi (ambapo ni duniani). Kwahiyo ni uthibitisho tosha kuwa huyo si mwingine Zaidi Ya MKUU WA UZIMA MWENYEWE YESU KRISTO, MUNGU MKUU.Haleluya!!…Na hapa anaapa kwa kusema kuwa…

“hapatakuwa na wakati baada ya haya; 7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii”

Hapatakuwa na wakati baada ya haya…anamaanisha kuwa, Dunia haitaendelea kuwepo tena baada ya hayo..isipokuwa katika siku za malaika wa saba atakapokuwa tayari kupita baragumu. Sasa kumbuka mpaka kufikia hapa Malaika wa saba alikuwa bado hajapiga baragumu lake..baragumu sita zimeshapita…Tutakuja kuona baragumu ya saba itapolia ni nini kitatokea…lakini kwa ufupi Baragumu la saba linahusiana na siku ya BWANA yenyewe. Ambapo hakuna tena muda.Mambo yote yatakuwa yamekwisha hakuna tena nyakati wala vipindi vya wanadamu…Utakuwa ni wakati wa kuanza majira mapya…

Kwahiyo huyu Malaika Mkuu anaapa ikimaanisha ni “hakika na ndivyo itakavyokuwa” kuwa hakutakuwa tena na muda wa nyongeza…Isipokuwa katika siku za malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu…Katika siku za Malaika wa saba kupiga baragumu hizo ndio siku za mwisho..hakutakuwa na baragumu la nane wala muhuri wa 8.

Lakini ukiendelea mbele kidogo inasema “7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.”

Mwisho Malaika wa saba atakapopiga baragumu ndipo SIRI YA MUNGU itakapotimizwa. Ikiwa na maana kuwa hii siri ya Mungu bado haijatizizwa mpaka sasa…Maana yake bado yote haijafunuliwa…kuna sehemu haijatimizwa, na hiyo itatimizwa katika siku za Baragumu la malaika wa saba.. Sasa hapa biblia inasema ni SIRI itatimizwa…yaani ipo MOJA sio siri zitatimizwa kana kwamba zipo nyingi hapana.

Sasa hiyo SIRI ni IPI? Kwa ufupi SIRI HII ni YESU KRISTO..Yeye ndiye SIRI YA MUNGU

Wakolosai 1:26 “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;

 27 ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu”.

Sehemu ya kwanza ya siri hii ilifunuliwa ilifunuliwa kwetu sisi mataifa kwamba KRISTO YESU, yule Masihi aliyekuja hakuwa zawadi kwa wayahudi tu peke yao..bali hata kwetu sisi watu wa mataifa, kwasababu hiyo tukapata baraka kubwa sisi tuliokuwa hatustahili, hiyo ilikuwa ni SIRI iliyofichwa ndani ya YESU KRISTO, tunapokea uponyaji kwa Kupitia YESU Kristo, wafu wanafufuliwa, tunazungumza lugha mpya, tunawekea watu mikono wanapata afya nk. Tunahesabiwa kuwa uzao wa Ibrahimu. Mambo hayo ambayo zamani za agano la kale, yasingeingia akilini kwamba siku moja Masihi wanayemtarajia eti atawapa Uwezo wa kipekee namna hiyo watu wa mataifa, wasio hata wa uzao wa Ibrahimu kwahiyo hiyo ilikuwa ni siri na ilipokuja kufunuliwa iliwashangaza wengi sana.

Mtume Paulo aliiandika siri hiyo katika 

Waefeso 3:4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6 ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;

7 Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa.

Pia sehemu nyingine ya siri hiyo ambayo imefunuliwa kwetu ni kuwa YESU NDIO YEHOVA mwenyewe. Alipokuwepo duniani siri hiyo ilikuwa bado imefichwa miongoni wa wanadamu wote, wanamjua tu kama mwana wa Mungu mteule wa Mungu, lakini siku alipopaa na Roho Mtakatifu afumbuaye mafumbo aliposhuka juu ya mitume ndipo siri hiyo ikafichuka kumbe tulikuwa tunatembea na Mungu duniani pasipo sisi kujua. Mtume Paulo aliliweka wazi hilo na kusema..

1Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.”

Unaona?…Kadhalika ipo sehemu nyingine ya Siri hii hii ya huyu mmoja ambayo bado haijatimia, mwishoni kabisa mwa wakati wa baragumu la saba ndio itakuwa imemalizika yote..Somo linalohusu SIRI YA MUNGU ni pana kidogo..unaweza ukalipata  kwa kubofya hapa ⏩ Siri ya Mungu.

Tukizidi kuendelea mbele tunasoma…

Ufunuo 10:8 “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.

9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi”.

Baada ya Malaika huyu Mkuu kuapa kwa sauti kuu, Yohana anaisikia tena ile sauti iliyomwambia asiandike zile ngurumo saba, ikimwambia akakitwae kile kitabu mkononi mwa yule malaika na akile, nacho kitakuwa kitabu kama asali kinywani bali tumboni kitakuwa kichungu.

Hapa Yohana anaambiwa akitwae akile, kwa namna ya kawaida huwezi kula kitabu, kwahiyo hilo ni ono, na kitabu hicho hakuambiwa akisome, hapana bali akile…kusoma ni tofauti na kula, mtu asomaye anaingiza taarifa katika Akili yake…lakini mtu alaye anaingiza taarifa au uzima ndani ya mwili wake…Kwasababu kile alichokila kinaingia katika tumbo lake kisha kinameng’enywa na kuingia katika damu na mfumo wa mwili mzima…baadaye kile alichokila kinageuka sehemu ya yeye kinageuka na kuwa nyama yake, misuli yake, Ngozi yake n.k…

Na sisi Neno la Mungu hatujapewa kulisoma tu au kulikariri  hapana! bali tumepewa tulile katika roho, ndio Maana Bwana anasema yeye ni “chakula cha uzima” ili kitakapoingia katika miili yetu ya roho kiwe ni sehemu yetu!..
Sasa hapa Yohana anaambiwa atwae akile, mfano ule ule wa  Nabii Ezekieli alioambiwa atwae GOMBO lile na kulila…

Ezekieli 2:8 Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho. 9 Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.

10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

Ezekieli 3: 1 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

 2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.

 3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.

 4 Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.”

Nabii Ezekieli alipewa alile lile gombo kabla ya kwenda kusema na Wana wa Israeli, gombo tafsiri yake ni KITABU. Kwahiyo Bwana alimpa Neema ya ufunuo wa kipekee juu ya maneno yake ili atakapokwenda kusema na wana wa Israeli na kuwaonya! Azungumze kitu anachokielewa na kinachotoka ndani yake..Na baada ya hapo tunamwona Ezekieli akipata nguvu ya ajabu katika kwenda kuwapa unabii wana wa Israeli waliohamishwa, utaona alikuwa ananguvu nyingi kiasi cha kuweza hata kustahimili ishara Mungu alizokuwa anampa, wakati mwingine alikuwa anaambia alale ubavu mmoja kwa siku 430 na ubavu wa pili kwa siku 40, sehemu nyingina anaambiwa ale kinyesi ili kuwa ishara kwa wana wa Israeli,sehemu nyingine Mungu anamuua mke wake aliyempenda, halafu anaambiwa asiomboleze bali avae nguo nzuri, awe kama mtu ambaye hana msiba wowote n.k .mambo hayo yote aliweza kuyafanya baada ya kulishwa hilo gombo..vinginevyo kwa hali ya kawaida asingeweza.

Kadhalika na Yohana hapa anapewa kile kitabu akile. Sasa Katika siku za Mwisho kutakuja uamsho wa mwisho, ambapo Roho Atamwagwa tena kama siku ile ya Pentekoste na kama ilivyotokea kule Mtaa wa Azusa, Marekani…Bibiarusi atapokea nguvu ya kwenda kutoa unabii kwa mataifa, lugha na jamaa wa dunia nzima..nguvu ya Roho Mtakatifu itamwezesha bibiarusi kufanyika ishara kwa dunia nzima kipindi kifupi kabla ya unyakuo, lakini ijapokuwa wengi wataona ishara za namna hizo lakini hawataamini. Kwahiyo Yohana katika hilo ono anamwakilisha bibiarusi wa Kristo atakavyokuja kupokea ufunuo katika siku za mwisho…Ingawa pia baada ya Yohana kutoka Patmo, alizunguka sehemu nyingi kutoa unabii kutimiza sehemu hii ya maandiko..lakini ufunuo halisi utakuja kutimia katika siku za mwisho ..

Je! Umempa Bwana Maisha yako?..Unaona ni kwa jinsi gani tunaishi katika muda wa kumalizia, Kristo yupo mlangoni, na hata kama huamini atakuja, basi fahamu kuwa hujui siku yako ya kufa, inaweza ikawa ni leo..Sasa huko utakapokwenda utakuwa mgeni wa nani ?..hukukaa kikao na yeyote cha kuamua wewe kuja duniani kadhalika hutakaa kikao na yeyote cha  kuamua ni lini utaondoka! Hukuja na kitu utaondoka bila kitu! Hivyo jitafakari Maisha yako yatakapoishia..Na kama umempa Bwana Maisha yako kumbuka maandiko yanasema “pasipo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (Waebrania 12:14)je! Maisha yako yanastahili wokovu?.

Kama hujajiweka sana, na kujiandaa huu ndio muda wa kufanya hivyo haraka bila kuchelewa, tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kutokuzifanya tena, na kisha katafute ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kulingana na Matendo 2:38, na kisha Bwana atakuzawadia nguvu ya kushinda dhambi (Roho wake Mtakatifu). Na yeye ndiye atakayekutia MUHURI mpaka siku ya ukombozi wako Katika huyo utakuwa na uhakika wa kwenda mbinguni.

Usikose mwendelezo huu w asura zinazofuata.

Shalom! Maran atha! Kwa Mwendelezo >>>Ufunuo: Mlango wa 11

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312,jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana.

SIRI YA MUNGU

MJUE SANA YESU KRISTO.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments