MIJI YA MAKIMBILIO.

MIJI YA MAKIMBILIO.

Wana wa Israeli walipoingia katika nchi ya Ahadi, Na kuigawanya ile nchi, Makabila yote yalipewa Urithi wa ardhi isipokuwa kabila la Lawi, Wao waliganywa katikati ya makabila mengine yote 11 yaliyosalia..  Kati ya makabila hayo ilitengwa miji 48, sehemu tofauti tofauti kwa ajili ya Wana hawa wa Lawi.

Lakini kati ya miji hiyo 48, Ilitengwa miji 6 maalumu, ambayo iliitwa “miji ya makimbilio”…Miji hiyo haikuwa sehemu moja bali  ilikuwa imezagaa karibia  taifa zima. Miji hiyo ilitengwa mahususi kwa ajili ya wale watu ambao walifanya makosa ya uuaji yasiyokuwa ya makusudi, kwa wageni wa wenyeji..(Soma Hesabu 35:1-8)

Ikumbukwe kuwa katika torati ya Musa, ilikuwa ni kosa linalostahili kifo, ikiwa utamua mtu mwenzako, (Kutoka 21:14), hata moja ya zile amri 10 ilikataza tendo hilo.. Sasa mtu yeyote ambaye alipatikana na kosa la mauaji, ilikuwa ni lazima auawe kulingana na sheria au,auawe na mlipiza kisasi.

Lakini pamoja na hayo yapo makosa ambayo yalijulikana sio ya makusudi kwamfano, wakati mwingine labda wanakata magogo maporini na kwa bahati mbaya shoka likamponyoka mmojawao na kwenda kumpiga mtu mwingine ikampelekea mauti, sasa kosa kama hilo ni la bahati mbaya, kwasababu huyo hakukusudia kuua ni bahati mbaya tu (Soma Kumbukumbu 19:5)..Hivyo sheria inaweza isimuhukumu lakini “mlipiza kisasi” labda ndugu yake yule aliyeuliwa anaweza akalipiza kisasi kwa tendo hilo na isiwe ni dhambi. Sasa mtu kama huyu nusura yake ili apone..Ilikuwa ni sharti akimbilie kwenye mojawapo wa miji hiyo sita iliyotengwa.

Miji hiyo iliwekwa karibu na miji yote, kiasi kwamba mkimbizi, atatumia mwendo wa siku moja tu au chini ya hapo, kuufikia mmojawapo wa miji hiyo.. Vitabu vya kihistoria vya kiyahudi vinasema  njia za kuelekea miji hiyo zilikuwa ni pana, zilizochongwa vizuri, bila mabonde, au miinuko yoyote, ili kumsaidia mtu huyo afikie miji hiyo kwa haraka bila kipingamizi chochote, na pembeleni kunakuwa na kibao kimeandikwa ‘Miklat’ yaani “Makimbilio”

Sasa anapofika malangoni mwa miji hiyo, anakutana na wazee wa mji pale,(Ambao ni walawi). Anawaeleza tatizo lake, (kwamba ameua pasipo kukusudia), ndipo wale wazee wanampa hifadhi. Na wale washitaki wake watakapokuja na kuwaomba wazee  wamtoe wamuue wale wazee hawatawaruhusu..kulingana na torati.

Mtu huyo ataendelea kubaki huko mjini mpaka kuhani mkuu atakapokufa (kasome Yoshua 20:6) ndipo atakapokuwa huru kurudi katika nchi yake mwenyewe. Lakini akiondoka ndani ya mji ule kabla ya kuhani mkuu kufa, wale walipiza kisasi wakimwona wakamvizia na kumuua, wale watu waliomuua hawatashitakiwa kwa mauaji yale.(watakuwa hawana hatia kwa watakachokifanya)..Kwahiyo huyo mtu hataruhusiwa hata kwenda kuwasalimia ndugu zake nje ya mji, wala kwenda kununua chochote, wala kutalii..atabaki humohumo…mpaka kuhani mkuu atakapokufa ndio atakuwa huru kutoka.

Yoshua 20:1 “Kisha Bwana akanena na Yoshua, na kumwambia,

2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa;

3 ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu.

4 Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao.

Hivyo ndivyo watu waliofanya makosa ya uuaji usio wa makusudi walivyonusuka Israeli..

Je! Habari hiyo inafunua nini katika agano jipya?

Sisi tumepata neema iliyo kubwa zaidi ya hao, sio tu wanaofanya dhambi za bahati mbaya ndio wanaopata neema ya wokovu kama hao .Hapana, bali sasa hivi ni wote waliofanya dhambi..ziwe za bahati mbaya au makusudi, Mungu ametupa MJI WA KUKIMBILIA, nao ndio  huo “kuwa ndani ya KRISTO”..

Haijalishi umeua watu wengi kiasi gani kwa makusudi, umetoa mimba nyingi namna gani, umeloga watu wengi vipi, umezini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, umejibadilisha maumbile yako, umekuwa shoga, umekuwa msagaji, anaiba, unatapeli.. Mambo ambayo unajua kabisa unastahili ziwa la moto leo hii, unastahili kuuliwa na Mungu, unastahili hukumu wakati huu..

Lakini Bwana anakupa nafasi nyingine, ambayo itakuwa ni salama yako..Nayo ni msalabani.

Hakuna sehemu nyingine yoyote utakayoweza kuepuka hukumu isipokuwa kwa Yesu ndugu yangu. Hizo dhambi zako huwezi kuzificha ili usihukumiwe, kama leo hii hutayasalimisha maisha yako kwa Bwana Yesu.

Nje yake, ni HUKUMU tu  wala hakuna kingine..Ukifa leo katika hali uliyopo, fahamu kuwa hakuna msamaha milele, Vilevile ukiendelea kuishi katika maisha hayo ya dhambi fahamu kuwa ibilisi mshitaki wako anakuwinda usiku na mchana akuangamize.. Anakupangia mipango mingi kwasababu anajua unastahili hukumu kwa hizo dhambi zako nyingi..Hawezi kukuacha kukufuatilia maadamu anakuona bado upo nje ya Kristo. Biblia inasema shetani ni mshtaki…maana yake anafananishwa na huyo mlipiza kisasi Habari zake tulizozisoma hapo juu.

Kimbilia kwa YESU, ndiye Kuhani mkuu leo..

Vilevile na wewe ambaye upo tayari ndani ya wokovu, baki huko huko usifikirie hata kidogo kurudi kwenye ulimwengu..Kama vile tunaona wale ambao walitoroka kabla kuhani mkuu hajafa, walijiweka wenyewe hatarini kuuliwa na walipiza kisasi wao..Nawe pia usijaribu kufanya hivyo, dhambi ulizomfanyia Mungu huko nyuma zinatosha,.Usitoke nje ya mji wa Yesu wa makimbilio.

Na katika Habari hiyo makuhani wakuu walikuwa wanakufa ndipo mtu yule aliyeua bila kukusudia awe huru kurudi kwenye mji wake wa zamani…Lakini sasa hivi kuhani mkuu wetu YESU HAFI MILELE!!…Yupo…na maadamu yupo hai, hatupaswi kutoka nje ya uzio wake tusije tukafa.

Na kitu kingine cha kipekee ni kwamba….Ndani ya hiyo miji sita ya makimbilio…ilikuwa ni miji ya raha, haikuwa ni miji ya shida, kwasababu ilikuwa ni miji makuhani wa Bwana wanaishi..hivyo hakukukauka chakula, zaka zote na baraka zote wana wa Israeli walizokuwa wanamtolea Mungu, za mashambani na katika shughuli zao zote walikuwa wanazipeleka kwenye hii miji..Hivyo ilikuwa ni miji ya baraka, neema na rehema…aliyekimbilia kule aliishi Maisha yake yote bila shida!..kwani ni miji iliyobarikiwa, mtu huyo hawezi kamwe kupungukiwa na chochote kile iwe mavazi, chakula wala mahitaji mengine yoyote..lakini pia ilikuwa ni miji mitakatifu sio ya anasa, kwasababu ndio watumishi wa Mungu (makuhani wa Bwana) walikuwa wanakaa huko.

Kadhalika na leo ndani ya milki ya Yesu ambaye ndie Kuhani mkuu wetu, ni mji mtakatifu, wote wanaomkimbilia yeye wanakaa salama, wanatunzwa na kuhifadhiwa Maisha yao yote. Huoni hizo ni baraka za ajabu?

Ikiwa hujatubu na leo upo tayari kumkabidhi Kristo maisha yako kwa Bwana. Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

NA YEYE ALIYEKETI JUU YA WINGU AKAUTUPA MUNDU WAKE JUU YA NCHI, NCHI IKAVUNWA.

JE KUJIUA NI DHAMBI?

TUZIJARIBU HIZI ROHO.

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments