KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Kipindi kifupi kabla ya ghadhabu ya Mungu kumwagwa juu ya dunia, biblia imetabiri kuzuka kwa mambo ya ajabu sana na ya kutisha ulimwengu…na mambo hayo yapo mengi ikiwemo kuzuka kwa manabii wa uongo na makristo wa uongo, lakini pamoja na hayo yapo mengine matatu ya muhimu, ambayo ni …1) VITA 2) TAUNI na 3) NJAA.

Luka 21:10 “Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; 11 kutakuwa na MATETEMEKO MAKUBWA YA NCHI; NA NJAA NA TAUNI mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni”.

Kama tujuavyo mgonjwa kabla hajaanza kuumwa anakuwa anaanza kuonyesha dalili kwanza, labda ataanza kusikia kichefuchefu na baadaye akawa sawa, muda kidogo atasikia kichwa kinamuuma lakini si sana..na baadaye tena homa lakini si sana..kiasi kwamba anaweza akazivumilia dalili zile na kuendelea na shughuli zake kipindi cha mwanzoni..na wakati mwingine hata akajisikia nafuu kabisa kana kwamba haumwi tena….

Lakini siku ikifika yenyewe ambapo ugonjwa ule utanyanyuka..huo ndio wakati ambao kila siku kwake itakuwa ni afadhali na jana kuliko leo…zile dalili alizokuwa anazisikia mwanzo, kama kichwa kuumwa kidogo, homa kidogo, sasa vinazidi na kujizidisha na kuwa vikali mara nyingi zaidi..hapo atasikia kichwa kikiumwa hata mara kumi ya kile alichokuwa anakisikia hapo mwanzo..Homa inajizidisha mara nyingi kuliko mwanzo na mara nyingine anajikuta anaishia tu kalala kitandani. Mtu anapofikia hali ya kuumwa kiwango hiki huwa anatamani hata afe atokane na mateso hayo.

Sasa mambo hayo yanafananishwa na siku za maangamizi ya dunia zitakavyokuwa …Wengi wetu hatujui nini maana ya dalili ya siku za mwisho…Dalili maana yake ni mwanzo wa kitu…Hivyo biblia inavyosema kuwa dalili za siku za mwisho ni hizi au zile, inamaanisha kuwa mwisho wa siku mambo yatakuwa ni mabaya kuliko hata mwanzo.

Sasa Bwana Yesu alisema dalili mojawapo ya siku za mwisho ni kuwepo kwa matetemeko makubwa ya nchi(Luka 21:11)…maana yake ni kwamba siku yenyewe ya mwisho wa dunia ikifika kutakuwepo na tetemeko kubwa lisiloelezeka mara nyingi zaidi ya yale ya dalili..

Kadhalika Bwana Yesu alivyosema kwamba vita ni dalili mojawapo ya siku za mwisho, maana yake ni kwamba Siku yenyewe ya mwisho wa dunia ikifika kutakuwa na vita kubwa na kali na ya ajabu ambayo haijawahi kutokea, ambayo madhara yake hayajawahi kufananishwa na vita yoyote huko nyuma..na vita hiyo itakuwa si nyingine zaidi ya vita vya Har -magedoni.Kama hizi vita zilizopo sasa tumezoea kusikia watu elfu kadhaa wamekufa..vita hiyo ya mwisho ya Harmagedoni itamaliza mamilioni ya watu.

Pia alisema dalili nyingine ni NJAA, na njaa hiyo inasababishwa na kukosekana kwa mvua na kunyanyuka kwa wadudu wanaoharibu mazao kama nzige waliotokea wakati wa Farao, na waliopo sasa..Siku ya kuharibiwa dunia Itatokea Njaa ambayo haijawahi kuwa mfano wake…Baada ya watu kuifurahia chapa ya mnyama kwa kitambo..Mungu ataipiga dunia nzima kwa njaa..ambapo maji yote yatageuka kuwa damu na mifereji na mito..na mvua itaacha kunyesha(Ufunuo 16:4-6).

Kadhalika Bwana Yesu alisema dalili nyingine ya siku za mwisho ni KUZUKA KWA MAGONJWA MABAYA ambayo yanafanishwa na Tauni kibiblia(Luka 21:11)...magonjwa hayo yatakuwa hayana tiba na yanayoambukiza kwa kasi…Dalili za magonjwa hayo zimeanza kuonekana tangu mwanzo mwa karne ya 21, na mpaka kufikia sasa yameshaongezeka idadi..Kama ijulikanavyo kuna ugonjwa sasa unaoitwa Corona ulimwenguni.. Ugonjwa huu ni dalili tu (mwanzo wa utungu)..ambapo siku yenyewe ya mwisho ikifika ambayo inaweza kuwa hata leo..utazuka ugonjwa mpya ambao utakuwa ni mbaya kuliko huu uliopo sasa…utakuwa ni ugonjwa wa virusi mfano wa huu wa sasa…

Ugonjwa huu utashambulia ngozi na kusababisha majipu ya vidonda ambavyo vinaoza(Biblia inasema majipu yake yatakuwa ni mabovu, maana yake ni ya kuoza) na utakuwa unateseka kwa muda mrefu..Utakuwa ni tofauti na huu uliopo sasa ambao baada ya siku kadhaa mtu anaweza kupona…ugonjwa huo wa majipu utakuwa hauna tiba na wala hautakuwa unapona wenyewe, utampata kila mtu ambaye atakuwepo ulimwenguni wakati huo…

Ufunuo 16: 2 “Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake”.

Mambo haya sio hadithi bali ni mambo ambayo yatakuja kutokea dhahiri kabisa. Siku za ugonjwa huo jua litashushwa pia na kuwaunguza wanadamu wote wenye ugonjwa huo, duniani kutakuwa sio sehemu ya kuishi tena..kila mtu atakuwa kivyake akiugulia na kuteseka kivyake vyake kutakuwa hakuna hospitali itakayopokea wagonjwa kwasababu hata wauguzi wenyewe watakuwa na ugonjwa huo..(Hiyo itakuwa sio siku za dalili tena bali ya ugonjwa wenyewe, dalili ni wakati huu wa sasa).. Unyakuo upo karibu sana kutokea!..Kwasababu kabla ya siku hizo..watakatifu watanyakuliwa kwanza.

Ishara za magonjwa haya ni kutuonyesha kuwa Hukumu tayari imeshatamkwa juu ya ulimwengu..kama vile ambavyo ugonjwa unavyomwingia mtu..na hatua za kwanza ni dalili..na sasa tupo katika dalili ya ghadhabu ya Mungu. Hii hofu iliyopo sasa si hofu, hofu hasaa itakuja wakati huo wa mapigo hayo ya Mungu.

Ni nini kifanyike sasa? Katika hatua hii ya dalili?

Kinachopaswa kufanyika sasa ni kujiweka tayari tu…Tunajiwekaje tayari?..ni kwa kutubu, kujiosha mioyo yetu, kuacha dhambi na kuzidi kujitenga na ulimwengu kila siku… Kuacha kuziabudu sanamu na kuzisujudia , Kuacha ulevi, kuacha rushwa, kuacha wizi, kuacha matusi, kuacha kutazama picha za ngono, uasherati, kuacha kwenda ma disko, kuacha kuvaa nguo za kuonyesha maungo, na vimini na suruali kwa wanawake….mambo haya ndiyo yanayoisukuma ghadhabu ya Mungu imwagike haraka ulimwenguni na juu yako wewe..ni kama mgonjwa ambaye tayari kashaanza kuonyesha dalili, halafu bado hazingatii tiba..pasipo kujua kuwa ndio anazidi kujiharibu na kuuvuta ugonjwa zaidi..

Wakolosai 3: 5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; 6 kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”.

Umeona mstari wa 6, usemavyo?… “kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”..Soma tena..

Waefeso 5:5 “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.

6 Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi”.

Unaona tena? mstari wa mwisho huo wa 6.. “kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi”

Hiyo pekee ndiyo njia ya kujikinga na kujiepusha na ghadhabu ya Mungu…

Utauliza kutokana na tatizo hili lililopo sasa…je ! ni sahihi kunawa mikono na kutosalimiana na mtu kwa kushikana mikono njiani?

Kama tunavyoambiwa ni wajibu wa kila mtu kusimama pindi wimbo wa Taifa unapoimbwa…na wakristo pia wanatii agizo hilo..Hivyo na agizo la kunawa mikono popote tufikapo, tuingiapo na tutokapo wakristo tunatii bila shuruti kwasababu hakutupunguzii chochote katika Imani yetu…Tukijua ya kwamba mioyo yetu tayari imeoshwa kwa sabuni ya kimbinguni (Damu ya Yesu)..Na tumaini letu halipo katika maji na sabuni za mwilini bali katika maji na damu ya Yesu Kristo. Hiyo ndiyo inayotutakasa na kutulinda na kutuepusha na ghadhabu ya Mungu. Hivyo hatuna hofu, na hatuogopi kwasababu tunamtegemea Bwana, wakati ulimwengu unaogopa magonjwa, na njaa na vita sasa…sisi tunaigopa dhambi tu!..

Zaburi 125:1 “Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.

2 Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele”.

Lakini kama tukinawa mikono na mwili mzima mahali popote tuingiapo na tutokapo na huku mioyoni mwetu bado kuna uasherati, bado kuna wivu, hasira, wizi, ufisadi, ibada za sanamu, rushwa, na ulevi hakuna chochote tunachoweza kuepuka…Maji na sabuni na mlo kamili kamwe haviwezi kutuepusha na ghadhabu ya Mungu…Havijawahi katika agano la kale na hata katika agano jipya.

Hivyo kwa hitimisho kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, Hizi ni siku za mwisho..huhitaji kuhadithiwa na mtu tena..leo hii ile mipira uliyokuwa unajitumainisha nayo kuwa itakupatia faraja iko wapi? Kule kubet ulikokuwa unajitumainisha nako kuko wapi?…Zile visa na zile biashara zako ambazo ulikuwa unajitumainisha nazo unazifanya ulimwenguni kote ziko wapo leo?, elimu unayojitumainia iko wapi?, disko unayojitumainishia nayo iko wapi? Katika mataifa makubwa zimeshafungwa labda na kwako inaweza kuwa hivyo siku sio nyingi, wale waliokuwa wanakuambia kwamba dunia haitafikia mwisho wako wapi leo?..Uliwahi kufikiri kwamba ingetokea siku moja miji mikubwa mikubwa ingekosa watu barabarani?, mashule mengi ulimwenguni yangefungwa?,

umewahi kutafakari kwamba siku moja ingefika mamilioni ya watu hawataruhusiwa kwenda kazini wala makanisani?..Naam Hali inaweza kurudi kama kawaida na maisha yakarudi kama mwanzo na hata zaidi ya pale..lakini je! Umejifunza nini?…bado upo tu nje ya safina?

Huu ni mwanzo tu kwamba tutubu kwasababu siku yenyewe… ikifika hata hii Neema ya kutubu na ya kusikia mahubiri haitakuwepo?….Siku yenyewe ikifika itakuwa haiwezekani kabisa hata kwenda kanisani, licha ya kutafuta mtu wa kukuhubiria, hata kwa njia ya mitandao halitapatikana…wanaohusika na mitandao watakuwa matatizoni, vituo vya satellite vyote vitafungwa…Chapa ya mnyama itakuwa inafanya kazi na kipindi kifupi baada ya kuipokea chapa hiyo magonjwa hayo yataanza..

Yeremia 28:7 “Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote, 8 Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni”.

Kabla ya dunia kufikia maharibifu hayo..waliokuwa ndani ya Kristo watakuwa wamenyakuliwa je utakuwa miongoni mwao?..

Kama hujatubu..Na upo tayari kufanya hivyo leo hii, Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, . NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji Mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

UFUNUO: Mlango wa 16.

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.

Rudi Nyumbaani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments