ALIYOKUTANA NAYO YESU, YERIKO.

ALIYOKUTANA NAYO YESU, YERIKO.

Kuna watu wawili ambao tunaweza kujifunza leo katika ile safari ya Bwana Yesu kuelekea Yeriko, Biblia inatuambia kulikuwa na mkutano mkubwa wa watu waliokuwa wakimfuata, kumbuka wote hao kila mmoja alikuwa anatamani Yesu amuhudumie binafsi, walikuwa ni watu wenye matatizo mbalimbali, wengine matatizo ya familia zao, wengine biashara, wengine magonjwa, wengine walimfuata kwa lengo tu la kumwona Yesu n.k.

Sasa katikati ya umati mkubwa wote huo wa watu, waliokuwa wanataka kuhudumiwa, Bwana alikutana na watu wawili wa kipekee..

Mtu wa kwanza:

 Alikuwa ni Yule maskini kipofu..tusome habari yake:

Luka 18:35 “Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka;

36 na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?

37 Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.

38 Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.

39 Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.

40 Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza,

41 Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.

42 Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.

43 Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu”.

TAFAKARI: Huyu alikuwa ni kipofu, haoni, wala hakuwa na namna yoyote ile ya kumfikia Kristo ili ahudumiwe, lakini alikuwa wa kwanza kuhudumiwa na kumwona Kristo kwa karibu kuliko watu wote waliokuwa wanamfuata YESU tangu mbali, watu wenye macho, na wenye miguu, na wenye masikio, hata mmoja hakumteka YESU.

Mtu wa PILI:

Alikuwa ni Zakayo; Huyu alikuwa ni tajiri, lakini alifahamu utajiri wake usingemsaidia kumwona Yesu, licha tu ya kumkaribia..Na alipojaribu kupitia kutumia nguvu, walau kupiga vikumbo ili amwone tu Yesu, bado ilishindwa kutokana na ufupi wake.. Hivyo kwa namna ya kawaida kama kukata tamaa angepaswa awe ameshakataa tamaa siku nyingi..lakini turudie kusoma tena..

Luka 19:1 “Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake.

2 Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.

3 Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.

4 Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.

5 Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

6 Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha”.

Kama tunavyosoma, alikwenda mbele akapanda juu ya mkuyu. Na Yesu alipopita alikuwa wa kwanza kumwona, na kumwita,  akawashinda hata watu wengi ambao walikuwa warefu, wenye mbavu, wepesi..

Jambo gani tunaweza kujifunza:

Watu wengi tunafikiri madhaifu yetu ndio kikwazo cha sisi kutomkaribia Mungu, au kutokuwa watumishi wa Mungu..Tunaishia kusema, Ahh! Yule si ni kwasababu amezaliwa katika familia ya kikristo, au Yule si ni kwasababu anayo pesa ya kutosha kuendesha huduma, au Yule si ni kwasababu anayo miguu miwili ya kuhubiri injili..Au Yule si ni kwasababu ni kijana, au mtu mzima n.k.

Tunavisingizio vingi lakini hatujui, watu wanaonekana haiwezekani kumfikia Yesu kwa madhaifu yao,ndio wanaokuwa wa kwanza kufaidika na yeye, kama  hawatakata tamaa katika kumtafuta kwa bidii katika hali zao hizo hizo.

Utashangaa siku moja Bwana anamfanya kuwa mchungaji, au mwinjilisti, wa jamii kubwa ya watu ambao tangu zamani walikuwa wanajiita ni wakristo.. lakini yeye hakuwa hata na dalili za kuwa mkristo, katokea katika jamii wa waabudu miti, au wachawi.

Hivyo katika hali uliyonayo ambayo pengine inakufanya ujione ni kikwazo cha wewe kumfikia Mungu, hupaswi kuvunjika moyo endelea kupaza sauti kwa Bwana, panda kabisa juu ya mkuyu mtafute Bwana kwa bidii, usiwaangalie waliokutangulia katika imani, wewe fanya kwa nafasi yako. Utashangaa tu wakati utafika utakuwa wa kwanza kuhudumiwa na Kristo, zaidi ya hao unaodhani wanamjua Mungu tangu zamani.

Sasa mambo hayo hayawezekani kama hujaokoka. Hivyo kama upo nje ya Kristo, huu ndio wakati wako wa kumkaribisha mwokozi moyoni mwako, Hivyo tubu kwa kumaanisha dhambi zako, kisha ukabatizwe, kisha Bwana atakupa Roho Mtakatifu, na kuanzia huo wakati na kuendelea, Kristo ataelekeza macho yake kukutazama wewe kwanza.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

SADAKA YA MALIMBUKO.

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

KUMBUKUMBU LA DHAMBI.

KUMBUKUMBU LA DHAMBI.

Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema; Mafarisayo Hupanua HIRIZI zao, na kuongeza MATAMVUA yao?

MAOMBI YA VITA

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments