JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

Shalom.Karibu tujifunze Biblia..Neno la Mungu linasema katika 1Timotheo 6:20 “ Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo”.

Moja ya vitu vinavyobomoa Imani au vinavyomharibu mtu au vinavyoharibu huduma ni mashindano ya dini. Aina yoyote ya mashindano ya dini yanaasisiwa na shetani mwenyewe.

Na chanzo kikubwa cha mashindano ya dini ni Ujuzi wa mambo Fulani. Inapotokea mtu anafahamu kitu Fulani ambacho anahisi mwingine hajakifahamu au anahisi mwingine hafanyi kama inavyostahili….Mtu huyu Ule ujuzi unaweza kumletea kiburi na ni rahisi kuzaa majivuno na mwishowe mashindano..

Biblia inasema hivyo katika 1Wakorintho 8:1 “… Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga”.

Baadhi ya mashindano hayo ambayo yametengenezwa na shetani mwenyewe katika hizi siku za mwisho ni haya.

  • Mashindano kati ya uislamu na ukristo.
  • Mashindano ya Yesu ni Mungu au si Mungu
  • Mashindano ya kushindania siku ya kuabudu kama ni jumapili, au jumamosi
  • Mashindano ya kula nyama ya nguruwe n.k
  • Mashindano ya dhehebu la kweli la kuabudu.

Yapo mengi lakini hayo ndiyo yanayoshika nafasi za juu..Utakuta watu wanabishana tangu asubuhi mpaka jioni kila mmoja akitaka kumthibitishia mwenzake kwamba yupo sahihi na kwamba yeye anajua Zaidi.

Sasa kama ukichunguza mwisho wa mabishano hayo ni magombano au kutukanana au kudhihakiana au kuwekeana vinyongo au kupigana au Kuumizana au kuaibishana… Na mabishano hayo huwa hayaishagi..utaona yametulia tu kidogo baada ya masaa kadhaa au hata siku kadhaa yanaanza tena..kila mmoja kaenda kukusanya point zake mpya huko alikokwenda..na anarudi kwenye uwanja wa mapambano upya!..na mashindano yanaanza tena.

Kamwe hutaona katika hayo mazungumzo pamoja na point zao zote wanazozitoa na kukosoana..hutaona hata mtu akitubu, hutaona mtu akigeuka na kusema asante Bwana kwa kunifumbua macho!..hutaona mtu akitoka na moyo wa furaha na upendo na uchangamfu!.. Sasa ikiwa kama matunda ya Roho hayapatikani katikati ya hayo mazungumzo unategemea vipi yawe mazungumzo ya ki-Mungu?..Ni wazi kuwa ni mazungumzo ya kishetani…kwasababu mazungumzo ya kishetani ndiyo yanayozaa hasira, vinyongo, chuki, wivu, matusi, dhihaka, kuaibishana n.k

Biblia imetuonya sehemu kadha wa kadha juu ya mashindano ya dini..kwamba tuyaepuke..

2Timotheo 2:14 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao”.

Sasa swali linakuja… kama je! Unafahamu jambo ambalo unaamini ni sahihi na unataka kumshirikisha mtu asiyelijua na unapoanza tu kumshirikisha anaanza kushindana na wewe..katika hali hiyo unafanyaje?.

Jibu: Unapokutana na mtu ambaye unapomweleza ukweli hataki kusikia, jambo la kwanza yeye ni kupinga na kutaka kuleta mashindano..katika hali kama hiyo wewe unayemhubiria unahitaji kuwa na hekima..Hapo unapaswa ujishushe uwe mpole…Hakuna mtu asiyempenda mtu mpole au anayejishusha!..Unaanza kumweleza kwa upole na kwa utaratibu…Yule mtu akiona upole wako na utaratibu wako, akiona amekutupia tusi umenyamaza hujamrudishia..amekulaani umetulia kimya…hawezi kuendelea kukutukana wala kukupazia sauti, anapoona hakuna muitikio upande wa pili..hivyo atatulia na kukusikiliza..na moyoni atajua kuwa wewe hujaja kushindana naye bali umekuja kumfundisha..hivyo atakuheshimu, hata kama hatakubaliana na wewe katika baadhi ya points lakini hatashindana na wewe!…

Sasa taratibu ataanza kukusikiliza na Roho wa Mungu atamshuhudia ndani yake kwamba unayoyasema ni kweli…hata kama hatayakiri hapo mbele yako lakini baadaye atakapokwenda kutafakari atagundua kuwa ni kweli.

Lakini pale tu unapokutana naye na kuanza kujionyesha kwamba wewe unajua Zaidi yake, na anapotoa maneno ya kutukana unachokiamini na wewe unatukana anachokiamini, anapokurushia mshale na wewe unajibu mapigo kwa kutumia mistari..hapo tayari utakuwa umeshawasha moto wa mashindano na kamwe hamtafikia suluhu..ataishia kusema wewe ni mbishi na hujui lolote, hata kama unachozungumza kina ukweli kiasi gani.

1Petro 3:15 “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu”.

Mungu hawezi kamwe kuwepo mahali penye machafuko kama Neno lake linavyosema katika..1 Wakorintho 14: 33 “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu”. Hivyo katika kuhubiri au kushuhudia au kumshirikisha mtu jambo Fulani ni lazima pawepo na hali ya utulivu ndipo Roho Mtakatifu aweze kuwepo katikati yetu kutuhudumia.

Na Zaidi ya hayo, wapo watu ambao wamepandikizwa na shetani mwenyewe katika kumharibu mtu wa Mungu ambaye amesimama katika Imani ili aonekane ni mwovu..Na watu hao ni watu wa kuanzisha ubishi, ambao kazi yao kubwa ni kwenda kumchochea mtu aliyesimama abishane au agombane ili watu wengine wanaomzunguka wamwone kuwa si kitu, ni mtakatifu feki!..na waishie kutomsikiliza tena…Watu wa namna hiyo watakuja tu na kuanzisha mada na kukutaja wakitaka mchango wako..lakini lengo lao ukiwasoma si kutaka kujifunza bali kubishana na wewe…Watu kama hao wameanzisha mada na umejaribu kuwajibu kwa upole na hawaonyeshi kuelewa hao biblia imeturuhusu tuwakatae…Tusizungumze nao, wakituhoji ni ruksa kutowajibu….Wengi wa hao wametumwa na shetani kabisa kufanya hiyo kazi.

Tito 3:9 “Lakini maswali ya upuuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana”

Hivyo mijadala ya mashindano tujiepushe nayo, mijadala ya kushindania mistari ya biblia tujiepushe nayo na mijadala ya kila aina ambayo mwisho wake ni ugomvi na makelele tujiepushe nayo vilevile…

2Timotheo 2:23 “Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake”

Bwana atusaidie katika kulitimiza na hilo pia..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

UFUNUO: Mlango wa 1

DANIELI: Mlango wa 1

ESTA: Mlango wa 1 & 2

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments