Makao ambayo Yesu alikwenda kutuandalia ni yapi?

Makao ambayo Yesu alikwenda kutuandalia ni yapi?

SWALI: Yesu alimaanisha nini kusema ninakwenda kuwaandalia makao? Ni makao yapi hayo alikwenda kutuandalia.


JIBU: Tusome,

Yohana 14 :1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”.

Makao ni mahali ambao mtu ataweza kutulia na kuendesha aidha maisha yake au kufanya shughuli zake kama alivyokusudia yeye mwenyewe kwa utulivu.. Mtu asiyekuwa na makao yoyote, (yaani haishi kwenye nyumba, au kibanda) utagundua kuwa maisha yake ni ya kutanga tanga leo utamwona huku kesho kule, leo utamsikia yupo mji huu, kesho ule..hiyo yote ni kwasababu hana mahali pa kutulia. Anakuwa kama mgeni duniani.

Sasa ndivyo ilivyo pia katika roho, Mungu alipomuumba mwanadamu, alikuwa ni roho kamili, lakini sasa alipokusudia mwanadamu huyu aishi hapa duniani, alimuundia na makao yake maalumu (yaani Nyumba ya roho yake) ambayo ndio mwili,. Sasa mwili huo unamsaidia, aweze kuishi, kutulia, na kuipumzisha roho yake akiwa hapa duniani.

Na ndio maana mwili unaitwa nyumba ya roho. Lakini pia kuna roho nyingine ambazo zipo hapa duniani, ambazo hazikuumbiwa makao,(yaani miili), na roho hizo ni mapepo, ambayo Mungu aliyatupa dunia baada ya kuasi zamani sana miaka mingi kabla ya mwanadamu kuumbwa.

Sasa hizi roho kwasababu hazina miili ya kutulia, huwa zinazurura zurura hapa duniani bila kazi yoyote, hivyo zinachofanya ni kufanya bidii zote, kutafuta makao, na ndio hapo zinawaingia wanadamu ambao wapo nje ya wokovu. Zikishawaingia mule ndio zinapata pumziko. Lakini zikiwa nje, hakuna raha yoyote, na ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 12:43 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.

44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.

45 Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”.

Umeona hiyo ndio kazi yao..kwasababu hawana maskani (Nyumba /Miili), hivyo huwa wanafanya juu chini, wakimwingia mtu wasitoke na kwenda kuzurura zurura tu.

Kwahiyo, tunaweza kuona hapo, mwanadamu anazo maskani mbili Na zote hizo ni nguzo muhimu za kumsaidia kuishi hapa duniani.

Maskani ya kwanza ni mwili wake mwenyewe, ambao Mungu kamwekea roho yake ndani yake. Na maskani ya pili ni nyumba/kibanda, ambayo anaweza kutulia ndani yake na kuishi na kuendeleza maisha yake.

Vivyo hivyo na huko mbinguni.

Tutakapofika kule zipo maskani za aina mbili, maskani ya kwanza, itakuwa ni hiyo miili ya kimbinguni, na maskani ya pili, itakuwa ni makao, kama makao, miji na majumba ya sisi kuishi.

Sasa Bwana Yesu aliposema anakwenda kutuandalia makao, alimaanisha yote, makao ya roho zetu, na makao ya hiyo miiili tutakayoipokea huko mbinguni.

Kumbuka miili hiyo haitakuwa kama hii inayoona uharibifu, iliyotengenezwa kwa udongo, hapana bali miili hiyo imeundwa na Mungu mwenyewe, Isiyougua, isiyozeeka, isiyosikia njaa, isiyo sinzia, isiyochoka.. Bwana Yesu alirahisisha akasema tutafanana na malaika, Kama vile tunavyowaona malaika na sisi ndio tutakuwa hivyo.

2 Wakorintho 5 :1 “Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.

2 Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni;

3 ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi.

4 Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twaugua, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima:.

Umeona, hivyo, siku ile ya unyakuo, ndipo tutapokea miili hiyo mipya ya kimbinguni, lakini ni sharti kwanza turudishwe kwenye miili yetu hii ya udhaifu, kisha ivaliwe na ile mipya, ndio tuende mbinguni. unaweza kujiuliza ni kwanini Mungu afanye vile, anafanya hivyo ili kutimiza maandiko yake kuwa hata nywele za vichwa vyetu zimehesabiwa, hakuna hata kimoja kitakachopotea (Mathayo 10:30).

1Wakorintho 5:51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

53 Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda”.

Pengine leo hii unaoudhaifu Fulani katika mwili wako, lakini ukifika kule, hutauona huo udhaifu.  Hivyo tukaze mwendo tuyafikilie hayo tuliyoandaliwa. Na hiyo Yerusalemu mpya wa kimbinguni, ambayo itakushuka kutoka kwa Mungu mwenyewe. Miji mizuri yenye kuvutia na kupendeza. Mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

Hayo ndiyo makao ambayo Bwana Yesu alikwenda kutuandalia sisi kwa miaka 2000 sasa.

Bwana atutie nguvu.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Ukoma wa nyumba ulifunua nini zamani?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

Mafundisho

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments