JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

Marko 13:32  “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33  Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34  Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35  Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;

36  asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37  Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Nyumba ya Mungu inayozungumziwa hapo ni Kanisa lake, na kanisa sio jengo, bali ni mkusanyiko wa watu waliomwamini Kristo, (walioitwa kutoka katika ulimwengu wa dhambi, na kuingizwa katika neema ya kumjua yeye Wakolosai 1:13). Jengo ni mahali kanisa linapokutanika kumwabudu Mungu, kumshukuru, kumwimbia na kufarijiana, kuonyana pamoja na kukumbushana mambo ya msingi katika safari ya Imani.

Sasa katika mfano huo tunaona Bwana anaunganisha vitu viwili kwa pamoja; Anaunganisha shughuli za nyumba yake na ujio wake. Maana yake kuna vitu anategemea avikute vinaendelea kufanyika katika nyumba yake, na kila mtu ambaye ni amemwita na kumtoa katika ulimwengu wa dhambi,  kwa ufupi ni kwamba anataka akute kila mtu yupo kwenye shughuli yake fulani, aliyompangia aifanye..

Kama ndani ya nyumba ulipangiwa kazi yake kuhakikisha usafi wa nyumba pamoja na choo, anataka akija akukute upo bize katika shughuli yake hiyo, na choo akikute kisafi muda wote, kadhalika kama mtu kazi yake ilikuwa ni ulinzi anataka akija amkute yupo macho muda wote, anazunguka huku na huko kuhakikisha usalama wa nyumba n.k.

Na katika kanisa la Kristo kuna kazi, hatujaitwa tukae tu…Bali tuifanye kazi yake, kwa karama alizotupa… Na vipawa alivyotupa sio vya maonyesho, mlinzi wa getini hajakabidhiwa ile bunduki na zile sare ili ajisifu yeye ana silaha, au ni shujaa, au atembee na hiyo silaha mtaani na kujionyesha, kwamba ni nani kama yeye, na kwamba yeye ni zaidi ya wote, ana uwezo wa kuua wote kwa dakika moja. Hapana, bali alipewa silaha hiyo kwaajili ya ulinzi wa pale alipowekwa,Sio kwa sifa.

Na karama za rohoni zote hatujapewa kwaajili ya sifa zetu, bali kwaajili ya kazi ya nyumba ya Mungu, kama una karama ya kinabii, au kiinjilisti au nyingine yoyote hujapewa kwa lengo la kujisifu, bali ili uwatumikie wengine katika nyumba ya Mungu. Kama Mungu kakubariki sauti nzuri ya kumwimbia, hujapewa hiyo kwaajili ya sifa zako, wala Mungu hajakupa kwasababu anataka kukuinua kuliko wengine, bali amekupa ili kwa kuimba kwako watu watubu wamgeukie yeye, huku wewe mwenyewe ukiwa kielelezo. Hiyo ndio kazi uliyoitiwa uifanye.

Kwahiyo Kristo anataka akija akute kazi yake inafanyika ipasavyo, kila mtu katika eneo lake.

“Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe”.

Kwahiyo ni kama vile tupo katika jaribio, kila mtu anajaribiwa uaminifu wake kwa Mungu kulingana na kile Mungu alichokiweka ndani yake.

Na anasema anakuja haraka sana, na ujira wake (yaani mshahara wake) upo mkononi mwake..

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.

Kwahiyo huu sio wakati wa kuchezea karama au karama Mungu alizoziweka ndani yetu, ni wakati wa kuzifanyia kazi, kwasababu muda uliobaki ni mchache mpaka Kristo awasili, si wakati tena wa kulala, na kusema nitatubu kesho, nitamtumikia Mungu kesho, ni wakati wa kusema kila kitu kinachohusiana na ufalme wa mbinguni naanza kukifanya leo.

Na kama hujaokoka, huwezi kumtumikia Mungu..utafanyaje kazi katika kampuni ambalo hujaajiriwa??..Hivyo unapoamua kuokoka (yaani kumkabidhi Yesu maisha yako) unasajiliwa katika ufalme wa mbinguni, na hivyo Roho Mtakatifu anakupangia kazi kama anavyotaka yeye na si kama unavyotaka wewe au mtu mwingine yeyote. Kwahiyo kama hujampokea Yesu tubu leo kwa dhati huku ukiziacha kwa vitendo dhambi zote ulizokuwa unazifanya hapo awali. Kama utahitaji msaada zaidi katika hatua hii ya kumpokea Yesu, unaweza kutujuza inbox, au mtafute mtu yeyote aliye mtumishi wa Mungu karibu na wewe atakusaidia.

Na pia kama umeshaokoka, lakini unashindwa kuelewa karama/au huduma Mungu anayotaka umtumikie kwa hiyo, wasiliana na sisi tutakupa mwongozo wa jinsi ya kujua Neema ya Mungu iliyo juu yako.

Mwisho, kumbuka Bwana Yesu alisema katika Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake KILA SIKU, anifuate.”.

Kwahiyo katika kumfuata Yesu ni lazima tujikane kila siku, na si siku moja tu wala mara moja tu.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Bawabu ni nani/nini?

UJIO WA BWANA YESU.

TAWI LIZAALO HULISAFISHA ILI LIZIDI KUZAA.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments