JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.


Contact

Paulo katika kazi yake ya utume, hakuwa tu na jukumu la kuwahubiriwa watu Kristo  ili wamwamini, kisha wapokee ondoleo la dhambi halafu basi..Hapana, bali pia ni mtu ambaye alikuwa anatia bidii nyingi sana katika kuwajuza watu juu ya ukweli wote wa Mungu na siri nyingine zilizojificha katika maandiko tangu zamani.

Na ndio maana utaona alisema..

Waefeso 5:17 “KWA SABABU HIYO MSIWE WAJINGA, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana”.

Paulo alipiga vita ujinga ambao watu wanao kuhusu Mungu, kwasababu alijua ni jinsi gani unavyoweza kumgharimu mkristo kwa sehemu kubwa. Ujinga ni ile hali ya mtu kukosa maarifa ambayo kama angeyapata basi yangemsaidia kuishi au kutenda mambo fulani kwa ufanisi mahali alipo.. Kwamfano, mtu ukikosa kufahamu kuwa duniani kuna kitu kinachoitwa teknolojia, na kwamba ukitaka kuwasiliana na mtu aliye mbali utatumia kifaa kinachoitwa simu,

Sasa wewe hataki kusikia habari za simu, badala yake unataka tu kukaa maporini , kuwinda swala, kuna wakati utafika utahitaji kuwasiliana na ndugu zako wa mbali, hapo ndipo itakugharimu utumie  miguu yako au punda kwenda kuwafuata na hiyo pengine itakuchukua mwezi mzima kwenda na kurudi, kiasi kwamba kama angepata maarifa ya simu, au vyombo vya moto basi kuwasiliana kwako au kusafiri kwako kungekuwa ni kurahisi sana na kwa haraka.

Vivyo hivyo na katika Ukristo, tunakosa maarifa mengi sana, na hiyo inapelekea pengine tunashindwa kuufurahia wokovu wetu , au kuona safari  hii ni ngumu sana, au kushindwa kabisa kustahimili mengi.  Siku zote Hatuwezi kumtumikia Mungu, juu ya kiwango cha ufunuo tulichonacho kuhusu yeye. Kiwango chako cha kumwelewa Mungu ndicho kitakachoeleza maisha ya wokovu unayoishi sasa.

Sasa Mtume Paulo ni mtu ambaye alikuwa anatamani kupata maarifa ya kutosha kuhusu ufalme wa mbinguni, na ndio maana siri nyingi zihusuzo kanisa, na Mungu tunazipata katika nyaraka zake.Na ndio maana sehemu nyingi utaona anasema Neno hili SITAKI MKOSE KUFAHAMU. Akiwa na maana hataki tuwe wajinga..

Embu tuangalie baadhi ya vitu ambavyo alitaka sisi tusikose kufahamu.

  1. Tumaini la ufufuo wa wafu:

Anasema..

1Wathesalonike 4:13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini”.

Ukiendelea kusoma pale utaona anaeleza jinsi siku ya unyakuo itakavyokuwa, kwamba utatangulia kwanza ufufuo wa wafu, hivyo wewe kama ni mkristo, ukiifahamu siri hiyo kwamba lipo tumaini la kufufuliwa na kuonana wa wapendwa wetu katika Imani waliotutoka, hatutakuwa na huzuni ya kupitiliza, kama watu wa kidunia walivyo, hatutakuwa wa kulalamika, na kulaumu laumu muda wote.

2) Kuhusu hukumu watakayokabidhiwa watakatifu.

1Wakorintho 6:2 “Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?”

Watakatifu watakaoshinda hawatahukumu tu ulimwengu, bali mpaka na malaika, Je ulishawahi kulifikiria hilo wewe utawahukumuje malaika? Fikiria tena hilo, uone ni  mambo makubwa kiasi gani Mungu amewaandalia watu wake huko mbeleni.

3) Siri ya Yesu iliyojificha katika agano la Kale.

1Wakorintho 10:1 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

3 wote wakala chakula kile kile cha roho;

4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.

Paulo anatufunulia siri nyingine kuwa hatupaswi kusoma agano la kale kama historia Fulani tu, tunapaswa tujue ndani ya historia zile Kristo amejificha, na Hivyo tunapaswa tusomapo tumwone Kristo, kwasababu vyote vile vilimfunua yeye. Hivyo Paulo anatuasa tusiwe wajinga pia katika hilo, tusome mawazo yetu tukiyaelekeza kwa Kristo.

4) Kuhubiri injili kuna dhiki.

2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi”.

Wengi tunadhani katika kumtumikia Mungu ni mteremeko tu wakati wote, hapana, Bwana Yesu kiongozi wetu alipitia dhiki, mitume pia walipitia dhiki wakati mwingine, vivyo hivyo na wewe, unapaswa ulielewe hilo, ili kusudi kwamba litakapotokea, usije ukawa mjinga kwa kuacha kuifanya kazi ya Mungu, ukasema huyu ni shetani, kwani Mungu sikuzote haruhusu watu wake wapitie dhiki.

5) Miili yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu.

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Anataka tufahamu kuwa hii miili tuliyopewa na dhamana, ni mali ya mwingine sio yetu, hivyo tuithamini kwasababu tukiiharibu kwa uzinzi, au pombe, au michoro, au chochote kile, tutaharibiwa na sisi. Hilo tusiwe wajinga, wengi wameuliwa na Mungu kwa njia hiyo.

6) Utumishi wa Madhabahuni.

1Wakorintho 9:13 “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?”

Paulo hataki watu wawe  wajinga pia kufahamu, watumishi wa Mungu wana haki ya kula vya madhabahuni, kwasababu ndivyo Mungu alivyoagiza na wala sio mwanadamu. Hivyo sio jambo la kujadiliana nalo au kushangaa utakapokutana nalo.

7) Karama za Rohoni.

1 Wakorintho 12:1 “Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu”.

Hapa yapo makundi mawili ya wakristo, lipo kundi ambalo haliamini kabisa, au haliruhusu karama za Mungu kutenda kazi katika kanisa la Kristo, wakisikia kuna mtu anakarama ya kuona maono wanasema ni shetani, wakiona kuna mtu ananena kwa lugha wanasema huyo sio Roho. Hivyo utakuta kanisa limebakiwa kuongozwa na wenyeviti na makatibu, na maaskofu- jina, na makasisi, basi, hakuna chochote cha Zaidi ya litrujia kufuatwa.

Kundi lingine,  ni lile lisiloweza kumbanua karama za Roho, huduma za Roho, Utendaji kazi na Ujazo/Ubatizo  wa Roho Mtakatifu. Haya yote Mtume Paulo alitaka tusiwe wajinga, matokeo yake ni kuwa leo hii utakutana na watu wengi wenye karama huku wakiendelea na maisha yao ya kale wakidhani kuwa wana Roho Mtakatifu kumbe walishaachwa zamani, japokuwa karama zao zinaendelea kufanya kazi.

8) Mpango wa Mungu kwa mataifa.

Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili”.

Hii ni siri kubwa ambayo  tukiijua  hatutaishi maisha ya patapotea kwenye ukristo wetu, siku tukifahamu kuwa Utimilifu wa mataifa utawasili, na kwamba kuanzia huo wakati na kuendelea sisi hatutakuwa na neema tena ya kuupokea wokovu, bali itarudishwa tena Israeli kwa kipindi kifupi, ndipo tutakapoishi maisha ya umakini sana katika Ukristo wetu.

Wengi wetu tunadhani, tutaendelea tu hivi hivi mpaka Yesu atakaporudi, Ndugu, Wokovu utaishia kwa wayahudi sio sisi. Kwahiyo tukiwa wajinga tukidhani kuwa tutaendelea hivi hivi, tujue tupo katika hatari kubwa sana ya kuuokosa, Unyakuo. Bwana Yesu kuna wakati atasimama, na kuufunga mlango. Wakati huo utakuwa ni hapa hapa duniani, na sio mbinguni. Kwasababu Utimilifu wa mataifa utakuwa umewasili. Mungu atakuwa ameshamalizana na sisi, utakuwa ni wakati wa wayahudi tena.

Embu jiulize, Je, ikiwa neema hiyo inarudishwa kule Israeli, utampatia wapi tena Kristo, na wakati Roho Mtakatifu hayupo tena juu yako. Ikiwa leo hii, unamkataa unampinga, angali neema ipo, unadhani nafasi hiyo itakuwepo tena? Hivyo usiichezee hii neema ambayo ndio tunakaribia kumaliza nayo. Dalili zote zinaonyesha kuwa hatuna muda mrefu Unyakuo utapita. Wafu watafufuliwa, na sisi tutaungana nao kwenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni.

Hivyo tubu dhambi zako mgeukie Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

UTAWALA WA MIAKA 1000.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
2 years ago

Barikiwa sana mwalimu nimekuelewa.

Fadhili Edward
Fadhili Edward
2 years ago

YESU atukuzwe, Nimebarikiwa sana

Anonymous
Anonymous
3 years ago

Leave your message