BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.

by Admin | 25 May 2022 08:46 am05

Kuna majira yakupasa uisikie sauti ya Mungu, kuliko hasara utakayoingia, ili kuiponya nafsi yako.

Kuna mfalme mmoja wa Yuda anaitwa Amazia, Huyu mfalme siku moja alijikuta anaingia katika vita na maadui zake (Waedomi), Hivyo alichokifanya ni kupanga vikosi vya wanajeshi yake, ili kwenda kushindana nao. Lakini bado aliona majeshi yake hayatoshi, hivyo akaenda kwa ndugu zake, waliokuwa upande wa Israeli, ili awaajiri wanajeshi wao kwa fedha nyingi sana..

Hivyo akawaajiri wanajeshi takribani Laki moja (100,000).

Lakini tunaona alipokuwa anakaribia kwenda vitani, nabii wa Mungu alimfuata, akamwambia, achana na hao askari uliowaajiri, kwasababu mimi sipo nao..Nenda mwenyewe na jeshi lako vitani.

Likawa ni jambo gumu kwake, kwasababu tayari anapunguza nguvu, na kama hiyo haitoshi, tayari alishalipa fedha nyingi sana kwa ajili ya majeshi hayo..Amewekeza fedha zake nyingi katika vita na haziwezi kurudishwa.

Lakini kwasababu Amazia alikuwa anamcha Mungu, alitii sauti ya Mungu, akawa tayari kuipokea hasara, hiyo. Akaenda vitani na jeshi lake dhaifu, na Bwana akamsaidia kushinda, tena kwa ushindi mnono.

2Nyakati 25:6 “Akaajiri pia watu mashujaa mia elfu wa Israeli kwa talanta mia za fedha.

7 Lakini mtu wa Mungu akamjia, akasema, Ee mfalme, usiwaache jeshi la Israeli waende nawe; kwa kuwa Bwana hayupo pamoja na Israeli, yaani, wana wote wa Efraimu.

8 Lakini ukitaka kwenda, haya, jitie nguvu upigane; Mungu atakuangusha mbele ya adui; maana MUNGU ANAZO NGUVU ZA KUSAIDIA, NA KUANGUSHA.

9 Amazia akamwambia mtu wa Mungu, Lakini tuzifanyieje zile talanta mia nilizowapa jeshi la Israeli? MTU WA MUNGU AKAJIBU, BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO”.

Ni mara ngapi, watu wengi wanashindwa kumfuata Yesu, kisa hasara watakazoingia kwa uamuzi huo?

Niliwahi kuzungumza na mtu mmoja, anasema anampenda Mungu kweli, lakini anamiliki bar tena sio moja bali kadha wa kadha, na anasema ndipo anapopatia rizki. Nikamwambia hana budi kuacha biashara hiyo, kwasababu Mungu anaouwezo wa kumpa kitu kingine bora kuliko hicho, ikiwa tu atamtii Kristo. Lakini jambo hilo likawa bado ni gumu kwake kulipokea, akaendelea na biashara yake.

Mwingine pia tulimshuhudia akawa yupo  tayari kuokoka, lakini madai yake ni kuwa hana kazi, anatumia njia ya kujiuza ili apate pesa za kulipa kodi, na bili za maji na umeme.. Anasema kabisa nikiokoa najua hii kazi nitaacha, na sitakuwa na chanzo chochote cha mapato, nitaishije mjini?

Ndugu ikiwa na wewe ni mmojawapo wa watu wanaoshindwa kuacha kazi za ibilisi, kisa tu, umewekeza pesa nyingi katika hizo, au unahofia utakuwa maskini, au ukifanya kazi nyingine utapata kipato kidogo.. Nataka ukumbuke hilo andiko hapo juu kuwa “Bwana anazo nguvu za kusaidia, na kuangusha”.. Na “tena, Anaweza kukupa Zaidi sana kuliko hizo”

Anaweza kukupa mara dufu ya hivyo. Na hata kama hatokupa basi anaweza kukufanya uishi kwa raha na amani kuliko hata hapo ulipokuwepo. Bwana Yesu anasema,..Itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima, kisha upate hasara ya nafsi yako?. Amazia, alikubali kuingia hasara akijua kabisa Mungu kweli atampa Zaidi ya vyote alivyovipoteza.

Ni heri ukampa Yesu Maisha yako ayaokoe, kipindi hichi cha kumalizia, watu wengi wamenaswa kwenye vitanzi hivi…Wakiangalia mitaji yao yote imelalia kwenye michezo ya kamari, imelalia kwenye madawa ya kulevya, imelalia kwenye biashara za pombe na sigara, imelalia kwenye mavazi ya kikahaba na kidunia.

Achana nayo, mwamini Mungu anayekuita. Utakuwa salama, na atakusaidi kumudu Maisha yako..

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Kwanini wakristo wengi ni maskini?

ORODHA YA WAFALME WA ISRAELI.

JAWABU LA MAISHA YA MTU.

APENDAYE FEDHA HASHIBI FEDHA.

NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)

Kuvyaza ni nini katika biblia? (Ayubu 21:10).

ENZI NA MAMLAKA AMEZIFANYA KUWA MKOGO

Uru wa Ukaldayo ni nini?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/05/25/bwana-aweza-kukupa-zaidi-sana-kuliko-hizo/