ENZI NA MAMLAKA AMEZIFANYA KUWA MKOGO

ENZI NA MAMLAKA AMEZIFANYA KUWA MKOGO

Jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Wakolosai 2:14 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;

15 AKIISHA KUZIVUA ENZI NA MAMLAKA, NA KUZIFANYA KUWA MKOGO KWA UJASIRI, akizishangilia katika msalaba huo”.

Je unajua maana ya Mkogo? (mkogo ni nini?)

Mkogo ni neno lenye maana ya “tamasha”.. kwamfano watu wanaofanya tamasha la sarakasi, ni sawa na kusema wanafanya “mkogo wa sarakasi”

Hivyo hapo maandiko yaliposema “Bwana Yesu amezivua enzi na Mamlaka na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri”..Maana yake “amezivua enzi na mamlaka na kuzifanya kuwa tamasha kwa ujasiri”.

Sasa swali, ni Enzi gani na Mamlaka gani, Bwana Yesu aliyavua?.. ni yake mwenyewe au mengine?

Jibu: Enzi na mamlaka yaliyovuliwa hapo na Bwana sio yake yeye mwenyewe.. bali ni yale ya NGUVU ZA GIZA. Bwana amemvua shetani juu ya huu ulimwengu na wanadamu kwa kifo chake pale msalabani.. Na baada ya kumvua, akayavaa yeye mamlaka hayo.. (kumbuka mamlaka hayo ya shetani alimvua Adamu, pale Edeni).

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI”.

Huu ulimwengu sasahivi upo chini ya mamlaka ya Bwana Yesu, shetani ni kama mpangaji tu!..nyakati na majira yatakapotimia ataondolewa moja kwa moja. Hivyo shetani sasahivi si kitu kwa Bwana Yesu..

Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, WALA HANA KITU KWANGU”.

Sasa ni wakati gani ambapo Enzi na mamlaka yalifanyika mkogo (yaani tamasha)?

Ni wakati Bwana Yesu akiwa msalabani, wakati dunia inaona ni kifo cha aibu, lakini Bwana yeye aliona ushindi, wakati wachache wanamhuzunikia na kumlilia pale msalabani.. yeye (Bwana) alikuwa anashangilia ushindi, na kuonyesha tamasha la wazi kwa ujasiri, jinsi shetani na majeshi yake yalivyokuwa yanavuliwa mamlaka pale msalabani.

Wakolosai 2:15 “akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.

Bwana leo hii anatawala mbinguni na duniani, shetani hana lolote mbele zake.

Je kwanini tusimtumainie leo huyo?.. Kwanini tusimfanye kuwa nguzo ya Maisha yetu?..yeye ambaye amemvua shetani mamlaka na enzi. Hata sasa tunapozungumza Bwana Yesu anamiliki vitu vyote vya mbinguni na duniani, na vilivyopo chini ya dunia, na vitu vyote vinapiga goti, na vitapiga goti mbele zake.

Tukimwelewa Yesu kwa namna hii, kamwe hatutamtamani shetani na Fahari zake, na pia hatutamwogopa shetani, wala hatutawaogopa wachawi.. Ukiona unahofu ya shetani, au wachawi na umesema umeokoka au umempokea Yesu, basi jua bado hujamjua Bwana Yesu vizuri.

Siku ukimjua na kumwelewa, hutabaki kama ulivyo.

Mpokee Yesu, mtumainie Bwana.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

TUMEKUWA TAMASHA KWA DUNIA; KWA MALAIKA NA WANADAMU.

ZUMARIDI NI MADINI GANI?

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

NI NANI ALIYEKUPA MAMLAKA HII UYATENDE HAYA?

Hapo ndipo, atakapompa Mungu Baba ufalme wake.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
2 years ago

Amina Amina mwalimu,kwa kweli mbali kujifunza kupitia masomo haya pia yananifanya nisikie raha.Mbarikiwe sana.