Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Kuna njia kuu sita(6)

Ni vema ukazifahamu hizi njia Mungu anazozungumza na watu, ili usitegemee tu njia moja uifahamuyo wewe, matokeo yake ukakosa shabaha ya kuzisikia sauti za Mungu kila siku maishani mwako zinapozungumza na wewe.

1. Ya kwanza ni Njia ya moja kwa moja:

Hii ni Aidha kwa Sauti, ndoto, au maono,

Ni mojawapo ya njia ambayo Mungu anazungumza na watu. Na ndio inayojulikana na kutegemewa na wengi.

Ayubu 33:14-15

[14]Kwa kuwa Mungu hunena mara moja,  Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. [15]Katika ndoto, katika maono ya usiku,  Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;

Katika maisha yetu kwa namna moja au nyingine Mungu alishazungumza nasi kwa njia hii. Unaweza usione, maono au usisikie sauti lakini kila mtu huwa anaota. Na kwa njia hiyo Mungu huzungumza.

  1. Kwa njia ya Neno lake:

Hii ndio sauti ya Mungu namba moja ambayo inazungumza na mtu moja kwa moja na kwa wakati wote..ni sauti ambayo hailinganishwi na sauti nyingine zozote.

Ukiwa ni msomaji mzuri wa Neno, utamsikia Mungu katika nyanja zote za Maisha akikufariji, akikuonya, akikushauri, akikuongoza n.k. Ni pakeji iliyojitosheleza., ambayo hailinganishwi na njia nyingine yoyote.

2Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;”

    3. Njia nyingine ni Amani.

Ikiwa wewe umeokoka, na umejazwa Roho Mtakatifu, basi ujue mara nyingi sana Mungu atatumia amani yake moyoni mwako kuamua mambo mengi..

Na ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 10:11-13

[11]Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka. [12]Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.

[13]Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

Wakolosai 3:15a “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;..”

Kuonyesha kuwa amani itokayo kwa Roho ni sauti ya Mungu kutuongoza, ikiwa umepoteza amani ghafla katika mazingira fulani kuwa makini sana hapo. Wakati mwingine ni Mungu anazungumza.

   4. Kwa kupitia watu.

Hapa anaweza akachagua aidha apitie mtu mwovu au mtu mwema. Mara nyingi sana Mungu anazungumza na watu kupitia watumishi wake, yaani wahubiri, waalimu, wainjilisti n.k.

Yeremia 25:4

[4]Naye BWANA ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize.

Na mara nyingine tena anaweza kutumia watu wa kidunia kukuonya..kama vile maaskari, wakuu wa hii dunia n.k.

Hivyo ni kuzingatia sana unachokisikia au kufundishwa au kuonywa na watu, hususani watumishi wa Mungu..Mara nyingine sauti ya Mungu ipo nyuma yao.

     5. Kwa kupitia mazingira.

Mazingira yanaweza yakawa ya kimaisha, au ya kihali…kwa mfano Mungu akitaka uelewe jambo fulani, wakati mwingine hatumii sauti ya moja kwa moja, kwasababu pengine unaweza kulichukulia juu juu tu au usimwelewe, hivyo atakupitisha katika maisha fulani au mazingira fulani, na kwa kupitia hayo utajua kabisa hapo ni Mungu alikuwa akisema na wewe.

Mfano wa watu kama hawa alikuwa ni Nebukadreza, yeye alionywa na Mungu, awe mnyenyekevu na amche Mungu, lakini hakusikia, kinyume chake akapuuzia ule unabii aliopewa na Danieli. Matokeo yake baada ya miezi 12, akageuzwa kuwa kama mnyama, akawa anaishi huko misituni akila majani kama ng’ombe..mpaka siku alipoelewa somo kuwa aliye juu ndiye anayetawala falme zote za duniani. Ndipo akajinyenyekeza ,hivyo Mungu akamrudishia ufalme wote wa dunia. (Danieli 4)

   6. Kwa kupitia vitu vya asili na viumbe.

Sauti ya Mungu imejificha sana katika vitu vinavyotuzunguka na asili, kiasi kwamba tungefahamu vema basi tusingekuwa na ugumu wa kumwelewa Mungu.

Embu fikiri Bwana Yesu alivyotuambia..tafakarini Kunguru?..hawapandi hawavuni wala hawana maghala ya chakula lakini wanakula..Je sisi si mara nyingi zaidi ya hao? (Luka 12:24)

Hili ni neno ambalo lilikwepo tangu enzi na enzi kiasi kwamba watu wangekuwa wanalitafakari kabla hata ya Yesu, wasingekuwa na hofu ya maisha pale wanapotaka msaada kutoka kwa Mungu.

Vivyo hivyo utazamapo, bahari, milima, miti,  zipo sauti nyingi sana za Mungu nyuma yake .. Chukua muda mwingi kutafakari, utaisikia sauti ya Mungu waziwazi.

Mungu alimwambia Ibrahimu angalia juu tazama nyota za mbinguni na mchanga wa baharini upate imani kwangu.

Hivyo ni vizuri ukapata maarifa haya usije ukaangamia kwa kutomwelewa Mungu. Leo hii watu wanategemea njia moja tu..ile ya moja kwa moja..yaani kusikia sauti, au kuona maono au kuota ndoto. Na kusahau hizi nyingine.. Ndio hapo utasikia wakisema nimeomba sana, nimelia sana Mungu aseme na nini, lakini sijawahi kumsikia.

Ni kwanini? Nikwasababu wanalazimishia njia hiyo hiyo moja Mungu aseme nao..

Hawajui kuwa Mungu hapangiwi fomula ya kuzungumza.Hivyo wewe uombapo..kuwa mtulivu, soma sana Neno mtafakari Mungu..subiri azungumze kwa jinsi apendavyo yeye. Atakujibu tu aidha kwa Neno lake, au mtumishi wake, au amani moyoni mwako, au kwa kutazama mambo ya asili, ukiona hivyo basi ujue ni Mungu huyo.

Hivyo kaa katika utulivu wa Roho, zingatia kusoma Neno..kwasababu maarifa kama haya utayapata katika biblia na sio kwa kuota au kuona maono.

Yohana 8:32 “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI.

MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?

Unyenyekevu ni nini?

ALITOKA HUKO, AKAENDA MAHALI KARIBU NA JANGWA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amina