SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Habari za Esau na Yakobo zina mafunzo makubwa sana kwetu,. Unajua biblia inaposema mambo yote yaliyoandikwa katika agano la kale yalikuwa ni kwa ajili ya kutuonya sisi, ilimaanisha kweli (Soma 1Wakor 10:11). Hivyo tunapaswa tusome kwa umakini mkubwa sana kwasababu  hakuna jambo ambalo linaendelea sasa hivi duniani halijaandikwa kwenye biblia.

Ulishawahi kujiuliza ni kipindi cha siku ngapi, au wiki ngapi, au miaka mingapi kilipita, tangu ule wakati  Esau anauza haki yake  ya mzaliwa wa kwanza kwa mdogo wake, mpaka ule wakati Baba yao anawabariki. Unaweza kudhani ni kipindi kifupi sana wakiwa bado ni watoto, lakini sio.

Ni kweli wakati Esau anauza haki yake, walikuwa bado ni vijana wadogo, kulingana na hadithi za wayahudi, siku ile Esau alipomfuata ndugu yake ni kumuuzia haki yake kwa chakula cha dengu alipokuwa ana njaa inasadikika walikuwa na umri wa miaka 15.

 Lakini wakati ambao Baba yao sasa anakaribia kufa, walikuwa si watoto tena, bali watu wazima sana, Kulingana na hadithi hizo hizo za kiyahudi walikuwa ni wazee wa miaka 63, kwasababu wakati tu Esau anaoa wake wahiti alikuwa na umri 40, (Mwanzo 26:34)  na hapo bado sana baba yao kuwabariki kwahiyo zaidi ya miaka 48, Yakobo alikuwa anaipigania tu ile haki ya mzaliwa wa kwanza.

Lakini nataka leo tuone kwa undani ni kwanini, Mungu alimchukia Esau, kwa ile tabia yake kama tunavyoma katika maandiko.

Warumi 9:13 “Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia”.

 Wengi tunadhani ni kwa kosa la kule tu kile chakula alichopewa na ndugu yake baada ya kutegewa mtego wakati alipokuwa na njaa.. Ukweli ni kwamba Mungu asingeweza kuchukizwa na Esau kirahisi hivyo, kwa kosa la njaa, bali alichukizwa na Esau kwa ile kauli yake aliyoitoa ambayo aliendelea kuisimamia katika maisha yake yote..

Na kauli yenyewe ndio ile tunayoisoma katika biblia..(Zingatia vifungu vilivyo katika herufi kubwa)

Mwanzo 25:29 “Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana.

30 Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.

31 Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza.

32 Esau akasema, TAZAMA, MIMI NI KARIBU KUFA, ITANIFAA NINI HAKI HII YA UZAZI?

33 Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

34 Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. HIVYO ESAU AKAIDHARAU HAKI YAKE YA MZALIWA WA KWANZA”.

Sasa zingatia hiyo  kauli ya Esau..”mimi ni karibu na kufa, itanifaa nini hii haki ya uzazi”.. Ni heri angesema, “Haya nitakupa” Lakini yeye alisema ninakaribia kufa, itanifaidia nini hiyo haki za uzazi, akiwa na maana hiyo haki kama haiwezi kumtatulia matatizo yake aliyokuwa anapitia kwa wakati ule, haina maana yoyote, ni ya kudharauliwa tu,

Na ndio maana ukindelea kusoma utaona biblia inasema.. tangu huo wakati Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza,..Unaona bado aliendelea kushikilia msimamo wake huo huo, kwa miaka zaidi ya 40, mpaka siku ile ya kubarikiwa  na baba yao ilipofika, alipogundua umuhimu wa  Baraka hizo alikuwa ameshachelewa, japo alitafuta kila namna ya kumpendeza baba yake lakini jambo hilo halikufanikiwa hata kidogo, biblia inatuambia, alilia kwa machozi mengi yasiyoelezeka. Soma

Waebrania 12:16 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja.

17 Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi”.

Ndugu, hii roho ya Esau mpaka leo inafanya kazi sana, tena sana , nimekutana na watu wengi, unapowahubiria injili, ambayo ni kwa faida yao wenyewe, jambo la kwanza watakalokuuliza, nikiokoka, Yesu atanipa pesa za kumudu maisha yangu leo?, ukimwambia zitakuja kwa wakati wake, atasema, Basi simtaki hana faida kwangu, mwingine utampa kipeperushi chenye habari za wokovu,atatazama halafu kidogo, halafu saa hiyo hiyo atakuambia nilidhani unanipa pesa, wewe unanipa makaratasi, anakitupa hapo hapo mbele yako,.. Sasa watu kama hawa hawana tofuati na Esau, ambaye alikuwa anaidharau  haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwasababu haikuweza kumtatulia matatizo yake ya wakati ule.

Ndugu usiutafute wokovu wa kutatuliwa shida zako za sasa, kamwe usifanya hivyo, Mungu atakuona wewe ni kama Esau tu. Vilevile kama na wewe ni mmojawapo, wa wanaoidharau injili, ipo siku utautafuta wokovu kwa machozi mengi na kulia na kusaga meno na hautaupata.. Siku hiyo utakapoona, wenzako hawapo tena duniani wameshanyakuliwa wameenda  mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo, wanashangalia, kwa furaha isiyo na kifani, na wewe upo hapa duniani, huna lolote nakuambia siku hiyo utalia sana..Leo unacheka lakini hiyo siku  utalia sana,.

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Mpaka sasa hakuna asiyejua kuwa unyakuo upo karibuni kutokea, tumebakiwa na siku chache sana pengine wiki, au miezi, lakini tujue kizazi chetu kimekidhi vigezo vyote vya kushuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Yesu duniani. Swali ni je! Wewe umejiwekaje tayari leo? Je! Ni kama Yakobo ambaye usiku na mchana alikuwa anautafuta urithi usioharibika kwa hali na mali, au kama Esau aliyedharau Baraka za mbali kwa mafanikio, na pesa za muda tu.

Jibu unalo.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

UFUNUO: Mlango wa 15

kwanini Yakobo amefananishwa na mdudu?(Isa 42:14)

Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas mhula
Lucas mhula
1 year ago

Nimebarikiwa sana na somo Mungu wa Mbinguni akuinue zaidi Mchungaji kwa somo hili.