JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio mwanga wa njia zetu na taa ya miguu yetu. Zab 119:105..Leo tutajifunza kwa ufupi sana juu ya kulipa Zaka, Kimaandiko Zaka ni fungu la 10, yaani sehemu ya 10 ya mapato ya mtu anayatoa kwa Mungu. Kwahiyo zaka ni mojawapo ya aina ya sadaka.

Kabla hatujaenda kujifunza kuhusu umuhimu wa kulipa zaka, kama ina ulazima au la! Hebu tujifunze kidogo historia ya ZAKA.

Zaka kwa mara ya Kwanza ilianza kutolewa na mtu anayeitwa Ibrahimu, ambaye anajulikana kama Baba wa Imani.

Tunasoma hayo katika kitabu cha Mwanzo 14

Mwanzo 14:17 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme.

18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.

19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.

20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. ABRAMU AKAMPA FUNGU LA KUMI LA VITU VYOTE”.

Ibrahimu alimpa fungu la 10 huyu Melkizedeki, huyu Melkizedeki alikuwa ni Mungu aliyekuja katika Mwili wa kibinadamu… na pia anajulikana kama Kuhani Mkuu, mfano wa Mwana wa Mungu (Yesu Kristo) hana baba, wala mama, wala hana mwanzo wa siku wala mwisho wake. Kwahiyo alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyekuja katika mwili wa kibinadamu.

Sasa wakati Abramu ametoka kumwokoa ndugu yake Lutu ambaye alikuwa ametekwa yeye pamoja na wanawe, njiani wakati anarudi akakutana na Huyu Melkizedeki, na huyu Melkizedeki alikuwa amebeba Divai na Mkate, akampatia Abramu na kwasababu Abramu alimpenda sana Mungu, hakuona vyema kupokea bure bila kutoa chochote…zaidi ya yote Mungu amemwonekania na kumfanikisha katikati ya maadui zake na kuwashinda! Hivyo ndani yake kuna kitu cha kipekee kikamgusa akaona si vyema kutomrudishia chochote Mungu wake, hivyo akaamua mwenyewe pasipo kuambiwa na mtu yeyote kumtolea Mungu wake sehemu ya 10 ya vitu vyake!!! O huo ni moyo wa namna gani? Kumbuka hakuambiwa hata na Mungu afanye vile, ni yeye mwenyewe tu kuna kitu ndani yake kilimfanya ajisikie vibaya endapo angemwona Mungu wake anaondoka mikono mitupu, na hicho si kingine zaidi ya Roho Mtakatifu.

Je! Sheria ilifanya kazi?

Sasa wakati huo kulikuwa hakuna sheria yoyote, wala amri 10 na Mungu hakuingia Agano na Ibrahimu kuhusu zaka, Miaka kama 400 hivi baadaye ndipo wana wa Israeli, walikuja kupewa sheria na Mungu! Na miongoni mwa hizo sheria ilikuwa ni pamoja na kulipa zaka!, ilikuwa ni lazima kulipa zaka, mtu asipolipa zaka ilikuwa inahesabika kwake kuwa ni dhambi!, na mbele za Mungu ni kama mwizi (Malaki 3:8-9).

Lakini sasa hatuishi kwa sheria bali kwa Imani, na Imani tunayoizungumzia ni Imani ile ile ya kwanza kama ya Ibrahimu, yaani Imani ya kufanya mambo bila ya kusukumwa sukumwa, na Imani hiyo ndio kama hiyo ya Ibrahimu, ya kumtolea Mungu fungu la 10 pasipo masharti!..Ibrahimu alitoa pasipo masharti, wala sheria, wala torati kwasababu Torati hata bado ilikuwa haijaja, wala kulazimishwa, wala kusukumwa wala kuombwa, wala kumwuliza Mungu, wala kuhubiriwa na mtu yeyote bali alitoa kwa Imani na kwa moyo, akitafakari kwamba vyote vimetoka kwa Mungu, na Mungu ndiye mpaji wangu (Yehova-YIRE), hivyo kama yeye amenipa sehemu kubwa ya vitu hivi, basi mimi nitamrudishia walau sehemu ya 10 ya vitu alivyonipa. Na akajiwekea hiyo kuwa ndio sheria yake daima! Kila sehemu ya 10 anayopata anamrudishia Mungu.

Ndugu, Ibrahimu alikutana na Melkizedeki, na hata sasa huyu Melkizedeki yupo naye si mwingine bali ni Bwana wetu Yesu Kristo, maandiko yanalithibitisha hilo katika…

Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki”.

Waebrania 7:1 “Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;

2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;

3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.

4 Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara”.

Waebrania 5:5 “Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

6 kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele Kwa mfano wa Melkizedeki”.

Umeona Kristo amefananishwa na Melkizedeki, na kama Melkizedeki alipewa sehemu ya 10 na Ibrahimu, kadhalika Kristo naye anastahili sehemu ya 10, kwasababu yeye ndiye Melkizedeki wa Agano letu, na kama Melkizedekia alivyompigania Ibrahimu ndivyo Kristo anavyotupigania sisi sasa hivi,

Na kama Ibrahimu alimpa Melkizedeki fungu la 10 pasipo masharti, wala pasipo torati, wala pasipo sheria yoyote, wala pasipo kuhubiriwa na mtu, wala pasipo kushauriwa na mtu, wala pasipo kusukumwa na mtu yeyote ndivyo hivyo hivyo leo hii tunapaswa tumtolee YESU KRISTO fungu la 10 pasipo sheria yoyote, wala pasipo masharti yoyote, wala pasipo mahubiri yoyote, wala pasipo kusukumwa na mtu..Linapaswa liwe ni jambo linalotoka moyoni kwamba tunatambua uwepo wa Yesu Kristo katika maisha yetu na hivyo tunamheshimu kwa kumtolea fungu la 10, yeye hana shida na fedha! Lakini anaitazama mioyo yetu!. Na Bwana Yesu mwenyewe aliruhusu hilo katika (Mathayo 23:23).

Ukiona mtu anapinga kulipa ZAKA!(Na huku ameshaujua ukweli) Na anapinga kumtolea Mungu, Huo ni uthibitisho kuwa hana ROHO MTAKATIFU ndani yake! Ni moja ya uthibitisho wa mtu aliyekosa Roho Mtakatifu ndani yake!..Kwasababu ni wazi kuwa hampendi Mungu, kwasababu hawezi kumshukuru kwa kutoa hata sehemu ya 10 ya mali zake na kumrudishia yeye, ingawa anavuta pumzi bure, anakanyaga ardhi ambayo sio yake bure, anakula chakula ambacho hajui kimetengenezwaje tengenezwaje! Hathamini hata Kristo aliyeotoa uhai kwa ajili yake bure..Kwa ufupi ni mtu asiye na shukrani.

Na mtu wa namna hiyo atawezaye kumshukuru Mungu kwa kutoa sehemu ya 10 ya maisha yake kuhubiri Injili?, atawezaje kutoa kutoa hata uhai wake kwaajili ya Injili?, au atawezaje kuifia Imani? Kama tu sehemu ya 10 ya fedha yake hawezi kuitoa?. Huyo Mtu atawezaje hata kuacha vyote na kumfuata Kristo kama tu sehemu ya 10 kutoa ni vita?..Atawezaje kumtolea Mungu katika vyote alivyonavyo kama Yule mwanamke aliyetoa senti mbili na Bwana akamsifia? Tafakari tu!

Hivyo ZAKA sio kitu cha kukwepa kabisa! Hakitolewi kwa sheria wala kwa torati, wala kwa imeandikwa wapi kwenye biblia, bali kwa moyo kama vile Ibrahimu!..Kama huna kazi yoyote inayokupatia kipato hapo upo huru!, lakini chochote unachokipata tofauti na kazi kitolee sehemu ya 10 katika hicho na kumrudishia Mungu, huna kazi lakini umepewa zawadi kiasi Fulani cha fedha kitolee sehemu ya 10, na utoe kwa moyo pasipo kulazimishwa, kwasababu Mungu sio mkusanyaji mapato! Anataka tumtolee kwa Moyo na kwa furaha, huku tukielewa umuhimu wa kumtolea yeye kama Ibrahimu alivyofanya.

Sasa swali ni je! Usipotoa Zaka utakwenda kuzimu?

Kitakachompeleka mtu kuzimu sio kitendo cha kukiuka kulipa zaka au kuzini, au kuiba, au kutukana hapana kitakachompeleka mtu kuzimu ni kutokuwa na Roho Mtakatifu ndani yake, ambapo sasa matokeo ya kutokuwa na Roho Mtakatifu ndio hayo sasa atakuwa mwizi, mwasherati, mtukanaji, atakuwa ni mtu asiyekuwa na Moyo wa Utoaji kabisa, likija suala la utoaji ni vita, anakuwa hawezi kuwasaidia wengine, na pia hawezi kuchangia chochote katika ufalme wa mbinguni katika utoaji wake, pia anakuwa mtu asiyesamehe Kwasababu Mtu aliye na Roho Mtakatifu hawezi kufanya mojawapo ya hayo mambo kwasababu Roho Mtakatifu atakuwa anaugua ndani yake kuhusu dhambi na atakuwa anaugua pia kuhusu ni kwanini hamtolei Mungu, hivyo hawezi kukwepa kulipa zaka kama vile asivyoweza kukwepa kuwasaidia wengine au kusali.

Upo usemi unaosema kwamba, mimi ni mkamilifu katika kila kitu! Isipokuwa ni zaka tu ndio sitoi!

Ndugu huo ni uongo wa shetani! haiwezekani mtu akawa mkamilifu katika mambo yote halafu akakosa tu kitu kimoja kwamba halipi zaka! Hakuna kitu kama hicho! Kama mtu halipi zaka kwa makusudi, na kashaujua ukweli, basi ni lazima atakuwa pia ni mwovu katika mambo mengine, ni sawa na kusema huyu mtu ni mtakatifu katika kila kitu lakini kasoro tu ni mwasherati! Huo ni uongo…

Dhambi moja inashirikiana na nyingine, aliye mwasherati ni lazima atakuwa na tamaa, kinyongo, mwongo na msaliti, mwenye wivu, mshindanaji hata kama kwa nje hatakuwa haonekani lakini moyoni mwake hivyo vyote anavyo. Kwahiyo kukwepa kulipa zaka ni uthibitisho wa kukosa Roho, na wote wasio na Roho wa Mungu biblia imesema hao sio wake (soma Warumi 8:9), na kama sio wake maana yake watakwenda kuzimu!.

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

Rudi Nyumbani:

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments