TUUTAZAME PIA MWISHO WA UJENZI WETU.

TUUTAZAME PIA MWISHO WA UJENZI WETU.

Kumbukumbu 22:8 “Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko”.


Bwana Yesu alisema, mtu yeyote anayeyasikia maneno yangu na kuyatenda anafananishwa na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba…(Mathayo 7:24), Hii ikiwa na maana kuwa kumbe Maisha ya kila mtu aliyeokoka ni sawa na nyumba inayoijenga yeye mwenyewe,..Hivyo kila mtu anapaswa awe makini anapoijenga nyumba yake sio tu pale anapoujenga msingi wake bali pia mpaka pale anapomalizia…

Kwamfano tutaona hapa Bwana Yesu alikuwa anasisitiza juu ya msingi, ambao ndio mwanzo wa ujenzi wa maisha ya mtu, kwamba ukitaka nyumba yako(Maisha yako) yasiwe kazi bure basi zingatia ni ardhi gani unayoijengea nyumba yako, kama ni mwamba (ambao ndio maneno ya Yesu Kristo yenyewe) basi fahamu kuwa msingi wako nyumba yako utakuwa salama na nyumba yako itasimama imara milele lakini kama ni nje ya Kristo basi ujue Maisha yako unayoyaishi sasa hivi ni kazi bure kwasababu yatafikia mwisho yatakoma na utakuwa umepata hasara kubwa..

Lakini Sio tu kufanikiwa kuijenga nyumba yako juu ya mwamba imara, unapaswa pia uzingatie umaliziaji wa nyumba yako ili iwe katika ujenzi bora na salama..Kama tunavyosoma hapo juu enzi za agano la kale Mungu alitoa amri kwa waisraeli wote, pindi tu wanapomaliza kujenga nyumba zao, hawapasi kuzifunika tu kwa sakafu au matofali na kuziacha hivyo hivyo bila uzio wowote kama ujenzi mwingi unavyofanyika sikuhizi wa kuweka mabati, hapana bali Mungu aliwapa maagizo wahakikishe kuwa wanaweka ukuta kando-kando ya dari zao, ulionyanyuka, kusudi kwamba ikitokea mtu amepanda kule, na akateleza bahati mbaya, basi ule ukuta ulio kando kando ya dari umzuie asianguke mpaka chini, tofauti na ujenzi mwingi wa sasa hivi ulivyo, mtu akiteleza kwenye bati basi moja kwa moja ni mpaka chini, na pengine kumsababishia majeraha ya kudumu au mauti kabisa. Angalau baadhi ya magorofa marefu yana uzio huo kule juu kabsia, ingawa si yote.

Hivyo nyumba zote, na majengo yote ya kiyahudi ndivyo yalivyojengwa enzi zile. Na kama mtu asipofanya hivyo na ikatokea mtu akaanguka darini kwake, basi damu ya huyo mtu, Mungu ataitaka juu ya huyo mwenye nyumba.

JE! UJENZI HUO WA KUWEKA UKUTA KANDO-KANDO YA DARI UNAFUNUA NINI KATIKA AGANO JIPYA?

Kama tulivyoona mkristo kweli anaweza akawa ameanza vizuri katika ujenzi wake, ameokoka, amemwamini Yesu Kristo, amepokea uzima wa milele, lakini hazingatii kuchukua tahadhari katika nyumba yake anayoijenga, haweki kuta, hajiwekei mipaka ya njia zake, hajui kuwa wapo watu wanamwangalia, wapo watu wanayatambelea Maisha yake kila siku, wanapanda mpaka juu ya dari lake, mahali ambao anadhania watu hawawezi kufika,Sasa kwa kutolijua hilo wale watu wanapofika, na kukutana na kikwazo kidogo tu, pengine wanamwona ni mvaaji wa vimini, unatembea nusu uchi barabarani halafu unasema umeokoka, ni rahisi wao kuanguka, na kusema kama wokovu ndio huu, ni heri niendelee kuwa kahaba milele…Hajui kuwa ameshamkosesha yule mtu na damu yake itatakwa juu yake.

Unakwenda disko, unatukana , na bado unasema umeokoka, unacheza kamari, una-bet na huku bado unasema umeokoka, wale watu wanaokutazama, wakiona mapungufu kama hayo, umewasababishia wao kuanguka mara mbili Zaidi. Ni heri ungesema sijaokoka wasingekuwa na la kujikwaa, na hiyo yote ni kwasababu hujiwekei kuta za kuilinda nyumba isiwe ya lawana.

Unasikiliza miziki ya kidunia, muda huo huo unamwimbia Mungu, wale watu wanaokuzunguka watakuonaje? Watasema kuna wokovu kweli hapo? unakula rushwa, unaongea matusi hivyo vyote ni vikwazo, unawasengenya wengine, hatujui kuwa sisi ni barua inayosomwa na watu wote. Ujenzi wetu wa mwisho unapaswa uthaminiwe kama ulivyokuwa ule wa kwanza.

Vinginevyo tutajikuta tunakwenda kulaumiwa kwa kuwakosesha wengine,. Na adhabu ya kuwakosesha wengine ni kubwa Zaidi, Bwana Yesu alitoa mfano wake na kusema ni heri mtu wa namna hiyo angefungiwa jiwe la kusagia na kutupwa baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hao.

Hivyo kama tumedhamiria kweli kumfuata Kristo, basi kila siku tujiangalie, tujiwekee mipaka, tuhakikishe ndani yetu hakuna mahali popote pa kumkwaza asiye amini..kuvaa vizuri ni mipaka!, kutokushiriki usengenyaji ni mipaka, kutoshiriki mazungumzo ya mizaha na kujiheshimu ni mipaka…Bwana atusaidie sote katika hilo.

Ubarikiwe. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

HAMJAFAHAMU BADO?

NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI.

NGUVU YA UPOTEVU.

 

 

http://wanatai.wingulamashahidi.org/

 

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments