Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?

Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?

SWALI:Tunasema Yesu karejesha kila kitu Adamu alichopoteza pale Edeni, Lakini kiuhalisia mbona hajarejesha kila kila kitu, mbona tunaona kifo bado kipo, mbona waovu ndio wanaotawala dunia, mbona magonjwa na ajali vinakithiri duniani?


JIBU: Ni kweli kabisa Bwana wetu Yesu Kristo, amekabidhiwa umiliki wa vitu vyote, Kuanzia juu mbinguni, mpaka huku duniani, vyote vipo chini yake. Na kazi kuu aliyokuja kuifanya ni kuvirejesha vyote vilivyoharibiwa na adui, katika nafasi yake, na hata Zaidi yah apo.

Mathayo 11: 27a Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu;..

Soma pia,

Waefeso 1:20 “…. akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;

21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;

22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo

23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”.

Basi kama ni hivyo, utauliza ni kwanini basi, hatuoni mamlaka yake yote yakitimia ulimwenguni?

Jambo ambalo watu wengi hawajui ni  kuwa, Huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo haijaishia pale tu alipopaa kwenda mbinguni..bali aliondoka kwa muda tu, akaahidi kurudi, Na ndio maana ujio wake,aliugawanya mara  mbili, ambapo mara ya kwanza alikuja kwa lengo la kuokoa roho za watu na mauti, ndipo hapo akalazimika kufa msalabani, ili damu ipatikane kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Hivyo kipindi chote hicho hakuhangaika, na mambo yoyote ya mwilini, au ya kiutawala, au ya kijeografia japokuwa alikuwa amekabidhishwa vyote.

Lakini ujio wake wa pili, hautakuwa tena kama ule wa kwanza, wenye lengo la wokovu wa roho za watu..Hapana, bali atakuja mahususi kwa lengo la kuukomboa huu ulimwengu na mifumo yake yote mibovu, Hapo ndipo atakapokuja kama mtawala, yaani MFALME WA WAFALME na BWANA WA MABWANA. Katika ule utawala wa miaka 1000 (Ufunuo 19:16)

Sasa atakapokuja katika awamu hii,

1) jambo la kwanza atakalofanya ataleta Amani duniani. Kutimiza lile andiko kwamba siku ile Mbwa-mwitu atalala Pamoja na mwana-kondoo, mtoto anyonyaje atacheka kwenye tundu la nyoka. (Isaya 11:5-9, 65:25)

2) Pili atadhibiti uchungu; Watu hawatazaa t tena kwa uchungu (Isaya 65:23)

3) Tatu atabidhibiti, magonjwa na maajali: Hilo ndilo litakalowafanya watu waweze kuishi miaka mingi hata karibia na 1000. (Isaya 65:20). Biblia inasema kipindi hicho, mtu atayekufa na miaka mia ataitwa mtoto mchanga.

4) Nne atadhibiti uharibifu: Yaani Hutajenga, akakaa mwingine, wala hutapanda akala mwingine..(Isaya 65:22)

5) Tano atadhibiti dhambi: Kumbuka wakati huo shetani atakuwa amefungiwa, na mtu yeyote atakayeonyesha dalili za uvunjifu wa amani, fimbo ya chuma, itamlalia.(Ufunuo 12:5)

6) Na mwisho kabisa atamalizana na  MAUTI, huyu ndiye adui wa mwisho.

Kiasi kwamba hakutakuwa na kifo tena ulimwenguni, wala machozi, wala maombolezo.

Hapo ndipo atakamporejeshea Baba mamlaka yote. Na kazi yake itakuwa imekwisha ya ukombozi. Na ndio hapo tutaingia katika ile mbingu mpya na nchi mpya, ambayo Jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

1Wakorintho 15:24 “Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.

25 Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.

26 ADUI WA MWISHO ATAKAYEBATILISHWA NI MAUTI”.

Hivyo, kwa kipindi hichi tulichopewa hapa katikati, tangu siku alipopaa hadi sasa, ni kuhakikisha kila mmoja, anaupokeo huo ukombozi wa roho yake, kwa gharama yoyote ile. Na hiyo inakuja tu kwa kumwamini Yesu Kristo, na kumpokea Roho wake.

Lakini kama mtu atakutwa katika hali ya dhambi hadi siku anayorudi mara ya pili, ajue kuwa hakuna neema tena ya ukombozi juu yake kwasababu Kristo ameshabadili ofisi. Wakati huo, atawaangamiza waovu wote kwa kuwaua kwa pumzi yake (Ufunuo 19:21). Kisha kwenda kuwatupa katika ziwa la moto.

Hivyo, uovu unaouna leo hii duniani ni wa kitambo tu, vita unavyoviona, uchungu, magonjwa na vifo, vyote vina muda mfupi. Hivi karibu Bwana anarudi, kuja kutawala na sisi kwa muda wa miaka 1000. Ndani ya hichi kipindi kila kitu kitarejeshwa katika hali yake.

Na ndio maana huna sababu ya kukimbizana na huu ulimwengu mbovu, ambao tumezungukwa na hatari ya kila namna, ndugu jiwekee hazina mbinguni, kwenye huo ulimwengu ujao wa amani unaokuja.

Lakini kwa bahati mbaya si wote watapokea neema hii ya kutawala na Kristo. Ikiwa utakufa leo katika hali yako ya dhambi. Utabakia huko huko makaburini hadi siku ile ya ufufuo, kisha uhukumiwe na kutupwa motoni.

Je! Bado unaendelea katika dhambi zako? Bado unaichezea tu hii neema? Kisa Kristo ni mpole sasa kwako unadhani atakuvumilia hivyo katika hali yako ya dhambi milele ? Ndugu yangu. Bwana Yesu Kristo ni mkuu kuliko unavyoweza kufikiri, utalithibitisha hilo, siku ile atakaporudi mara ya pili. Ambapo biblia inasema kila kinywa kitakiri, na kila goti litapigwa. Na mataifa watamwombolezea.

Heri ukampa Yesu Kristo Maisha yako angali bado una muda mchache, hivi karibuni Parapanda italia, Na Kristo atabadili ofisi yake.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments