NUNUA MAJI YA UZIMA.

NUNUA MAJI YA UZIMA.

Maji ya uzima, tunayoyasoma katika biblia sio maji ya chemchemi, wala ya bombani,  wala kisimani, wala ya mto Yordani ulioko kule Israeli na wala sio maji ya upako, yanayouzwa leo huku na huko.

Maji ya uzima ni jambo lingine la kiroho ambalo leo ningependa tuliangalie kidogo.

Katika kitabu cha Yohana, Bwana Yesu alijaribu kugusia kidogo kuwa maji ya uzima yaliyo hai…sio maji ya kisimani..

Yohana 4:5“ Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

 7 Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

8 Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.

9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)

10 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, UNGALIMWOMBA YEYE, NAYE ANGALIKUPA MAJI YALIYO HAI.

11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo MAJI YALIYO HAI?

12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;

14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; BALI YALE MAJI NITAKAYOMPA YATAKUWA NDANI YAKE CHEMCHEMI YA MAJI, YAKIBUBUJIKIA UZIMA WA MILELE.

15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka”.

Umeona hapo? jinsi Bwana alivyomfafanulia huyo mwanamke kuwa Yale maji anayoyadhania ya kisimani, sio maji ya uzima..Bali maji ya uzima ni kitu kingine kabisa lakini chenye tabia zinazofanana na hayo maji ya asili.

Sasa swali hayo maji ni nini?

Bwana Yesu, yeye mwenyewe alitupa majibu ya swali hili katika kile kitabu cha Yohana.

Yohana 7:37 “ Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, MITO YA MAJI YALIYO HAI ITATOKA NDANI YAKE.

39 Na NENO HILO ALILISEMA KATIKA HABARI YA ROHO, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; KWA MAANA ROHO ALIKUWA HAJAJA, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa”.

Umeona hapo?..Maji ya uzima ni ROHO MTAKATIFU.

Maana yake mtu anayepokea Roho Mtakatifu, anakuwa amekata kiu yote ya dhambi.

Kiu ya kunywa pombe na kuvuta sigara inakufa..kiu ya kufanya zinaa na uasherati inakufa, kiu ya kufanya mabaya inakufa, na mambo mengine yote mabaya..

Kwasababu yeye anatoa raha ambayo inazidi raha zote zinazopatikana katika mambo hayo ya  ulimwengu yasiyompendeza yeye..

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kumpokea Roho Mtakatifu.

Lakini pia jambo la muhimu kufahamu ni kuwa MAJI HAYA YA UZIMA maandiko yanasema TUNAYANUNUA. Lakini si kwa fedha, wala kwa mali..BALI KWA MAISHA YETU!. Yaani tunapompa Yesu maisha yetu, hiyo ni gharama tosha ya kununua maji hayo.

Fedha haiwezi kununua hayo maji..kwasababu si maji ya kimwilini bali ya kiroho.

Isaya 55:1 “Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.

2 Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono”.

Umeona tena hapo??..anasema Njooni MNUNUE bila fedha na si NJOONI MCHUKUE BILA FEDHA. Maana yake hayo maji yananunuliwa lakini si kwa fedha bali kwa kitu kingine..Na hicho si kingine zaidi ya MAISHA YETU. Yaani kumpa yeye na kubatizwa.

Swali ni je??. Umempokea huyu Yesu? Na kubatizwa ubatizo sahihi wa maji tele na kwa Jina la Yesu?..Kumbuka hiyo ndiyo tiketi pekee ya kuyapata hayo maji, hakuna njia nyingine.

Bwana Yesu anasema..

Ufunuo wa Yohana 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.

Je unayataka maji ya uzima leo?

Mwamini Yesu na tubu dhambi zako leo kwa kumaanisha kuziacha, na ukabatizwe kama bado hujafanya hivyo.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312 Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Ubarikiwe..sasa nimeelewa

JOSHUA AMIRI MUTUNGU
JOSHUA AMIRI MUTUNGU
2 years ago

Asante Sanaa mtumishi wa Mungu,nmebarikiwa Sanaa

Friedrich@son ofJESUS%
Friedrich@son ofJESUS%
2 years ago

Barikiwa sana mtumishi wa BWANA!
Nimetambua kumbe unaweza kusema , nimeokoka; kumbe bado hujayapata MAJI YA UZIMA {ROHO}