USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

Shalom jina Kuu la Mwokozi wa Ulimwengu, Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu lililo hai.

Katika biblia tunasoma kisa cha Nabii Mmoja aliyetumwa na Mungu kwa mfalme Yerobohamu, amtolee unabii juu ya maovu anayoyafanya, ambayo kwa hayo anawakosesha Israeli yote. Na nabii Yule alipomaliza kutoa unabii ule, kama tunavyosoma, Mungu alimwonya asirudi kupitia njia ile aliyoijia, wala asile kitu njiani, wala asiingie kwenye nyumba ya mtu yeyote.  Na alipomaliza kutoa unabii ule kwa Mfalme Yeroboamu aliondoka mbele zake na kwenda kama Bwana alivyomwagiza.

 Lakini tunasoma wakati yupo njiani alitokea Nabii mwingine, akamwambia kuwa “Mungu kamwonyesha kwamba arudi aingie nyumbani kwake ale”. Lakini Nabii Yule alidanganya, Mungu hakumwambia chochote. Alitaka tu Yule nabii arudi, apumzike kwake..Na Yule nabii aliyetumwa na Mungu kutoa unabii, bila kufikiri mara mbili, alijikuta anarudi na kuungana na huyu nabii wa uongo, na hatimaye kufanya dhambi.

Tusome.

1Wafalme 13:7 “Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.

8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;

9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.

10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.

12 Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.

13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.

14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.

15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.

16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;

 17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia

18 AKAMWAMBIA, MIMI NAMI NI NABII KAMA WEWE, NA MALAIKA AKANIAMBIA KWA NENO LA BWANA, KUSEMA, MRUDISHE PAMOJA NAWE NYUMBANI KWAKO, ALE CHAKULA, AKANYWE MAJI. LAKINI ALISEMA UONGO.

19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.

20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;

 21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, KWA SABABU UMEIASI KAULI YA BWANA, WALA HUKUISHIKA AMRI ILE ALIYOKUAMURU BWANA, MUNGU WAKO,

 22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.

23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.  24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.

 25 Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.

26 Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya Bwana; kwa hiyo Bwana amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia.”

Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho, yaliyomtokea huyu mtu wa Mungu wa kweli, ndio yanayoendelea kuwatokea wengi katika siku hizi za Mwisho. Wengi wanarudishwa nyuma na kuangushwa na watu wanaojiita watumishi wa Mungu, ambao pengine hapo kwanza waliowaona wakitoa unabii wa kweli, na ukatimia,  ambao hapo kwanza waliwaona wakifanya miujiza mingi, watu hawa wanajitambulisha mbele za watu kuwa ni watumishi wa Mungu, na Mungu anazungumza nao, lakini wanadanganya n.k.

Lakini jambo la kuogopesha na kustaajabisha ni kwamba, japokuwa ni waongo, ni wazinzi, ni walevi wengine..lakini upako wa Mungu haujawaacha…wataendelea kusikia sauti ya Mungu ikiwapa unabii wa kweli, wataendelea kufanya miujiza mingi..LAKINI  NI WAONGO!!!, mfano wa huyu Nabii mzee, alimdanganya mwenzake tena kwa jina la Bwana, lakini tunaona bado Mungu aliendelea kuzungumza naye…anaendelea kumpa unabii tena wa kweli kabisa na si wa uongo!!. Hilo ni jambo la kuogopesha sana kwa kweli, ikifunua kuwa sio tu kutoa unabii ndio tiketi ya kuwa mtumishi wa Mungu wa ukweli. Hapana!!..

 Leo hii manabii na watumishi kama hawa wapo wengi, wanakuja na “BWANA ANASEMA HIVI, yeye hatazami mavazi anatazama roho, na wanalithibitisha neno hilo kwa kutoa ishara Fulani, ya kiungu” Lakini kumbe ni waongo, wanajua kabisa “Mwili wa mtu ni hekalu la Mungu, lakini wanadanganya makusudi ili kupata faida Fulani kutoka kwa Yule mtu”…na wengi  pasipo kusimama katika Neno la Mungu wanachukuliwa na uongo wao.

Kwamfano Neno la Mungu limetuambia…

Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate”.

Na tena inasema..

Luka 17:32  “Mkumbukeni mkewe Lutu.

33  Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya”.

Lakini anatokea Mtu anayejiita (mtumishi wa Mungu), anakuambia.. Kumfuata Yesu hakuna haja ya kujikana, huna haja ya kubeba msalaba wako, huna haja ya kuacha kuvaa nguo za kikahaba, huna haja ya kuacha kupaka wanja na lipstick, huna haja ya kumwacha mtu unayeishi naye ambaye si mke wako/mume wako, huna haja ya kuuacha ulimwengu!!…. Nataka nikuambie, unarudishwa Betheli na huyo Nabii bila wewe kujijua!. Jiokoe nafsi yako, rudi katika agizo la awali la Mungu katika Neno lake.

Biblia ndio kitabu pekee kinachotupa maelekezo sahihi jinsi ya kuishi kulingana na mapenzi ya Mungu, na si unabii wa mtu yeyote, akitokea mtu yeyote akitoa unabii, na ule unabii unakinzana na Neno la Mungu, biblia imetuonya tusimsikilize huyo nabii haijalishi katoa ishara kubwa kiasi gani, hata kama atashusha moto kama Eliya, lakini kama atatuambia ni ruksa kuishi maisha ya uzinzi, huyo nabii tumeambia tujihadhari naye.

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

 2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

 4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye”

Dada Mhubiri wako anayekuambia kuwa kuvaa vimini na suruali si dhambi!..anakudanganya, usipumbazike na unabii anaotoa,au ishara anazozifanya..wewe litazame Neno la Mungu…linalosema.

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe KWA MAVAZI YA KUJISITIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu. 2.11  Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna”.

Mhubiri anayekuambia kuwa Ulevi si dhambi, na mtu unaweza kuoa mke zaidi ya mmoja, Usimsikilize, bali lisikilize Neno la Mungu linalosema…

Waefeso 5:17  “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.

18  Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”.

Mhubiri anayekuambia kwamba Bado sana Kristo arudi, na kwamba endelea kuponda mali, na kujitumainisha na ulimwengu…Usimsikilize, bali lisikilize Neno la Mungu linalosema..

Mathayo 24:43  “Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44  Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.

Na mambo mengine yote, yanayozungumzwa na yeyote anayejulikana kama mtumishi wa Mungu, ni muhimu kuyaweka katika mizani ya Neno la Mungu, kuyapima..kama yanakubaliana na Neno au la!..Kama hayakubaliani basi tunayaweka chini na kulifuata Neno la Mungu, kwasababu tumeshaonywa tuwe watu wa kuzipima roho.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

BIRIKA LA SILOAMU.

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

Rudi nyumbani > jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments