WAKO WATATU WASHUHUDIAO MBINGUNI NA DUNIANI.

WAKO WATATU WASHUHUDIAO MBINGUNI NA DUNIANI.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu.

Maandiko yanasema kuwa wapo watatu washuhudiao mbinguni, na vile vile wapo watatu washuhudiao duniani.

1Yohana 5:7 “Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.

8 Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, BABA, NA NENO, NA ROHO MTAKATIFU, na watatu hawa ni umoja.

9 Kisha wako watatu washuhudiao duniani], ROHO, NA MAJI, NA DAMU; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe”.

Lakini swali la kujiuliza ni je!, hao watatu NI WAKINA NANI na WANASHUHUDIA NINI na WANASHUHUDIAJE?

Kama ukianzia juu kidogo katika habari hiyo utaona Mtume Yohana alikuwa anajaribu kuelezea habari za ushuhuda wa Yesu kuwa ndiye “Mwana wa Mungu”. Alikuwa anajaribu kuelezea kuwa habari ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, sio jambo la kutunga tu!, bali mbingu na nchi zimelishuhudia hilo. Na akawa anajaribu kueleze vitu vikuu vilivyoshuhudia au kulithibitisha hilo, vilivyopo duniani na vilivyopo mbinguni..

Na vitu hivyo ndio Mtume Yohana kwa ufunuo wa Roho anaviorodhesha. Kwamba kwa duniani ni ROHO, MAJI na DAMU.. Na kwa mbinguni ni BABA, NENO na ROHO. Sasa ni kwa namna gani vitu hivi vinashuhudia

1Yohana 5:5 “Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba YESU NI MWANA WA MUNGU?

6 Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu.

7 Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli”.

Hebu tuanze kuutazama Ushuhuda kutoka mbinguni.

Tusome.

Mathayo 3:16 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona ROHO WA MUNGU akishuka kama hua, akija juu yake;

17 na tazama, SAUTI KUTOKA MBINGUNI IKISEMA, HUYU NI MWANANGU, MPENDWA WANGU, ninayependezwa naye”.

Hapo tunaona vitu vitatu vimeshirikiana kumshuhudia Kristo kama ni Mwana wa Mungu. Cha kwanza ni SAUTI ambayo ndio NENO. (Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu). Cha pili ni BABA ambaye ndiye kazungumza maneno hayo, na cha tatu ni ROHO ambaye ndiye kashuka juu yake kama Hua (yaani njiwa)..kuyathibitisha maneno ya Baba.

Kwahiyo unaweza kuona hapo BABA, kazungumza NENO kutoka mbinguni, kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu kweli,  na Kamshusha ROHO wake kulithibitisha neno lake hilo.

Hivyo kutimiza hilo Neno linalosema wapo watatu washuhudiao mbinguni BABA, NENO na ROHO.

Lakini Sehemu ya pili inasemaje?.. Wapo watatu pia washuhudiao duniani, nao ni ROHO, DAMU NA MAJI..Sasa ni kwa namna gani hawa wanashuhudia kuwa ni kweli Yesu ni Mwana wa Mungu, kama vile Baba alivyoshuhudia kwa Neno na Roho?.

Tusome,

Yohana 19:33 “Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;

34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara IKATOKA DAMU NA MAJI.

35 NAYE ALIYEONA AMESHUHUDIA, NA USHUHUDA WAKE NI KWELI; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki”.

Umeona hapo?. Huyu Askari alipofika kwa Bwana Yesu na kumchoma ubavuni kwa mkuki, akashangaa kuona MAJI mengi yanatoka,  jambo ambalo sio la kawaida, na baadaye inatoka DAMU. Kwa ishara ile Askari yule akakiri ya kwamba YESU NI MWANA WA MUNGU, na hapo Mtume Yohana anatia msisitizo kuwa “huyo Askari aliyeona ameshuhudia na ushuhuda wake ni kweli”.

Sasa utauliza mbona hapo maandiko hayajaonyesha kama Askari huyo kashuhudia kwamba YESU NI MWANA WA MUNGU kwa tukio hilo?.

Jibu ni kwamba alishuhudia hilo, na kukiri kwamba YESU NI MWANA WA MUNGU Baada ya kulishuhudia tukio hilo la kifo cha Yesu.Tunaweza kusoma habari hiyo vizuri tena katika kitabu cha Marko..

Marko 15:39 “Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu”.

Kwahiyo MAJI na DAMU vilivyotoka katika mwili wa Bwana Yesu, Na SAUTI (yaani NENO) la BABA, lililoshuka juu yake wakati anabatizwa. VINASHUHUDIA KUWA YESU NI MWANA WA MUNGU. Kadhalika Maji yaliyotoka ubavuni mwa Yesu, na Damu yake iliyomwagika Kalvari, vinatushuhudia kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu.

Ndio maana na sisi ili Baba atushuhudie kuwa ni WANA WA MUNGU, kama alivyomshuhudia mwanaye ni lazima na sisi tuwe na ushuhuda wa MAJI, na ROHO na DAMU tukiwa hapa duniani.

Maana yake ni kwamba lazima tubatizwe kwa MAJI na kwa ROHO MTAKATIFU na kutakaswa kwa DAMU. Tusipofanya hivyo sisi sio wana wa Mungu mbele za Baba mbinguni na wala hatatushuhudia. Bwana Yesu aliposhuka pale Yordani kubatizwa kwa MAJI na ROHO aliposhuka juu yake ndipo sauti ikasikika kuwa yeye ni mwana wa Mungu. Na sisi ni hivyo hivyo, ni lazima tuwe na ushuhuda huo wa kubatizwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu, ili Damu ya Yesu iweze kutusafisha.. kutushuhudia kuwa sisi ni wana wa Mungu.

Yohana 3:5 “Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu”.

Leo hii ubatizo unapuuziwa sana na wengi ni kwasababu bado hawajaelewa ufunuo uliopo katika ubatizo.

Ukielewa ufunuo uliopo katika ubatizo, ndipo utajua hicho kitu ni cha umuhimu kiasi gani.. Ilimpasa Kristo abatizwe ili sauti ije juu yake kuwa yeye ni Mwana wa Mungu, inatupasaje sisi?.. Ubatizo ni tendo dogo lakini lina madhara makubwa sana katika Roho.

Na kumbuka ubatizo halisi na wa kweli, si ule wa vichanga bali ni lazima mtu ajitambue na kuamua kukiri kwa kinywa chake, Bwana hakushindwa kubatizwa wakati akiwa na siku nane, kipindi anakwenda kutahiriwa.. vyote hivyo viwili vingeweza kwenda pamoja.. Lakini ilimpasa awe mtu mzima kwanza.

Vile vile ubatizo sahihi ni kwa jina la BWANA YESU KRISTO, kulingana na Matendo 2:38, Matendo 8:16, Matendo 10:48, na Matendo 19:5.

Bwana atufumbue macho tuzidi kumwelewa.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MJUE SANA YESU KRISTO.

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

Neno “Via” linamaanisha nini katika biblia?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

BIRIKA LA SILOAMU.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Barikiwa mtumwa wa kristo!

Friedrich@son of JESUS%
Friedrich@son of JESUS%
2 years ago

Amina mtumishi!
Nuru ya BWANA na izidi kutumlikia; ili tusiwe vipofu tena!