Je kauli ya Bwana Yesu inajichanganya? Katika Yohana 8:14 na Yohana 5:31?

Je kauli ya Bwana Yesu inajichanganya? Katika Yohana 8:14 na Yohana 5:31?

Katika Yohana 5:31, tunasoma Bwana Yesu anasema “Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli.” Na ukiendelea mbele kidogo katika Yohana 8:14 anasema tena “mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli”.. Sasa hapo, tuamini lipi na tuache lipi?


Jibu: Awali ya yote ni muhimu kufahamu kuwa kauli zote hizo mbili zimeoka ndani ya kitabu kimoja, cha Yohana, tena ni katika utofauti wa sura 3 tu, na mwandishi ni huyo huyo mmoja Yohana, hivyo kwa vyovyote vile asingeweza kuandika kauli mbili zinazokinzana, tena ndani ya  waraka mmoja, kwasababu ni lazima alihakiki waraka huo mara nyingi kabla ya kuutoa..

Kwa muhtasari huo basi tutakuwa tumeshajua kuwa Kauli mbili hizo hazikinzani, bali ni fahamu zetu ndio zimeshindwa kuzipambanua.

Hivyo leo tutakwenda hatua kwa hatua  kuzichambua kauli hizo, na mwisho tutaona kabisa kuwa hazikinzani hata kidogo.

Hebu tuanze na kauli ya kwanza tunayoisoma katika Yohana 8:14, lakini tuanzie juu kidogo kuanzia mstari wa 12 halafu tuendelee hadi wa 18..

Yohana. 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

13 Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.

14 YESU AKAJIBU, AKAWAAMBIA, MIMI NINGAWA NINAJISHUHUDIA MWENYEWE, USHUHUDA WANGU NDIO KWELI; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako………..

17 TENA KATIKA TORATI YENU IMEANDIKWA KWAMBA, USHUHUDA WA WATU WAWILI NI KWELI.

18 MIMI NDIMI NINAYEJISHUHUDIA MWENYEWE, NAYE BABA ALIYENIPELEKA ANANISHUHUDIA.”

Hapo katika mstari wa 17, anasema “Ushuhuda wa watu wawili ni kweli”. Maana yake wakitokea wawili wanaoshuhudia kitu kimoja basi ule ushuda ni wa kweli..

Sasa kulingana na Maneno hayo ya torati..maana yake ni kwamba Ushuhuda wa Yesu kwamba yeye ndiye Nuru ya ulimwengu, Mwana wa Mungu NI KWELI!!

Kwasababu Yeye mwenyewe (Yesu) kwanza anajishuhudia, HUYO NI WA KWANZA!! na kisha Baba yake mwenyewe amemshuhudia HUYO NI WA PILI…(Na alimshuhudia pale sauti ilipotoka  mbinguni na kusema huyu ni mwanangu mpendwa wangu niliyependezwa naye)…

Hivyo mpaka kufikia hapo, tayari wameshapatikana wawili wanaoshuhudia kitu kimoja, ambao ni YESU MWENYEWE na BABA MBINGUNI.. Kwahiyo ushuhuda anajishuhudia Yesu ni kweli.. kwasababu torati imesema “ushuhuda wa watu wawili ni kweli”..na hapo idadi imeshatimia wawili..

Maana yake angekuwa ni Yesu peke yake anajishuhudia na hakuna mwingine, huo ushuhuda ungekuwa ni uongo.

Ndio maana tukirudi sasa kwenye Mlango wa 5 katika kitabu hicho hicho cha Yohana, tunaona Bwana Yesu ndio analifafanua jambo hilo kwamba, angekuwa ni yeye mwenyewe anajishuhudia (yaani yupo yeye peke yake na hakuna mwingine wa kumshuhudia, basi ushuhuda wake ungekuwa ni wa UONGO),

Yohana 5:31 “MIMI NIKIJISHUHUDIA MWENYEWE, USHUHUDA WANGU SI KWELI.

32 YUKO MWINGINE ANAYENISHUHUDIA; NAMI NAJUA YA KUWA USHUHUDA WAKE ANAONISHUHUDIA NI KWELI. …………….

37 Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona.”

Umeona hapo? hakuna ukinzani wowote katika kauli hizo mbili. Ni fahamu zetu tu ndizo zinazojichanganya, na kushindwa kuelewa.. Yesu kamwe hajawahi kujichanganya katika maneno yake wala hajawahi kusema uongo.. Sisi ndio tunaojichangaya katika maneno yetu na ndio tunaosema uongo!, na kuwa vigeugue.

Hivyo kupitia habari hiyo  tunachoweza kujifunza kikubwa ni kwamba YESU kashuhudiwa na Baba, kuwa ni Mwana wa Mungu.. “Sauti ilisikika kutoka mbinguni kuwa yeye ni Mwana wa Mungu”, na zaidi ya yote ni NURU ya Ulimwengu. Na mtu yeyote atakayemfuata hatakwenda gizani.

Je wewe tayari umemfuata mwokozi Yesu, ambaye ndiye Nuru ya Ulimwengu?.. au bado upo gizani?.

Na utajitambuaje kama upo gizani, ni kwa matendo ya giza unayoyafanya..na mfano wa matendo ya giza ndio hayo; uzinzi, usengenyaji, wizi, utukanaji, uasherati, kutazama picha chafu mitandaoni, kujichua, kuvaa nguo za kubana, na zisizo na heshima, kujipodoa, kuupenda ulimwengu zaidi ya Mungu (kama kuwa mshabiki wa mipira na mambo ya kidunia, ambayo yanaziba hata nafasi ya kuwa karibu na Mungu) n.k Hakuna mtu yeyote aliyemfuata Yesu kweli kweli akawa anafanya hayo matendo au yanayofanana na hayo…

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATIKA HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU”.

Kama bado hujampokea Yesu, saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubalika ndio huu..Hakuna wakati fulani utasema “nitampokea Yesu, au nitaokoka!”. Huo wakati HAUPO!.. Kama utakuwepo basi biblia itakuwa ni Uongo!, iliposema “saa ya wokovu ni sasa!!”.

Hivyo usingoje kesho, fanya uamuzi sasa hivi, pale ulipo piga magoti, kisha kiri na tubu dhambi zako zote kwa Bwana Yesu, naye ni mwaminifu, atakusamehe.. Na baada ya kutubu, fanya hima kutafuta ubatizo, kwa maana ubatizo ni nguzo muhimu sana katika kuukamilisha wokovu wako, ni huyo huyo uliyemwomba Toba, ndiye aliyeagiza kuwa baada ya kuamini ukabatizwe, na ubatizo sahihi sio wa kunyunyiziwa wala wa vichanga, bali ni wa kuzama mwili wote na kwa JINA LA YESU KRISTO (Matendo 2:38) na si vyeo vya utatu.

Kama utahitaji msaada katika kuongozwa sala ya toba basi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba hizo hapo chini.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

UFUNUO: Mlango wa 1

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen

Maige
Maige
2 years ago

Amen