Monthly Archive May 2022

Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.

Injili ya Yesu Kristo imejificha katika viumbe vya asili. Bwana mahali biblia inamfananisha Bwana Yesu na Mwanakondoo, sehemu nyingine kama Simba, sehemu nyingine Bwana Yesu anafanishwa na “Jiwe” , mahali pengine Roho Mtakatifu anafanishwa na Huwa (njiwa).

Lakini pia kuna mahali Bwana Yesu alituwaambia tuwatazame kunguru pamoja na Maua ya kondeni (Luka 12:24), na sehemu nyingine aliufananisha mbinguni na Wafanya biashara, na sehemu nyingine wakulima, na sehemu nyingine aliufananisha na wavuvi wanaokwenda kuvua..Na sehemu nyingine aliwafananisha watu kama samaki wanapaswa kuvuliwa.

Kwahiyo kwa ufupi ni kwamba Injili ya Bwana Yesu Kristo imejificha pia  katika viumbe vya asili. i.

Hivyo wakati mwingine hatuna budi kujifunza juu ya baadhi ya  viumbe, na kupata hekima..

Leo tutamtazama Samaki mmoja aitwaye Eeli.

Je unamjua Samaki aina ya Eeli? Je unayajua maajabu yake?, na Injili gani imejificha nyuma ya Maisha yake?

Eeli ni Samaki ambao ni familia moja na Kambale. Samaki hawa wanaishi katika maji mafupi, . Lakini Samaki hawa maajabu yake ni kwamba wanatengeneza umeme mkubwa sana katika miili yao, ambao umeme huo wanautumia kujilinda dhidi ya maadui na kujitafutia vitoweo.

Eeli  anapokumbana na hatari mbele yake, labda Samaki mwingine aliye mkubwa kuliko yeye, au kiumbe kingine chenye kutishia usalama wake,  basi huitoa shoti hiyo na kumpiga adui yake.

Na kiwango cha umeme Samaki Eeli mmoja anachoweza kuzalisha kwa pigo moja ni mpaka Volti 650, na wakati Volti za 150 tu zinatosha kumuua Mwanadamu, lakini yeye hutoa hadi volti hizo 650, ambazo kama zikimfikia mwanadamu, sio tu kumuua papo kwa hapo, bali pia zinaweza kumuunguza viungo vyake vya ndani.

Lakini Pamoja na kwamba Samaki huyu, anayo silaha hatari namna hiyo kuliko samaki wote,  ambayo inaweza kumuua mtu au kiumbe hai chochote ndani ya dakika moja, lakini bado ni Samaki mpole sana, bado hayupo katika orodha ya viumbe au viumbe hatari duniani. Hayupo hata 100 bora ya viumbe hatari, hata samaki sangara kamzidi kwa ukali!.

Ni samaki ambaye ni hatari sana lakini anayejihadhari sana na maadui zake, na asiyetumia uwezo wake wote kiasi kwamba hata ikitokea kakanyagwa na mtu ndani ya maji kwa bahati mbaya,  yeye hutoa  kiwango kidogo tu cha shoti, ambacho kitamshtua adui yake, amwache au akae mbali naye lakini si kumuua kabisa.

Tofauti na Samaki wengine kama samaki jiwe, au jelly au papa ambao hawana silaha kali kama hiyo,  lakini ni wakorofi mno, kiasi kwamba akipita adui mbele yao, au akihisi hatari basi ana uwezo wa kutumia uwezo wake wote, kudhuru.

Laiti Eeli angekuwa mwenye hasira kama za Papa, au samaki mwingine yeyote, leo hii engeshika nafasi ya kwanza kwa viumbe hatari ulimwenguni. Kwasababu hakuna kiumbe chochote chenye silaha kali kama hiyo, hata nyoka ijapokuwa sumu yake ni kali na inayoua kwa haraka, kama mtu hajapatiwa matibabu..

Eeli yeye silaha yake ya shoti, inaua papo kwa hapo endapo akitumia uwezo wake wote. Na kutokana na maisha yake hayo imemfanya kuwa moja ya samaki wanaoishi muda mrefu sana, mpaka kufikia miaka 85.

Ni nini tunajifunza kwa Eeli?

Na sisi kama watu wa Mungu, tunazungukwa na nguvu za Mungu,  kwa kiwango kikubwa sana… Lakini Nguvu hizi hatupaswi kuzitumia kuharibu wengine, nguvu hizi zimo ndani yetu, kutulinda tu na mishale ya yule adui, lakini si kutufanya tuonekane watofauti duniani.

Hebu tumtazame mmoja aliyekuwa kama huyu Samaki Eeli, ambaye alikuwa na nguvu nyingi kuliko wote, lakini hakuutumia uwezo wake wote..

Tusome,

Luka 9:51 “Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;

52 akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.

53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.

54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?

55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]

56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”.

Hapo Bwana Yesu alikuwa ana uwezo wa kushusha moto, na ndani ya dakika moja wale wale wasamaria wangekufa wote, bila kubakia hata mmoja lakini, hakuutumia uwezo wake huo, bali aliwarehemu kwasababu alikuwa anajua hawajui watendalo. Soma tena kisa kama hicho hicho katika Mathayo 26:51-53.

Na sisi pia hatuna budi kuwa kama Bwana Yesu..Bwana Yesu alipigwa lakini hakurudishwa, ingawa alikuwa na uwezo wa kurudisha mapigo makali, alitukanwa lakini hakurudisha matusi, aliambishwa lakini hakuabisha, ingawa alikuwa na uwezo wa kuabisha..n.k.

Alikuwa mfano wa Eeli ambaye anao uwezo mwingi lakini ni pole..

Wafilipi 4:5 “Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu”.

Hatupaswi kuwalaani watu kwa jina la Bwana, hata kama wanatumia nguvu za giza, tunachopaswa kukilaani na kukiharibu ni zile kazi wanazozifanya, na tunazilaani kwa kuomba, kuhubiri, kusoma Neno na kuishi maisha matakatifu..

Tuwe kama Eeli.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

UNAMCHUKULIA YESU KWAKO KAMA NANI?

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.

UVUVI BORA HAUCHAGUI, CHA KUVUA.

Nini tofauti ya Uwezo na Uweza kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri.

SWALI: Mwandishi, alimaanisha nini, kusema Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi? (Wimbo 1:5-6)


JIBU: Tusome,

Wimbo 1:5 “Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za Kedari, Kama mapazia yake Sulemani.

6 Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda”.

Huyu ni mwanamke , anayejaribu kueleza hali yake ya nje jinsi inavyoonekana, ilivyo tofauti na uhalisia wake wa ndani. Anaanza kwa kusema mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Yaani japokuwa naonekana ni mweusi, nisiyevutia, lakini ninao uzuri wa kupendwa hata na mfalme,

Mstari wa 6 anaendelea kueleza Weusi wake, ulitokana na nini,.. Anasema, ulitokana na kazi za mashambani, ambazo aliwekwa kama mlinzi azisimamie, ikiwa na maana muda wote a jua linapochomoza jua linapozama, ni lazima awepo pale alitunze,

Wakati ndugu zake, wakiwa wamestarehe nyumbani kwenye uvuli wa makasri, wakila na kufurahi, yeye yupo mashambani anatanga na jua.

Na kwa kawaida, mtu anayekaa kwenye jua muda mrefu Ngozi yake itakuwa nyeusi tu, na vilevile itapunguza mvuto. Ndicho kilichomkuta huyu binti, aliyekuwa tofauti na mabinti wengine, kama ilivyozoeleka kuwa  mabinti huwa hawakai mashambani, wala hawafanyi shughuli  za ulinzi, . Lakini yeye alikuwa hivyo, na katika hayo yote anasema bado anaoozuri unaotoka ndani.

Hii inafunua nini kwetu, au ni ujumbe gani tunapitishiwa sisi ?

Huyu binti anafananishwa na watumishi wa Mungu, wanaotumika katika shamba la Mungu, ambao pengine kutwa kucha wanajitaabisha kuwapelekea wengine Habari njema,(Vijinini na mijini, na kwa njia mbalimbali), sasa kwa taabu hizo, kwa kawaida ni lazima watakosa vitu vingi vyema, kwasababu muda wote wapo mashambani, pengine watakuwa wadhaifu kimwili/au kimwonekano, watakuwa hawana mali, watakuwa hawana mvuto wowote. Lakini Bwana anawaona ni wazuri sana,

Mtume Paulo aliliona hilo akasema,

2Wakorintho 4:16 Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;

 18 tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.

Kuonyesha kuwa utu wetu wa nje, waweza kuchakaa kwasababu ya utumishi, lakini ule wa ndani wafanywa upya kila siku, Sehemu nyingine aliandika Maisha ya utumishi ni ya kufa kila siku, kujitoa kwa wengine na sio kwa ajili yako, kama huyu binti (1Wakorintho 15:31).

Hivyo na wewe ambaye, unamtumikia Bwana kwa uaminifu, pengine  wajiuliza, mbona mwonekano wangu haupo, kama nilivyokuwa hapo nyuma simtumikii? Fahamu kuwa upo shambani, jua litakuwa ni lako, lakini uzuri wako unatoka ndani na Mungu anauona, na anapendezwa na wewe.

Siku zitakuja, utapewa mwili wa utukufu, mwili usioonja uharibifu, mwili wa milele, ndipo utakapojua kuwa wewe ulipendwa na Bwana, na hiyo haikuwa kwa mwonekano wako, lakini kwa uaminifu wako.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UBATILI.

KUJIPAMBA NI DHAMBI?

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

Biblia inamaana gani kusema “vipo sita, naam saba”?

Kuvyaza ni nini katika biblia? (Ayubu 21:10).

KWANINI MIMI?

ANGALIA UZURI WAKO, USIGEUKE KUWA KITANZI CHAKO.

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

Donda-Ndugu ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

Je unajua ubatizo unaua na vile vile unaokoa?.

Ipo siri kubwa sana katika ubatizo ambayo laiti watu wengi wangeijua wangeutafuta kwa bidii zote.

Hebu tusome mistari ifuatayo,

1 Petro 3:20 “watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, WALIOKOKA KWA MAJI.

21 MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO, UNAOWAOKOA NINYI PIA SIKU HIZI; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo”.

Hapo kuna vitu 3 vya kuzingatia katika mistari hiyo..na tutatazama kipengele kimoja baada ya kingine.

  1. WATU WANANE WALIOKOKA KWA MAJI.

Hapa tunachoweza kuona ni kwamba..“kumbe maji ni njia ya wokovu?”. Nuhu pamoja na mkewe na wanawe watatu na wake zao, jumla nafsi 8, waliokoka kwa maji!!!!! 

Wakati wengine wasioamini wanaangamia kwa maji, Nuhu aliyeamini, maji hayo hayo yanamwokoa na ghadhabu ya Mungu. Hili ni jambo la kwanza la kuzingatia…hebu tulitazame jambo la pili.

2. MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO, UNAOWAOKOA NINYI PIA SIKU HIZI.

Kumbe kama Nuhu alivyookoka kwa Maji zamani hizo, na sisi siku hizi hatuna budi kuokoka kwa kupitia maji hayo hayo? Yaani kwa Kubatizwa. Si ajabu Bwana Yesu alisema katika Marko 16:16 kuwa..“Aaminiye na kubatizwa ataokoka”..na si “atakayeamini tu peke yake”

Huu ni ufunuo mkubwa sana ambao Mtume Petro alifunuliwa na Roho Mtakatifu..

Kumbe wakati sisi tunasoma habari za gharika ya Nuhu kama gazeti, kumbe nyuma yake kuna ufunuo wa ubatizo..

Si ajabu na Yohana Mbatizaji pengine naye alitolea ufunuo wa ubatizo humu humu.
Unapomwamini Yesu (Ni sawa na umeingia ndani ya safina kama Nuhu)..unapobatizwa kwa kuzamishwa katika maji mengi na kuibuka juu (Ni sawa na umeingia kwenye gharika ukiwa ndani ya safina na umetoka salama).

Na kama vile baada ya gharika Mambo yote yakawa mapya kwa Nuhu, akaingia katika ulimwengu mpya na kuanza maisha mapya, yale ya kwanza yenye shida na dhuluma na maasi yamepita. (Kwa ufupi uchafu wote wa kwanza ukaondoka).

Vivyo hiyo na sisi tunapobatizwa katika roho tunaondoa uchafu wote unaozunguka maisha yetu ya kiroho… Yale maisha ya kale yanazikwa, zile dhambi za kale zinaisha nguvu, kile kiburi cha kale kinafifia n.k
Faida hii kuu inatupeleka katika kipengele cha tatu na cha mwisho.

 3. SIYO KUWEKEA MBALI UCHAFU WA MWILI, BALI JIBU LA DHAMIRI SAFI MBELE ZA MUNGU.

Kumbe lengo la ubatizo sio kuondoa uchafu wa mwilini kama JASHO au VUMBI..bali ni kuondoa uchafu wa rohoni ambao huo ndio jibu la Dhamiri zetu safi mbele za Mungu.

Swali ni Je! umebatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu kulingana na Matendo 2:38?.

Kama bado unasubiri nini na tayari umeshajua faida zote hizi?..Haraka sana katafute ubatizo sahihi, kwa gharama zozote baada ya wewe kumwamini Bwana Yesu na kutubu dhambi zako.

Kama unapata ugumu kupata sehemu ya ubatizo, basi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba zilizopo chini ya somo, tutakusaidia, kukuelekeza mahali karibu na ulipo.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

UBATIZO NI NINI NA ULIO SAHIHI NI UPI?

KWANINI UBATIZO NI WA MUHIMU.

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

Je! Unaweza kubatizwa na usipokee Roho Mtakatifu?. Na Je! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono?

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Rudi nyumbani

Print this post

MIKONO YENU IMEJAA DAMU.

Sulemani kwa uvuvio wa Roho alipewa kujua  kati ya mambo sita yanayomchukiza Mungu, mojawapo ni mikono imwagayo damu za watu.(Mithali 6:17).

Na sehemu nyingi sana katika maandiko utaona Bwana akiwakemea watu wake kwa dhambi hii ya umwagaji damu, kwamfano ukisoma hapa utaona anasema,

Isaya 1:15 “Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane”.

Soma na hapa pia;

Ezekieli 9:9 “Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, Bwana ameiacha nchi hii, naye Bwana haoni”.

Sehemu kadha wa kadha, Mungu alipowaona watu wake aliona damu nyingi mikononi mwao.. (Isaya 59:3, Yer 22:3, Eze 23:37, 45).

Sasa ni rahisi kudhani kuwa, katika mwili ni kweli walikuwa ni wauaji, wanawaua watu kwa siri au wanauana wao kwa wao ovyo . Hapana si kweli, Waisraeli hawakuwa hivyo. Kama tu vile walimwengu wengi wasasa walivyo leo.

Hivyo wenyewe hawakuelewa Mungu alikuwa anawaonaje matendo yao kwa jinsi ya Roho,

Hadi Bwana Yesu alipokuja kutufunulia  jambo hilo katika agano jipya Mungu alikuwa anamaanisha nini;

Tusome.

1Yohana 3:15 “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake”.

Akaeleza, kwa undani Zaidi, jinsi mtu wa namna hii ambaye, anamchukia ndugu yake, anavyostahili adhabu sawa tu na yule Mhalifu aliyemwaga damu ya mtu.

Mathayo 5:22 “Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Ndugu unayesoma haya maneno, tufahamu kuwa, tunaweza tukawa ni waombaji wazuri, ni waalimu wazuri, ni wasaidizi wazuri, ni wachungaji wazuri, lakini mbele za Mungu tukawa watu hatari sana, tukaonekana kama wahalifu sugu kabisa, ambao tumeuwa roho za watu wengi sana, mikono yetu inabubujika damu, tumeshika visu, na mapanga, na mashoka, tunaua, na bado tunaendelea kuua watu kila siku. Sababu ni nini? Sababu ni chuki zilizopo mioyoni mwetu kwa watu wengine.

Tunapokuwa na visasi na watu, au hasira, Mungu anatuona tunastahili jehanamu ya moto. Hata sadaka yetu tunayompelekea yeye bado anaiona ni chukizo kubwa sana, ndio maana asema tusiitoe mpaka tutakapopatana kwanza na majirani zetu.

Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,

24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako”.

Hivyo, tujifunze kuachilia, ili tusiwe wauaji, na njia pekee ya kuweza kuishinda hiyo hali, ni kuwa mtu wa kutafakari sana Neno la Mungu. Kwani Neno ni tiba, inayotupa maonyo,na Faraja na ushauri, ukiona hiyo hali inakushinda, fahamu kuwa kiwango chako cha utafakariji wa maandiko ni kidogo..

Lakini tunaposoma lile Neno mfano lile andiko linalosema, ndugu yako akikusoma, mara ngapi umsamehe.. Na Bwana akajibu na kusema, hata SABA MARA SABINI.. Yaani mara 490, kwa siku moja,(Mathayo 18:22) tutagundua ni nini maana ya msamaha.. Ni Zaidi ya vile tunavyofikiria, ni Zaidi ya kuachilia mambo yote, na kukubali kuonekana mjinga, ni Zaidi ya kukubaliana na kila hali. Hapo ndipo tutakapojua hakuna sababu ya kushikamana na kila jambo ndugu zetu au marafiki, au majirani zetu wanayotufanyia, au kutuudhi kwayo.

Kwasababu katika hayo yote hawajawahi kuyarudia mara 490, kwa siku, pengine ni mara mbili tu au kumi. Hivyo tunapaswa tusamehe.

Bwana atusaidie sana, mkono yetu iwe safi kama ya mwanakondoo wake Yesu Kristo.

Ndipo tutakapomkaribia Bwana wetu na kutubariki.

Ayubu  17:19 “Lakini mwenye haki ataishika njia yake, Naye mwenye mikono safi atazidi kupata nguvu”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

RACA

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU UPENDO.

Unyenyekevu ni nini?

JIFUNZE NAMNA YA KULITUMIA NENO LA MUNGU.

JE! DAMU INA UMUHIMU WOWOTE KATIKA MAISHA?

USIWE ADUI WA BWANA

MIAMBA YENYE HATARI.

Rudi nyumbani

Print this post