NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, libarikiwe.

Zipo njia nyingi za kuvuta rehema za Mungu, juu yako.. baadhi ya hizo ni kuwa Mwombaji, mtoaji, na mtu wa kusamehe.

Lakini ipo njia nyingine ambayo tukiijua basi, siku zote tutakuwa watu wa kupata rehema kutoka kwa Bwana na hata kama kuna mabaya tuliyofanya mbele za Mungu, basi anatusamehe na kughairi kutuadhibu.

Na njia hiyo si nyingine Zaidi ya “kutojilipiza kisasa” au kutofurahia “anguko la wanaofanya vita nawe”.

Watu wengi leo hususani Wakristo, wanakosa maarifa kwa kudhani kuwa Mungu anapendezwa sana na anguko la maadui zao. Hivyo kila siku, na kila saa wanawaombea shari maadui zao, na kila siku wanakaa wakisubiria anguko lao ili wafurahi.. (Kama vile Nabii Yona alivyokaa chini ya mtango, akingoja kuona Ninawi inaangamizwa).

Na hiyo yote ni kutokana na jinsi tulivyofundishwa au kujifunza. Pasipo kujua kuwa hayo sio mapenzi ya Mungu kabisa.. Ingekuwa Mungu ana hasira sana na adui yako, nadhani asingemuumba kabisa.. Lakini mpaka unamwona anaishi, jua ni mapenzi ya Mungu yeye awepo pale..

Sasa hebu tujifunze mstari ufuatao ili tuweze kuelewa vizuri..

Mithali 24:17 “Usifurahi adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”.

Umeona hapo?..Anasema usifurahi, ukimwona adui yako anaanguka!.. kwasababu Bwana kamwangusha kwa lengo la kumnyenyekeza na si kwa lengo la kumwangamiza kabisa!, kama wewe unavyofikiri..

Hivyo unaposhangilia anapoadhibiwa na Mungu, jambo hilo halimpendezi kabisa Mungu… na Bwana akiona unashangilia kuanguka kwake, basi anaghairi ule ubaya na kukugeukia wewe. (Kwasababu na wewe sio kwamba ni mkamilifu mbele zake, kwamba haustahili adhabu yoyote, unazo kasoro nyingi sana, isipokuwa Mungu ni mvumilivu kwako).

Vile vile, watu wanaofanya vita na wewe na kukushutumu, kukusengenya, kukulaumu, kukuudhi, kukuumiza, au hata kukutesa pasipo hatia yoyote, usijaribu kamwe kuwarudishia mabaya, wala kuwashitaki mbele za Mungu, wewe waombee rehema…na kubali mashutumu yao..Kwasababu kwa kufanya hivyo, Mungu, sio kwamba utakuona wewe ni mjinga mbele zake, kinyume chake utaonekana mwenye busara na hivyo utapata rehema Zaidi na kibali mbele zake.

Usichukizwe na laana watu wanazokulaani, kwasababu laana hizo kwako, ndio baraka kwako, mashutumu hayo unayoshutumiwa, Mungu anayasikiliza na yanamhuzisha, hivyo Bwana atakupa wewe rehema kwa mashutumu hayo, atakuhurumiwa kwa masengenyo hayo…N.k

Daudi aliijua hii siri, ndio maana kamwe hakuwahi kutoa Neno la laana kwa waliokuwa wanamlaani, wala hakuwahi kufurahia kuanguka kwa waliokuwa wanaitafuta roho yake, ndio maana utaona alilia sana, siku Sauli alipokufa, vile vile alilia sana Absalomu, mwanae alipokufa!..ambao hawa wote walifanyika maadui zake.

Sasa ni kwanini hakuwalaani waliokuwa wanamlaani?, ni kwasababu alijua KUWA KULAANIWA KWAKE NA WATU NDIO KUBARIKIWA KWAKE NA BWANA.

Utakumbuka wakati Fulani alipokuwa anamkimbia Mwanae Absalomu, alikutana na mtu mmoja aliyeitwa Shimei, mtu huyo alianza kumlaani, lakini Daudi hakurudisha laana hata moja, wala hakumwua ingawa alikuwa anao huo uwezo.

2 Samweli 16:5 “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; ALITOKA, AKALAANI ALIPOKUWA AKIENDA.

6 Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.

7 Na Shimei alipolaani, alisema hivi, NENDA ZAKO! NENDA ZAKO! EWE MTU WA DAMU! EWE MTU USIYEFAA!

8 Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya sauli ambaye umetawala badala yake; naye bwana ametia ufalme katika mkono wa absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.

9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.

10 Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?

11 Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? MWACHENI ALAANI, KWA SABABU BWANA NDIYE ALIYEMWAGIZA.

12 LABDA BWANA ATAYAANGALIA MABAYA YALIYONIPATA, NAYE BWANA ATANILIPA MEMA KWA SABABU YA KUNILAANI KWAKE LEO.

13 Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; SHIMEI NAYE AKAAENDELEA JUU YA UBAVU WA KILE KILIMA, KWA KUMKABILI, HUKU AKIENDELEA, AKILAANI, AKIMTUPIA MAWE, NA KURUSHA MAVUMBI”.

Je na sisi leo hii tunaweza kukubali mashutumu namna hii?.. kiasi kwamba wanaotusengenya na sisi hatuwarudishii masengenyo, wala kuwalaumu?.. kiasi kwamba tunahuzunika kuanguka kwa wanaoshindana nasi?

Tukifikia hatua hii tutapata kibali sana Mbele za Mungu. Unaona Daudi hapo baada ya kukubali mashutumu na laana anasema.. “MWACHENI ALAANI, KWA SABABU BWANA NDIYE ALIYEMWAGIZA.  LABDA BWANA ATAYAANGALIA MABAYA YALIYONIPATA, NAYE BWANA ATANILIPA MEMA KWA SABABU YA KUNILAANI KWAKE LEO. ”

Daudi alijua ili kupata Mema, hana budi kukubali laana, ili kupata kibali hana budi kukubali mashutumu. Na si Daudi peke yake, utaona pia na Ayubu, katika Maisha yake yote anasema hajawahi kufurahia anguko la wanaomchukia au wanaoshindana naye.. jambo lililomfanya apate kibali kikubwa sana mbele za Mungu, na kuonekana kuwa mkamilifu kuliko watu wote waliokuwepo chini ya jua katika kipindi chake..

Ayubu 31:29 “Kama nilifurahi kwa kuangamia kwake huyo aliyenichukia, Au kujitukuza alipopatikana na maovu;

30 (Naam, sikukiacha kinywa changu kufanya dhambi Kwa kuutaka uhai wake kwa kuapiza);”

Na sisi ili tupate rehema na kibali na baraka, na Mema kutoka kwa Mungu, hatuna budi kuwa kama Daudi na Ayubu..Ni kanuni inayoonekana kama ni ngumu, lakini ndio iliyokubalika mbele za Mungu. Injili za kupiga maadui, na kutwa kuchwa kushindana na maadui zako na kusubiria kuona shari yao ili ufurahie nataka nikuambie ni injili za kuzimu, ingawa kwa nje zinaonekana kama zina hekima.. Bwana Yesu Mkuu wa uzima alisema maneno haya..

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44 lakini mimi nawaambia, WAPENDENI ADUI ZENU, WAOMBEENI WANAOWAUDHI,

45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?”

Unataka Rehema?, unataka kibali?, unataka Mema kutoka kwa Mungu??.. huna budi kukubali mashutumu, kwasababu Kristo naye alikubali mashutumu na kejeli na kudharauliwa lakini sasa ana utukufu kuliko vitu vyote.

Bwana YESU ANARUDI!!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

VITA DHIDI YA MAADUI

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO.

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
7 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
2 years ago

Shalom mwalimu!hii ni moja kati ya tabia ambayo nimekuwa nayo kutokana na kujifunza na kufundishwa hivyo.Moja kati ya shauku na maombi yangu ilikuwa ni kuijua KWELI na kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda, MUNGU ananijibu pole pole na kugundua kuwa ile ambayo nimekuwa nikidhani ndiyo KWELI na wengi kuamini ndiyo KWELI kumbe sio kabisa.

M
M
2 years ago

Amen.Be blessed.

Getrude Charles
Getrude Charles
2 years ago

Amen, Barikiwa sana Mtumishi wa Mungu, hakika hili somo linafundisha kitu. Maana Injili ya kuteketeza na kutuma moto kwa maadui ndo ibada ya walokole walio wengi leo. Mungu awabariki sana na azidi kuwatumia kwa viwango vya juu zaidi. Amen

Getrude Charles
Getrude Charles
2 years ago

Amen, Barikiwa sana Mtumishi wa Mungu, hakika hili somo linafundisha kitu. Maana Injili ya kuteketeza na kutuma moto kwa ndo ibada ya walokole walio wengi leo. Mungu awabariki sana na azidi kuwatumia kwa viwango vya juu zaidi. Amen

Ulimbaga Knowledge
Ulimbaga Knowledge
2 years ago

Bwana YESU awabariki, nashukuru nimejifunza hakika.