MIKONO YENU IMEJAA DAMU.

MIKONO YENU IMEJAA DAMU.

Sulemani kwa uvuvio wa Roho alipewa kujua  kati ya mambo sita yanayomchukiza Mungu, mojawapo ni mikono imwagayo damu za watu.(Mithali 6:17).

Na sehemu nyingi sana katika maandiko utaona Bwana akiwakemea watu wake kwa dhambi hii ya umwagaji damu, kwamfano ukisoma hapa utaona anasema,

Isaya 1:15 “Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane”.

Soma na hapa pia;

Ezekieli 9:9 “Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, Bwana ameiacha nchi hii, naye Bwana haoni”.

Sehemu kadha wa kadha, Mungu alipowaona watu wake aliona damu nyingi mikononi mwao.. (Isaya 59:3, Yer 22:3, Eze 23:37, 45).

Sasa ni rahisi kudhani kuwa, katika mwili ni kweli walikuwa ni wauaji, wanawaua watu kwa siri au wanauana wao kwa wao ovyo . Hapana si kweli, Waisraeli hawakuwa hivyo. Kama tu vile walimwengu wengi wasasa walivyo leo.

Hivyo wenyewe hawakuelewa Mungu alikuwa anawaonaje matendo yao kwa jinsi ya Roho,

Hadi Bwana Yesu alipokuja kutufunulia  jambo hilo katika agano jipya Mungu alikuwa anamaanisha nini;

Tusome.

1Yohana 3:15 “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake”.

Akaeleza, kwa undani Zaidi, jinsi mtu wa namna hii ambaye, anamchukia ndugu yake, anavyostahili adhabu sawa tu na yule Mhalifu aliyemwaga damu ya mtu.

Mathayo 5:22 “Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Ndugu unayesoma haya maneno, tufahamu kuwa, tunaweza tukawa ni waombaji wazuri, ni waalimu wazuri, ni wasaidizi wazuri, ni wachungaji wazuri, lakini mbele za Mungu tukawa watu hatari sana, tukaonekana kama wahalifu sugu kabisa, ambao tumeuwa roho za watu wengi sana, mikono yetu inabubujika damu, tumeshika visu, na mapanga, na mashoka, tunaua, na bado tunaendelea kuua watu kila siku. Sababu ni nini? Sababu ni chuki zilizopo mioyoni mwetu kwa watu wengine.

Tunapokuwa na visasi na watu, au hasira, Mungu anatuona tunastahili jehanamu ya moto. Hata sadaka yetu tunayompelekea yeye bado anaiona ni chukizo kubwa sana, ndio maana asema tusiitoe mpaka tutakapopatana kwanza na majirani zetu.

Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,

24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako”.

Hivyo, tujifunze kuachilia, ili tusiwe wauaji, na njia pekee ya kuweza kuishinda hiyo hali, ni kuwa mtu wa kutafakari sana Neno la Mungu. Kwani Neno ni tiba, inayotupa maonyo,na Faraja na ushauri, ukiona hiyo hali inakushinda, fahamu kuwa kiwango chako cha utafakariji wa maandiko ni kidogo..

Lakini tunaposoma lile Neno mfano lile andiko linalosema, ndugu yako akikusoma, mara ngapi umsamehe.. Na Bwana akajibu na kusema, hata SABA MARA SABINI.. Yaani mara 490, kwa siku moja,(Mathayo 18:22) tutagundua ni nini maana ya msamaha.. Ni Zaidi ya vile tunavyofikiria, ni Zaidi ya kuachilia mambo yote, na kukubali kuonekana mjinga, ni Zaidi ya kukubaliana na kila hali. Hapo ndipo tutakapojua hakuna sababu ya kushikamana na kila jambo ndugu zetu au marafiki, au majirani zetu wanayotufanyia, au kutuudhi kwayo.

Kwasababu katika hayo yote hawajawahi kuyarudia mara 490, kwa siku, pengine ni mara mbili tu au kumi. Hivyo tunapaswa tusamehe.

Bwana atusaidie sana, mkono yetu iwe safi kama ya mwanakondoo wake Yesu Kristo.

Ndipo tutakapomkaribia Bwana wetu na kutubariki.

Ayubu  17:19 “Lakini mwenye haki ataishika njia yake, Naye mwenye mikono safi atazidi kupata nguvu”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

RACA

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU UPENDO.

Unyenyekevu ni nini?

JIFUNZE NAMNA YA KULITUMIA NENO LA MUNGU.

JE! DAMU INA UMUHIMU WOWOTE KATIKA MAISHA?

USIWE ADUI WA BWANA

MIAMBA YENYE HATARI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Getrude Charles
Getrude Charles
1 year ago

Amina, Mungu atusaidie sana. Kwa akili zetu hatuwezi.