Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe.
Karibu tujifunze Biblia,
Umewahi kujiuliza kwanini siku zote vita vya wanajeshi vinakuwaga ni vigumu? Haijalishi watakuwa wamevaa mavazi gani ya kujikinga na silaha na risasi, lakini bado vita huwa vinakuwa vigumu? Umewahi kujiuliza ni kwanini?
Ni kwasababu wale wanaokwenda kupambana nao wapo kama wao…Adui naye kashikilia silaha kama ya kwao, wamepitia mafunzo kama ya kwao, nao pia wamevaa mavazi ya kujikinga na risasi kama wao. Kwaufupi karibia kila kitu alilichonacho mwanajeshi adui yake naye anacho..Hapo ndipo unapokuja ugumu wa vita. Na sio tu katika vita, bali hata katika michezo wanaocheza watu wa kidunia..Michezo yao inakuwa ni migumu kwasababu wapinzani wao nao pia wamejiandaa kama wao, wana mbinu kama zao, na pia wana akili kama zao..
Na katika ulimwengu wa roho tunapaswa tulitambue hilo. Kwamba tupo vitani, na tunayepambana naye hayupo mikono mitupu, bali naye pia ni askari kama sisi.
Pale tunaposoma andiko la kwenye Waefeso 6:11 kwamba “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Maana yake ni kwamba shetani naye upande wa pili kashika silaha kama sisi. Angekuwa si askari kama sisi biblia isingetuambia tushike ngao, ngao ya nini kama unayepambana naye hana silaha kali? Unaona.
Kwaufupi katika ulimwengu wa roho, wote tunafanana kimwonekano…shetani na mapepo yake pamoja na sisi. Wote tumevaa silaha.
Ukizidi kusoma hiyo habari ya kwenye Waefeso utaona biblia inasema tukamate upanga wa roho ambao ni Neno la Mungu…sasa jambo la muhimu kufahamu ni kuwa upanga huo huo (yaani Neno la Mungu) shetani pia anao. Na upanga huo huo tunaotumia kumkata, ndio huo huo anaotumia na yeye kutukata sisi tusipokuwa watashi.
Utauliza ni wapi shetani amewahi kuwa na Neno la Mungu (na kulitumia hilo kumkata mtu wa Mungu)?
Kasome Luka 4:9-13, uone jinsi alivyolitumia kumshambulia Bwana kule jangwani.
Hivyo mwanajeshi wa kweli aliye vitani hafurahii tu kubeba bunduki au mkuki na kuvaa kijeshi, kwasababu anajua hata adui yake naye kashika bunduki kama yake, na anajua asipokuwa makini anaweza kufa na silaha zake mkononi, hivyo anachojiaminisha nacho ni UTASHI wa kutumia silaha yake, uwezo wa kukwepa, uwezo wa kukinga, na ushapu na ushupavu. Kwahivyo ndivyo atakavyomshinda adui yake, lakini akilala tu na kusema tayari ana bunduki mkononi, tayari amevaa nguo ya kuzuia risasi basi ni dhahiri huyo mwanajeshi anakwenda kufa huko.
Ndugu kama askari tusifurahie tu kulikariri Neno, bali tufurahie uwezo wa kulichambua vyema, kama aliokuwa nao Bwana Yesu…Kwasababu biblia inasema Neno la Mungu ni upanga ukatao kuwili, lina makali pande zote kama sime, maana yake pia adui yako akilishika anaweza kukudhuru nalo na ukakatikakatika kabisa.
Na kama tulivyotangulia kusema kuwa shetani na mapepo yake ni wanajeshi kama sisi, yamevaa makombati, na yanaouwezo mzuri wa kutumia silaha, hivyo ni ushapu wetu, na utashi wetu ndio utakaowashinda…Sasa utauliza ni wapi biblia inasema kwamba mapepo ni majeshi?
Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya MAJESHİ YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho”.
Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya MAJESHİ YA PEPO WABAYA katika ulimwengu wa roho”.
Hebu jiulize kwanini biblia haijatumia neno hapo “umati wa pepo wabaya” badala yake imetumia neno “jeshi”?.. maana yake ni kwamba haya maroho nayo yamevaa silaha na makombati, yapo vitani kupambana…hayapo hayapo tu!
Pia tunaweza kusoma andiko lingine linalozungumzia majeshi ya mapepo wabaya..katika Luka 8:30 “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, JİNA LANGU Nİ JESHİ; kwa sababu pepo wengi wamemwingia”
Kwanini yalipoulizwa majina yao, hayakusema “jina letu umati” badala yake yakasema “jeshi”?. Hiyo ni kuonyesha kuwa yapo vitani, yameshika silaha. Na sisi wakristo hatupaswi kulala, tunapaswa tusimame tushike silaha!. Na tuongeze utashi wa hali ya juu katika kutumia silaha (yaani Neno la Mungu).
Hivyo hatuna budi kuingia ndani sana katika kujifunza Neno la Mungu, na kuweza kulitumia. Bwana wetu Yesu alikuwa mfano mzuri…Shetani alikuja na Neno, lakini Bwana alikuwa na Neno zaidi ya lile..hivyo shetani alipomtupia ule upanga, Bwana aliukinga na kumkata kwa utashi aliokuwa nao wa kuweza kulitumia Neno.
Vivyo hivyo katika maisha na katika wokovu tuna vitu vingi sana, ambavyo shetani anatutesa navyo kwasababu tu hatujui jinsi ya kulitumia Neno vizuri(hatuna utashi, wala ushapu, wala uzoefu wa Neno). Neno tunalo, lakini jinsi ya kulitumia ndipo tunaposhindwa na hivyo adui shetani analitumia hilo hilo kutumaliza.
Sasa Ni kwa namna gani tutaweza kulitumia Neno vizuri ili kuzishinda hila za shetani? Ni kwa kujifunza kwa bidii Neno, na si kusoma tu!. Ipo tofauti kubwa sana ya kusoma na kujifunza Neno. Mtoto wa darasa la kwanza aliyejifunza kusoma leo…ukimpa kitabu cha biolojia cha kidato cha sita, anaweza kukisoma chote, na hata kukariri baadhi ya picha na vimaneno. Lakini hapo bado hajajifunza chochote…haijalishi kakariri mistari mingapi ya kitabu hicho.
Hivyo na sisi hatupaswi kuisoma biblia tu peke yake, bali tunapaswa tujifunze..Maana yake tunakaa chini tunasoma kitabu kimoja, na kukitafakari, na kwenda kutafuta zaidi huku na huko, maarifa juu ya hicho kitu, ili kukijazia nyama kile tulichokisoma. Na si kusoma mstari mmoja tu! Pasipo kuelewa kiini cha huo mstari toka juu, na kujisifu kwamba tunazo silaha.
Bwana atusaidie na kuzidi kutujaza Roho wake mtakatifu, ili tuweze kulitumia vyema neno lake.o
2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKİTUMİA KWA HALALİ NENO LA KWELİ”
Bwana atubariki.
Kama hujaokoka! Bwana Yesu yupo mlangoni kurudi.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Mbinguni ni sehemu gani?
ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO
Je! Kusoma biblia kwenye simu ukiwa kanisani ni dhambi?
ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.
Neno la Mungu ni upanga.
UPONYAJI WA ASILI
Rudi Nyumbani:
Print this post
Wonderful teacherings
Amen Ubarikiwe..