UVUVI BORA HAUCHAGUI, CHA KUVUA.

UVUVI BORA HAUCHAGUI, CHA KUVUA.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, utukufu na heshima vina yeye milele na milele.

Utajiuliza, ni kwanini wengi wa mitume wa Bwana Yesu walikuwa ni wavuvi? Tukiachilia mbali wale wanne (yaani Petro, Yakobo, Yohana, na Andrea, ambao kazi yao rasmi ilikuwa ni uvuvi), Kulikuwa na wengine watatu, ambao walikuwa wanaifanya pia hii kazi, kama sio kuwa na uzoefu nayo (Soma Yohana 21:1-3). Hivyo tunaweza kusema, si chini ya mitume saba (7), walikuwa ni wavuvi.

Utajiuliza Ni kwanini Bwana alipendelea sana wavuvi, na sio watoza ushuru wengi, ni kwasababu kazi yake ya kuokoa watu ilifanana na hiyo, na ndio maana akamwambia Petro tangu sasa nitakufanya kuwa mvuvi wa watu, hakumwambia nitakufanya kuwa muhubiri wa watu, hapana bali mvuvi wa watu. Kuonyesha kuwa maarifa ya uvuvi, yana mchango mkubwa sana, katika kuokoa roho za watu.

Sasa tabia mojawapo ya mvuvi, ni kuwa hachagui cha kuvua pindi anapotupa nyavu yake baharini, huwa kichani pake anajua kabisa, vitakavyokuja juu, sio  Samaki tu peke yake, bali pia na viumbe vingine vingi vya majini, Pamoja na takataka nyingi.

Ndio maana Bwana Yesu alitoa mfano huu, akasema;

Mathayo 13:47 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

48 hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa”.

Umeona? Samaki waliovuliwa, inaweza ikawa ni asilimia 20 tu, lakini 80 yote iliyobakia, ni konokono, kobe, nyoka, magugu, minyoo n.k.

Hivyo akishafika ufukweni, kazi yake inakuwa ni kukusanya Samaki, lakini hao wengine anawatupa, kesho tena anaendelea na uvuvi wake huo huo, anatoa tena vitu kama hivyo. Lakini hilo halimfanyi akate tamaa. Kwasababu Neti/Nyavu yake ndio ilivyotengenezwa, kuvua kila kitu.

Anajua ndio hali halisi ilivyo.

Kuonyesha kuwa na sisi kama wavuvi wa rohoni, tunaowahubiria watu Habari njema ili waokoke, si kazi yetu, kuchunguza chunguza kama huyu ni wa Mungu kweli au sio, ukifanya hivyo, utakata tamaa mapema. Watu mia, utakaowahubiria Kristo, pengine ni kumi tu, wakawa na matokeo unayoyatazamia.

Kinyume chake wengine ndio wanakuwa mwiba kwako, badala ya faraja. Bwana Yesu alipochagua mitume wake, mmoja wao alikuwa mwizi na msaliti, Lakini hiyo haikumaanisha kuwa hakuwa makini katika uchaguzi wake, au alifanya hitilafu. Hapana, neti yake ilikuwa bora kabisa.

Vivyo hivyo na wewe ndugu, ikiwa upo katika kazi ya uvuvi wa watu wa Mungu, basi leweke akilini, hilo, utumishi wa kweli wa Mungu hauchagui, cha kuvua. Si kila utakayemshuhudia, atapokea ujumbe wako, hivyo usikate tamaa ukadhani kuwa kuna dosari katika utumishi wako, hapana, bali, ndivyo uvuvi ulivyo. Endelea kuwashuhudia wengine, ukijua kabisa kati ya mia hutakosa wachache watakaoponyeka. Na hao ndio Samaki.

Bwana alitaka hilo likae katika vichwa vya mitume wake,kabla ya kazi kuanza, ili wasikatishwe tamaa katika shamba la Bwana, pindi wakutanapo na wasivyovitarajia.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Juya ni nini kwenye biblia? (Mathayo 13:47)

TENGENEZA  NYAVU ZAKO, OSHA NYAVU ZAKO.

CHAMBO ILIYO BORA.

Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.

Nini maana ya kuokoka katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Magdalena
Magdalena
2 years ago

Bwana Yesu azidi kuinua Huduma hii iwafikie wengi zaidi,