NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

Unaweza ukajiuliza Je shetani anaweza kuwazuia watu wasihubiri injili?

Jibu ni ndio Tusome,

1 Wathesalonike 2:17 “Lakini ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.

18 Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia”.

Kulingana na maneno hayo ya Mtume Paulo, ni wazi kuwa shetani anahusika pakubwa sana katika kuizuia injili.

Siku zote shetani ni adui wa injili hakuna mahali alishawahi kukubaliana na watu kuipeleka injili. Hataki injili ihubiriwe kwasababa anajua ni uweza wa Mungu uletao wokovu. (Warumi 1:16).

Na yeye hataki kamwe watu wapate wokovu, anataka wasiisikie injili ili wafe katika dhambi zao na wajikute katika hukumu kama yeye siku ile ya mwisho.
Kwahivyo atafanya juu chini aizuie injili.
Sasa swali anaizuiaje?.

Anaizuia kwa kunyanyua matukio ambayo yataikwamisha safari ya kwenda kuhubiri.
Kwamfano akina Paulo labda walipanga kwenda huko Thesalonike lakini tarehe walizopanga kwenda hakukuwa na mashua za kuelekea huko au tufani zilianza kiasi kwamba haiwezekani kuanza safari kwa kipindi hicho.

Au wakati wameanza tu safari kufika maili kadhaa mbelen baharini ikachafuka, jahazi likavunjika, hivyo safari kuishia pale.

Au unakuta wamepanga safari vizuri tu inatokea wanapoteza nauli au wanaibiwa, hivyo safari inakuwa imeisha hapo.
Au wamepanga safari, ghafla mmojawao anaugua n.k.

Hayo ndio mambo shetani anayoyafanya kuizuia injili, na zaidi ya yote Mtume Paulo mwenyewe aliyashuhudia hayo mambo wanayokutana nayo katika safari zao za kwenda kuhubiri.

2 Wakorintho 11:25 “Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;

26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;

27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi”.

Mambo hayo pia yaliwatokea wanafunzi wa Bwana Yesu walipokuwa wanavuka kwenda nchi ya Wagerasi, wakiwa katikati ya safari baharini, shetani alijaribu kuwazuia kwa kuwaletea tufani kubwa, shetani alitaka kuwazuia kwasababu aliona kuna watu wawili kule nga’ambo wenye pepo wanaishi makaburini, wanakwenda kufunguliwa, hivyo hilo jambo hawezi kuliruhusu, ndipo akawaletea tufani njiani, mpaka Bwana alipoamka na kuinyamazisha.(Mathayo 8:23-34).

Hivyo kilichomtokea Paulo na Wanafunzi wa Bwana Yesu kinaweza kumtokea mhubiri yeyote yule, haijalishi umeitwa kwa wito gani kamwe shetani hawezi kuruhusu wewe uhubiri injili kirahisi, ni lazima atakupinga tu.

Sasa swali kama hivyo ndivyo tunapaswa tufanyeje kila tunapotaka kwenda kuhibiri injili?.

Bwana Yesu alitupa dawa ya kuepukana na majaribu ya namna hiyo, na hiyo si nyingine zaidi ya kuomba kwa bidii.
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake mara kadhaa waombe ili wasije wakaingia majaribuni, kwasababu alijua silaha moja kubwa ya kudhoofisha vizuizi vya shetani ni kuomba, ndio maana ijapokuwa yeye mwenyewe alikuwa ni Mungu lakini alikuwa anakesha kuomba, ili kutufundisha sisi.

Na jukumu la kuomba sio tu la Mhubiri, au mchungaji, au Muinjilisti, au Mtume.

Jukumu la kuomba ni la kila mtu aliye mkristo, kila mtu anapaswa kuiombea ili injili iweze kupelekwa bila kizuizi chochote, unapotenga muda na kuiombea injili ya Bwana Yesu, hujui ni mchango gani mkubwa uliouchangia.. Kwa kuomba kwako huko unaharibu mipango ya shetani ya kumvunjia jahazi mhubiri fulani mahali fulani.

Kwa kufunga kwako kuiombea injili ya Bwana Yesu, umeharibu mipango ya wizi na magonjwa shetani aliyoipanga juu ya wahubiri fulani waliopanga kwenda kupeleka injili mahali fulani. Hivyo na wewe unakuwa ni mojawapo ya jeshi la Bwana katika kuipeleka injili mbele.

Lakini ukiacha tu na kusema.. Aaah mimi sio mhubiri, sio muinjilisti hiyo sio karama yangu, huombi, hufungi, huchangii, hufanyi chochote, basi fahamu kuwa unaupa nguvu ufalme wa giza.

Ndio maana Mtume Paulo baada ya kuwaandikia waraka hawa Wathesalonike kwamba ameshindwa kuja kwao shetani kamzuia, alimalizia na kuwaambia hao Wathesalonike kwamba WAMWOMBEE.

Wasikae tu wakasubiri, kwani vita ni vikali.

1 Wathesalonike 5:24 “Ndugu, tuombeeni”

Na zaidi ya yote katika waraka wake wa pili aliwakumbusha tena jambo hilo hilo..

2 Wathesalonike 3:1 “Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu ”.

Je na wewe unaiombea Injili ya Bwana Yesu?.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Ni madhara gani yatampata mtu yule anayetafsiri Neno isivyopaswa!

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Matoazi na Matari ni nini? (Kutoka 15:20)

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amen