Kwanini Mungu anajifanya kama hajui mambo?

Kwanini Mungu anajifanya kama hajui mambo?

Kwamfano ile habari ya Kaini utaona Bwana anamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?


Tofauti na tunavyomchukulia Mungu kuwa ni Mkuu sana, hana haja ya kuambiwa chochote wala kujuzwa jambo, lakini kiuhalisia Mungu mwenyewe hajachagua kujiweka katika hiyo nafasi, tabia ya Mungu ni unyenyekevu.

Ijapokuwa anajua kila kitu, lakini wakati mwingine anajishusha kana kwamba hajui,
Vile vile ijapokuwa anauweledi na hakuna anayeweza kumshauri lakini wakati mwingine anajishusha na kukubali mashauri ya viumbe wake.

Kwamfano utaona Mungu anakubali ushauri wa Musa mara kadhaa.

Kutoka 32:9 “Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu

10 basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.

11 Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?

12 Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako.

13 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.

14 Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake”.

Kadhalika ijapokuwa Bwana anafahamu kila kitu, lakini utaona kuna wakati anajishusha na kuanza kufanya uchunguzi wa jambo mpaka analivumbua, utalithibitisha hilo katika kile kitabu cha Ayubu 28, wakati anafanya uchunguzi wa kuitafuta hekima.

Vile vile ijapokuwa anatujua wanadamu wote na matendo yetu lakini utaona kuna wakati anajishusha na kuanza utafiti kama mwanadamu kupima kiwango cha maovu duniani, utalithibitisha hilo kipindi anataka kuiangamiza Sodoma na Ghomora, kabla ya maangamizi alishuka katika mwili na kwenda kuhakiki mwenyewe kama kweli yaliyomfikia juu ndio hayo yanayoendelea chini..

Mwanzo 18:20 “BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,

21 basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua”.

Na sehemu nyingine nyingi ni hivyo hivyo. Utaona Mungu anajishusha na kuonesha tabia kama za mwanadamu, anajifanya dhaifu.. Ukitafakari sana unaweza kuona ni kama jambo lisilokuwa na maana, ni kama upumbavu hivi, lakini biblia inasema…

1 Wakorintho 1:25 “…. upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu”

Mungu amejifanya kama mdhaifu kwetu, kwa faida yetu sisi na si yake.

Hebu tafakari leo hii Mungu asingejishusha na kuuvaa mwili unaiotwa Yesu, leo hii tungekuwaje?, tungemwabuduje?, tungemwelewaje, Tungepata wapi nguvu ya kumtumikia?.

Tungesema Mungu hajui maumivu yetu, hajui shida zetu, hajui mzigo aliotutwika, hajui tabu tunazozipitia, yeye ni diktekta.

Lakini yeye Mungu mwenyewe naye alijishusha na kuwa mwanadamu, na yeye akapitia umaskini, na yeye anakipitia kujifunza, na yeye akapitia kutukanwa, na yeye akapitia kudhihakiwa na kukataliwa na kuumizwa na hata kifo ili atupe tumaini sisi.

Ili pale anaposema kwamba anayajua maumivu yetu, tufahamu kuwa ni kweli anayajua, anaposema anaujua umaskini wetu tujue ni kweli anamaanisha kuujua kwasababu na yeye aliupitia, anaposema anazijua tabu zetu, iwe kweli kwasababu naye pia alizipitia alipokuwa duniani.

Anaposema atatufufua tujue ni kweli kwasababu naye pia alikufa na kuona kifo hakimstahili mtu yeyote wa Mungu.

Hivyo udhaifu wake ni faida kubwa sana kwetu, una nguvu kuliko hekima zetu, Hekima zetu zingesema Mungu hawezi kujishusha kama mwanadamu.

Wafilipi 2:4 “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”.

Ni nini tunachoweza kujifunza kwa Bwana?

Kama Mungu alivyo mnyenyekevu kwa faida yetu sisi, kadhalika na sisi hatuna budi kuwa wanyenyekevu kwa faida ya wengine.

Hapo mstari wa 5 maandiko yanasema “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu”.

Umeona?..Nia ya Kristo ni kujishusha kwa faida yetu, na sisi hatuna budi kuwa hivyo hivyo..

1 Petro 5:5 “…Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

UPUMBAVU WA MUNGU.

Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)

MJUE SANA YESU KRISTO.

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amina