by Admin | 21 May 2022 08:46 pm05
Hebu tusome Habari ifuatayo kwa utaratibu halafu tutafakari Pamoja…
Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona”.
Hayo ni maneno ya Bwana Yesu aliyowaambia watu wa kanisa la Laodikia, ambalo kanisa hilo kiroho ni sisi wakristo wa siku hizi za mwisho.
Utaona anawashutumu watu wa kanisa hilo na kuwaambia kuwa WANAJIOTA KUWA NI MATAJIRI, kumbe ni MASKINI. Lakini Pamoja na hayo utaona anawashauri wakanunue kwake DHAHABU ili wawe matajiri!!!
Sasa swali la kujiuliza hapo, ni lini MTU AKINUNUA DHAHABU ANAKUWA TAJIRI??.. Ni heri angesema NJOO NIKUPE DHAHABU BURE!, Lakini yeye anasema NJOO UNUNUE!..Maana yake unatoa kitu ili uipate hiyo dhahabu.
Na kama wewe ni mtafakariji mzuri wa Maandiko utaona Bwana Yesu alichokuwa anakimaanisha hapo, ni kwamba ukainunue dhahabu hiyo kwake, kwa bei ya chini, na kisha ukaiuze kwa bei kubwa ILI UPATE FAIDA UWE TAJIRI. (Ndicho alichokuwa anakimaanisha hapo!).
Sasa tatizo ndio liko hapo, kutoa gharama kuinunua hiyo dhahabu iliyosafishwa kwa Moto. Ingekuwa ni bure wengi wangeenda kuichukua tu!.. lakini Bwana anaiuza!..na inahitajika gharama kuinunua. Sasa swali gharama hiyo ni ipi?
Gharama hiyo tunaisoma katika mfano mmoja Bwana alioutoa katika kitabu cha Mathayo Mlango wa 13.
Tusome..
Mathayo 13:45 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua”.
Lulu, ni kama dhahabu tu kwa gharama, kwasababu zinakaribiana thamani!.. Kwahiyo ni sawa kusema “ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara aliyeona dhahabu nzuri au lulu nzuri akaenda akauza alivyonavyo vyote, akainunua”
Sasa kumbuka huyu ni mfanya biashara, lengo lake ni apate faida awe Tajiri, hivyo katika pitapita zake akakutana na lulu mahali Fulani ambayo inauzwa kwa bei ya chini, na yeye anajua soko la mahali inapouzwa kwa bei ya juu.. na akaona endapo akienda kuinunua kwa bei hiyo ya chini na kwenda kuiuza kwenye soko la juu atapata faida nyingi sana…sasa kwa busara akaenda kuuza shamba lake, na vyote alivyonavyo ili aipate fedha ya kutosha kuinunua hiyo lulu inayouzwa kwa bei ya chini… Lengo la kwamba atakapoenda kuiuza kwa bei ya juu itamrudishia fedha ya kutosha ya kununua vyote alivyovipoteza na Zaidi sana kubakiwa na faida nyingi.
SASA UMEONA GHARAMA HIYO?
Maana yake kama hatakubali kuuza vyote alivyonavyo ili apate fedha za kuinunua hiyo Lulu hataweza kuinunua na ataendelea kuwa maskini hivyo hivyo hata kama anajiona hana mahitaji yoyote…
Ndicho Bwana Yesu alichokuwa anamaanisha hapo katika hiyo Habari ya dhahabu.. Kwamba mtu yeyote akitaka kuwa Tajiri basi aende kwake akanunue dhahabu hiyo, kwa bei ya chini, ili akaiuze kwa bei ya juu, na kubakiwa na faida ambayo ndio utajiri wenyewe.
Sasa mfano huo kiroho inamaanisha nini?
Tukitaka kuupata ufalme wa mbinguni ambao ndio unaofananishwa na Dhahabu na Lulu. Hatuna budi kuacha vyote tulivyonavyo vinavyozuia sisi kuupata huo uzima wa milele (Hiyo Ndio maana ya kuuza vyote na kwenda kuinunua lulu/dhabahu).
Tukishaacha vyote yaani Ulevi wetu, uongo wetu, wizi wetu, anasa zetu, kiburi chetu, uasherati wetu, umaarufu wetu, ujuzi wetu ambao unatuletea kiburi, ujuaji wetu, na biashara zetu haramu, kama za madawa ya kulevya, au uuzaji wa pombe, au utapeli au rushwa n.k Tunapoviacha hivi vyote, na kumfuata Yesu hapo ni sawa na tumeuza vyote, na katika viwango vya kimbinguni tumejipatia credit tosha za kuupata Ufalme wa mbinguni (ambao ndio unaofananishwa na ile lulu au dhahabu safi).
Mathayo 19:20 “Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni”.
Umeona gharama za kuinunua ile DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO!!!.. Suluhisho ni kuacha vyote, kuvitoa ndani ya moyo wako..
Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
Unaacha vyote na kumfuata Yesu kama ulivyo.. Bwana Yesu anawapenda watu wanyenyekevu, ambao wameamua kabisa kuanza moja katika Maisha yao, ambao wamejikana nafsi, ambao wamedhamiria kabisa kuzaliwa upya.. Leo Bwana anakuita, anataka akutumie kama chombo kipya, hivyo vua ujuzi wako leo, vua kiburi chako, acha dhambi zako, na mambo yote yanayokusonga na mfuate…naye atakupenda!, na kukupa zawadi ya Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia katika kushinda dhambi, na kukufanya kuwa mtumishi wake..
Usijione kuwa ni Tajiri, na huna haja ya kitu!.. (usiojione kuwa humhitaji Yesu kwa sasa) bado unamuhitaji sana, bado unaihitaji ile Dhahabu.. nenda kainunue kwa Bwana, kwasababu inapatikana kwa bei ya chini.. na ukiinunua na kwenda kuifanyia biashara, yaani kuwafundisha wengine Habari za ufalme wa mbinguni, utakuwa Tajiri sana katika ufalme wa mbinguni.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.
VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.
HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/05/21/kwa-kuwa-wasema-mimi-ni-tajiri/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.