Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

Tukisoma katika kitabu cha Ezekieli 14:9 tunasoma Mungu anaweza kumdanganya Nabii, sasa swali ni je Mungu anadanganya?

Jibu: Tusome

Ezekieli 14:9 “Na nabii akidanganyika, na kusema neno, MIMI, BWANA, NIMEMDANGANYA NABII YULE, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

10 Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno”

Kufuatia mstari huo ni rahisi kuamini kuwa Mungu anadanganya… lakini kiuhalisia ni kwaba, Mungu kamwe hawezi kudanganya na wala hasemi uongo!.. Yeye ni mtakatifu siku zote.. Isipokuwa Mungu anaweza kuruhusu roho ya upotevu kutoka kwa adui imwingine mtu,  endapo mtu huyo atayakataa mema na kulazimisha mabaya katika maisha yake, ndivyo maandiko yanavyosema katika 2Wathesalonike 2

2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Sasa ili tuelewe vizuri Mungu anaiachiaje nguvu ya upotevu juu ya mtu, hebu tusome kisa kimoja cha Mfalme Ahabu katika maandiko..

1Wafalme 22:16 “Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?

17 Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

19 Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.

20 Bwana akasema, NI NANI ATAKAYEMDANGANYA AHABU, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.

22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.

23 Basi angalia, BWANA AMETIA PEPO WA UONGO KINYWANI MWA MANABII WAKO HAWA WOTE; NAYE BWANA AMENENA MABAYA JUU YAKO”.

Umeona hapo?..Mfalme Ahabu alikuwa amemwacha Mungu na alikuwa anaabudu miungu na wala alikuwa hana mpango wa kubadili njia yake, na wakati huo huo anakwenda kumwuliza Mungu kwa habari ya vita iliyo mbele yake, huku moyoni amemwacha Bwana, yaani kwaufupi alikuwa anamgeuza Mungu kama mganga wa kienyeji kumtabiria mambo yake ya vita tu!

Lakini hapo tunasoma Mungu yeye mwenyewe hakumdanganya Ahabu, kwasababu yeye hasemi uongo, lakini aliiachia roho ya upotevu imfuate mfalme Ahabu.. Maana yake Mungu aliruhusu pepo liwaingie manabii wake 400, na kuwapa maono ya uongo, na kufikiri ni maono ya Mungu… Na hivyo Mfalme akadanganyika na maono yale na akaenda kufa katika vita badala ya kupona. Hivyo ni pepo ndilo lililomdanganya Ahabu na si Mungu, ingawa Mungu ndiye aliyeruhusu..hivyo ni sawa na kusema ni Mungu kamdanganya Ahabu..

Kama vile maandiko  yanavyosema kuwa Mungu alimpiga Ayubu.. lakini kiuhalisia si Mungu aliyempiga bali ni shetani, isipokuwa kwa ruhusa ya Mungu..

Ndicho biblia pia ilichomaanisha hapo katika  Ezekieli 14:9 “Na nabii akidanganyika, na kusema neno, MIMI, BWANA, NIMEMDANGANYA NABII YULE”.

Maana yake ni kwamba kama Nabii kamwacha Bwana moyoni mwake, Mungu anaweza kuruhusu pepo la uongo limwingie na kumpa maono ya uongo.. Sasa kitendo hicho cha Bwana kuruhusu upotevu umwingie mtu, ndio unaweza kutafsirika kama Bwana kamdanganya mtu huyo!.. Lakini kiuhalisia si Bwana aliyemdanganya bali ni mapepo ambayo yameruhusiwa na Mungu yamwingie na kumdanganya huyo mtu.

Sio jambo la ajabu pia Mungu anaweza kumuua mtu kwa kumweka mikononi mwa shetani..

Hivyo tunachoweza kujifunza ni kwamba hatuna budi kuwa makini sana na kutomgeuza Mungu kama waganga wa miungu ya kidunia, ambao unaweza kuwafuata wakutatulie matatizo yako,  na kuondoka kuendelea kuishi maisha yako ya ulevi, ya uzinzi, au mengine yoyote.

Kwa Mungu wa mbingu na nchi sio hivyo, tunapomwendea hatuna budi kumkubali kwanza, na kujinyenyekeza chini yake na kufuata kile anachokitaka yeye katika maisha yetu, na si kile tunachokitaka sisi.. Maana yake ni kwamba tunapomwendea Mungu kumuuliza jambo na huku mioyoni mwetu bado tunapenda ulevi, na hatutaki kuacha, bado tunaabudu sanamu, bado ni wachawi, bado ni wazinzi n.k Bwana ataachia nguvu ya upotevu, kwasababu yeye hadhihakiwi alisema hivyo katika neno lake..

Ezekieli 14:1 “Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.

2 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,

3 Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?

4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake;

5 ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao”.

Kama hujaokoka!, kumbuka kuwa Kristo ndiye njia kweli na Uzima, na hakuna njia nyingine ya kumfikia Baba zaidi yake yeye. Hivyo wote hatuna budi kumwamini na kumpokea ili tupate wokovu na ondoleo la dhambi zetu, na tunapata wokovu kwa kumwamini, na kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Bwana Yesu Kristo. Na Roho Mtakatifu atayakeyeingia ndani yetu atatuongoza katika kweli yote.

Marana tha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

MUNGU ATAKUUA UKIWA MBAYA MACHONI PAKE.

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments