YAKINI NA BOAZI.

YAKINI NA BOAZI.

Shalom, jina la Bwana wetu libarikiwe daima.

Neno linatuambia..

“Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.

Ni mpya kila siku asubuhi..” (Maombolezo 3:22-23).

Na wewe usomaye ujumbe huu rehema za Bwana zisikome juu yako daima.

Leo tutajifunza kwa ufupi, mambo machache ya kuzingatia tunapokwenda nyumbani kwa Bwana aidha kuzungumza naye, au kumwabudu, inaweza ikawa ni kanisani, au kwenye semina, au popote pale unapoweza kumfanyia Mungu ibada.

Kama tunavyosoma katika agano la kale tunaona kuna wakati ulifika wa Sulemani kumjengea Mungu Nyumba (Hekalu) ambalo lingekuwa ni kitovu cha waisraeli wote, na mataifa yote ulimwenguni kumwabudia Mungu , na kufanyiwa upatanisho wa makosa yao kwa wakati ule.. Kama tunavyojua hekalu lile lilijengwa kwa kipindi cha Miaka 7, na katika ujenzi ule, kulikuwa na vigezo vingi sana  vya kuzingatia, pamoja na vipimo. Na kila kitu kilichotengenezwa kule kilikuwa kilikuwa kinafunua jambo kubwa sana rohoni kwa kanisa la Sasa, wale makerudi waliowekwa kule walikuwa wanafunua jambo Fulani rohoni, vile vinara 7 vya taa, vilivyokuwa na maana yake pia, halikadhalika zile madhabahu za dhahabu na za shaba , zote zilikuwa na maana, na lile sanduku la agano, mpaka yale mapambo yaliyokuwa kule ndani.

Sasa, karibu na mwisho kabisa wa ujenzi ule, Sulemani aliongozwa kujenga vitu vingine viwili muhimu katika hekalu, navyo si vingine Zaidi ya  nguzo kubwa mbili zilizosimama katika maingilio ya  Hekalu. Nguzo hizo zilikuwa ni ndefu na pana..

Nguzo ya kwanza iliwekwa upande wa kulia mwa kuingilia hekaluni, Na nguzo pili iliwekwa upande wa kushoto.

Ile iliyokuwa upande wa Kulia iliitwa YAKINI.. Na ile iliyowekwa upande wa kushoto iliitwa BOAZI.

2Nyakati 3:17 “Akazisimamisha nguzo hizo mbele ya hekalu, moja upande wa kuume, na ya pili upande wa kushoto; akaliita jina la ile ya kuume Yakini, na jina la ile ya kushoto Boazi”

Sasa maana ya maneno hayo ni hii:

Yakini ni:  IMEDHANIWA KUWA ATATHIBITISHA.

Na Boazi: IMEDHANIWA KUWA IMO NGUVU.

Kulikuwa hakuna namna yoyote kuhani aingie hekaluni, apitilize mpaka patakatifu pa patakatifu, kwenda kufanya mambo ya ibada asipite katikati ya hizo nguzo mbili. Zilikuwa kama mihimili ya hekalu.

Ikifunua kuwa yeyote atakayeingia kule avukapo nguzo hizo ni lazima jambo hilo liwe kichwani mwake, kuwa Mungu atathibitisha(Yakini), Na humo humo ndani pia ipo nguvu ya Mungu (Boazi).

Hivyo kuhani akiingia mule, kwa shughuli yoyote ile aidha ya upatanisho au ya kuwasilisha maombi ya watakatifu, kichwani mwake anauhakika kuwa ni lazima Mungu ajibu maombi yao yaani alithibitishe agano lake alioingia nao kwa kupitia Ibrahimu, Na vilevile anajua kuwa nguvu ya Mungu ipo mule, kwahiyo ni lazima awe makini kwa atayayafanya vinginevyo atakuwa anajitafutia kifo mwenyewe au hata matatizo kwa wana wa Israeli wote.

Nguzo hizo zilisimama kwa wakati wote hekalu lilipokuwepo.

Lakini Ni ujumbe gani tunapewa kwa agano jipya?

Biblia inafananisha kanisa la Kristo kama hekalu la Mungu, tunapotoka na kwenda nyumbani mwake au uweponi mwake, Sisi wote tunaenda kuwa kama makuhani wa Mungu, hivyo Bwana anataka kila mmoja wetu, ajue kuwa nguzo hizo mbili (yaani Yakini na Boazi) zimesimama mbele ya hekalu lake takatifu.

Anataka tujue kuwa tunapokwenda nyumbani mwake tufahamu kuwa Mungu yupo pale, ili kulithibitisha agano lake aliloingia na watakatifu kupitia Yesu Kristo.. Na kwamba unapokwenda kusali, au kumwabudu au kumwomba chochote, yupo pale kukusikia na kukujibu maombi yako, sawasawa na maneno ya Kristo (Yohana 14:13) Huo ni uhakika, Hivyo uingie ukijua jambo hilo kichwani kuwa Mungu ni Mungu mshika maagano.

Vilevile anataka ujue kuwa ipo nguvu yake kule ndani, Hivyo uwe makini pia usiende kidunia/kimazoea.. Wapo watu wanajiamulia tu kuingia kanisani wanavyotaka na mavazi yao kizinzi, wanaingia kanisani na vimini, na suruali, wakidhani kule wanaenda kukutana na miungu isivyoweza kufanya jambo lolote. Hawajua jengo likishaitwa kanisa, Au nyumba ya Mungu, tayari nguzo mojawapo itwayo Boazi imesimama pale nje!, yaani ndani imo nguvu kubwa sana ya Mungu, inayoua na kuhuisha.

Kwahiyo pale mtu anapoingia bila heshima, anakuwa anajitafutia mwenyewe laana..Hilo unapaswa ulijue hili binti wa Mungu, hilo unapaswa ujue kijana,.Unapokwenda kanisani, halafu unajua jana umetoka kuzini, na wakati huo huo unakwenda kushiriki meza ya Bwana,..Unajitafutia matatizo yako mwenyewe..(Soma hapa uone laana iliyowapata watu wa dizaini hiyo katika kanisa la Kristo IWakorintho 11:27-34)

Nyumba ya Mungu, si ya kuifanyia mzaha hata kidogo..

Marko 11:17 “Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi”.

Hivyo ndugu kama wewe ni mkristo,  zingatia hayo mambo mawili, yaweke kichwani mwako daima Nyumbani mwake Mungu anathibitisha, na nyumbani mwake imo nguvu. (Yakini na Boazi)

Bwana akubariki.

Ikiwa hujaokoka, kumbuka leo tena tumepiga hatua nyingine ya kuukaribia ule mwisho, pengine itakuwa leo, au kesho asubuhi, au wiki hii au vyovyote vile, hatuhitaji kuishi maisha ya kubahatisha, hivyo tukiyajua hayo, ni wakati wa kuamka usingizini, na kuzisafisha taa zetu.. Mpe leo Kristo maisha yako ayaokoe. Ufanyike kuwa mwana wake.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

KUOTA UMEFUNGA NDOA.

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

IFANYE KAZI YA MUNGU PASIPO HOFU!

AHADI ZA MUNGU.

POPOBAWA NI KWELI YUPO?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments